Fitina, utawala mbovu, majungu, vinaua soka nchini

07Mar 2016
Romana Mallya
Nipashe
Fitina, utawala mbovu, majungu, vinaua soka nchini

KWA muda mrefu soka la Tanzania limekuwa likilalamikiwa kuwa ni ‘kichwa cha wendawazimu’ kutokana na matokeo mabaya ya timu zake kongwe kitaifa na kimataifa.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye

Licha ya timu kongwe Simba na Yanga mara kadhaa kuvuka mipaka kusaka makocha wa kimataifa wakiamini ndio wenye uwezo wa kulivusha soka letu, lakini mwisho wa siku, wameishia kuwatimua mara timu hizo zinapoboronga katika ligi.

Hali hiyo pia imezikumba timu nyingine hapa nchini na kusababisha kulidumaza soka la Tanzania ambalo sasa limeishia kuwa la ‘hapa hapa’.

Mtafiti mzalendo wa soka, Dennis Manumbu, amefanya tafiti ambazo anaamini Serikali, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na klabu ikiwa zitautumia soka litapiga hatua.

Manumbu anaamini njia pekee ya kulinusuru soka ni kufanya tafiti kubaini changamoto, kuwasilisha matokeo yake kwa wadau ili yajadiliwe kwa pamoja na kufikia maazimio ya nini kifanyike.

Mtafiti huyu ana elimu ya soka ngazi ya stashahada kutoka Chuo cha South Amptoncha cha Uingereza na sasa anasoma Shahada ya Uzamili katika ufundishaji soka kwa njia huria.

Kabla ya kujiunga na chuo cha Uingereza, alikuwa na elimu ya soka ngazi ya cheti aliyoipata Chuo cha Michezo cha Malya lakini pia ana kiwango cha Shahada ya Uzamili katika Sayansi kutoka Chuo Kikuu cha Nelson Mandela mjini Arusha.

Kuhusu tafiti anasema amefanikiwa kuzifanya katika nyanja tofauti na nyingine zimesajiliwa katika majarida mbalimbali.
Mbali ya kuwa na taaluma ya michezo, amewahi kuzichezea timu mbalimbali ambazo ni Sifa United na Livingstone za Manzese, Takukuru Sports Club na African Sports ya Tanga.

Pia amewahi kuwa kocha wa timu za mpira wa miguu za Vijana Handeni, Warumba Urambo, timu ya Wilaya ya Urambo, Wilaya ya Kilwa na Takukuru Sports Club.

MAANDALIZI YA WANASOKA

Mtafiti huyu anasema utafiti unaonyesha lazima maandalizi yawekwe kwenye makundi ambayo ni kabla ya mashindano, wakati wa mashindano na baada ya mashindano.

Anasema utafiti umebaini Tanzania hakuna utaalam wa kutosha wa kumwaandaa mwanasoka kwa kutofautisha vipindi hivyo tofauti.
Pia anasema umebaini hata programu zilizoandaliwa zikipitiwa wakati mwingine utakuta baada ya kumuimarisha mwanasoka zinaua kiwango chake.

“Tatizo lililopo ni la kiuchumi, wakati mwingine programu ya kumuandaa inakuwepo kuanzia kwenye mazoezi, kula, kupumzika, afya, malazi lakini fedha ya kuitekeleza hakuna,” anasema.

Anasema utafiti umebaini, maandalizi kwa vitendo, yamekuwa ni shida kutokana na vifaa vya kuweza kufanikisha wakati mwingine hakuna.

“Wakati mwingine unakuta wanasoka wapo lakini hawana mpira wala kocha wa kuwafundisha, siku ya mechi wanaingia uwanjani kucheza bila hata kujiandaa kiufundi, kimbinu,”anasema.

Maandalizi ya nadharia anaeleza kuwa sio ya kuridhisha hata kwa timu ya Taifa, wakati mwingine wanapungukiwa na elimu ya nadharia.

Anaeleza kuwa wanapaswa kufundishwa soka darasani kuzijua baadhi ya sheria na kanuni za uchezaji soka na kumjenga kisaikolojia.

“Utafiti umebaini hawapati maandalizi ya kutosha ya kuwawezesha kucheza, lakini pia hawapati vifaa, elimu ya kucheza soka inayohusisha ufundi, mbinu, saikolojia na utimamu wa mwili, malazi mazuri, chakula kizuri cha mlo wa mwanasoka na mapumuziko,”anasema.

Kuhusu tathimini yake ya uendelezaji wanasoka wachanga katika kupandisha kiwango cha soka, mtafiti anasema utafiti umebaini utaratibu uliowekwa na TFF wa kuwatambua kutoka ngazi za chini sio wa kudumu.

