Utaalamu asilia unavyokabili tabianchi

05Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Utaalamu asilia unavyokabili tabianchi

KATIKA vijiji vingi vya Tanzania ukame unatikisa kutokana na jua kali ambalo lingeweza kutumiwa kuzalisha nishati jua, japo teknolojia inakwamisha.

Ukame unawaumiza wanavijiji kwani huongeza uhaba wa maji ambayo licha ya kujaa ardhini ni vigumu kuyachimba kutokana na gharama kubwa na uduni wa teknolojia, unaokolezwa na umaskini.

Hata hivyo, ukame huo ambao ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi unatishia kukausha vyanzo vya maji, kwa baadhi ya jamii za mkoa wa Kilimanjaro hivyo mbinu za asili za kitamaduni zinatumiwa kuidhibiti hali hiyo. Wananchi wanafahamu namna ya kutunza vyanzo hivyo kwa kutumia mbinu za asili na utaalamu wa kijadi.

Zipo mbinu za kiasili au kijadi za kuhifadhi maji na rutuba ya ardhi au hata kuvuta maji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia mapokeo.

Kwenye kanda za milimani, vijiji vingi vina uoto wa kijani unaohifadhi vyanzo vya mito, ardhi oevu, misitu na wananchi wanajitahidi kupanda miti kutunza mazingira pamoja na kuhifadhi maji.

Baadhi ya miti maarufu kutunza na kuvuta maji yaliyo ardhini ni mikuyu, mivumo , mianzi na jamii ya magugu maji yaitwayo ‘majia’ (jina la asili) na masale.

Ziara ya Nipashe katika vijiji vya Chanjale, Ngujini na Vuchama Ndambwe wilayani Mwanga katika mkoa wa Kilimanjaro, ilibainisha kuwa wananchi wengi wanapanda majia, mikuyu na mivumo kutunza vyanzo hivyo.

Mapokeo ya kiasili yanataja kuwa majani ya miti hiyo yanayodondoka au kupukutika hutengeneza mboji inayorutubisha ardhi na kustawisha mazao mengine.Mazao kama migomba, magimbi, mahindi, maharage, iliki na kahawa ni miongoni mwa mimea inayostawi chini ya miti hiyo.

Kwa mfano, nakala za ripoti ya mkutano wa wanakijiji cha Chanjale wa kujadili utunzaji na uhifadhi wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi za mwaka 2014 zinasisitiza matumizi ya miti ya asili. Zinaeleza kuwa mimea hiyo inazalisha mboji na matunda yake ni mbolea bora ikilinganishwa na miti ya kigeni.

Miti kama maparachichi, mafenesi au mapera licha ya kuwa ni mazao ya biashara yanayoleta fedha kwani matunda yake yana soko, yanatajwa kuharibu ardhi kwa kukausha maji ndani ya mwamba ulio karibu. Kadhalika hata majani yake yanayodondoka si rafiki wa mkulima.

Ni