“Uliopo ni wa muda, mfano ni `Program Maalum ya Maboresho ya timu ya Taifa’ ambayo haikufanikiwa kwa kiwango kilichotakiwa, kwani wataalamu wa kuwatambua wachezaji wachanga wapo lakini hawajatumiwa ipasavyo,” anafafanua.

Pia utafiti umebaini utambuzi wa wachezaji wachanga unaotumika hauna tija kwa sababu hutoa fursa kwa wachache na hufanyika kipindi cha mashindano na huhusisha baadhi ya maeneo na ukiacha wachezaji wengi wenye vipaji.

Hata waliotambuliwa anasema, kumekuwa hakuna programu maalum ya kuwaendeleza zaidi ya wao kujiendeleza na kujitunza.

“Uendelezaji ili uwe na tija lazima soka liwe ni ajira, mazingira ya kiuchumi yawe mazuri kwa mchezaji, mashindano rasmi yawepo mara kwa mara, kuwepo na vivutio kwao kujikita kwenye soka, wapewe elimu ya kujitambua pamoja na shule za soka,” anasema.

Anaeleza kuwa, programu ya soka ya Real Madrid inayoshirikiani na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), iwe endelevu na isimamiwe vizuri ili itoe matokeo bora na mchango wa shule za msingi na sekondari katika kukuza soka.

“Kucheza soka mashuleni umekuwa kama ni suala la kujifurahisha tofauti na kipindi cha miaka ya 1980 na 1990 kulikuwa na kipindi maalum cha darasani,” anasema.

TATHMINI YA KIWANGO CHA SOKA

Kwa kuangalia viwango vinavyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), utafiti umebaini bado kipo chini na kimekuwa kikishuka ikilinganishwa na walipokuwa miaka ya 1990, 2008 hadi 2012.

“Tumeondoka kwenye nafasi za makumi sasa tupo kwenye nafasi za mamia hii ni hatari kwa maendeleo ya soka itafika kipindi hatutakuwa na uwezo wa kuifunga timu yoyote ya taifa kama hatutaweka na kuutekeleza mkakati madhubuti wa kuinua kiwango chetu cha soka,” anasema.

JE, TFF IPO KATIKA NJIA SAHIHI YA KUKUZA SOKA

Mtafiti huyo anasema usahihi wa TFF kuongoza ni kwa kufuata sheria ya uundwaji wake, kanuni mbalimbali za soka, miongozo mbalimbali ya soka na sera mbalimbali za soka.

“Tukumbuke muundo wa uongozi wa TFF unaanzia ngazi ya rais hadi kwenye klabu za mpira wa miguu vilivyosajiliwa na kutambuliwa na shirikisho hilo,” anasema na kuongeza:

“Kwa hiyo, kwenye ngazi ya juu ya uongozi wa TFF, rais ni lazima atekeleze majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kanuni za soka, kitu ambacho amekuwa anajitahidi kukifanya, tatizo kubwa katika uongozi wa TFF ni uwajibikaji, usimamizi na uwazi,” anabainisha.

Anasema utafiti umebaini uwajibikaji bado uko chini ndio maana TFF mikoa na wilaya zinalegalega kwa sababu hazisimamiwi, hazipati rasilimali za kujitosheleza kujiendesha.

Manumbu anasema bado kwenye sheria na kanuni za soka kunajitokeza migongano na katiba za klabu, wakati mwingine katiba ya klabu ya mpira inaruhusu jambo fulani kufanyika lakini kwenye kanuni za TFF linakatazwa.

Kwa tafsiri nyingine, anasema utafiti umebaini TFF ina wajibu wa kupitia vizuri katiba za klabu ili kuondoa migongano ili iwe rahisi kuongoza.

“Uwazi ni kitu muhimu sana, TFF ina miradi ya ufadhili wa ndani na nje ni vyema izingatie utawala bora iwe wazi kutoa taarifa za mapato na matumizi kwa wadau wake. Lakini kinachoonekana ni kwamba, uwazi katika uongozi huu wa TFF haupo katika kiwango cha kuridhisha.

Kuna msemo kwenye utafiti nimekutana nao unasema TFF inaongozwa kwa fitina, kwamba rais wa TFF ni mtu wa fitina kwa maana anaweka watu wake bila kujali uwezo wa mtu na hapa ndipo tatizo la kushindwa kuwajibika linapojitokeza” anabainisha.

Utafiti umebaini suala la kukuza soka halina ubunifu wa kuanzisha mikakati ya kutambua likuzwe vipi. Bado shirikisho hilo haijapata mwarobaini wa kukuza soka Tanzania hakuna njia sahihi ya kulikuza," anafafanua.
Je, vipi mchango wa Serikali katika kukuza soka? Itaendelea wiki ijayo.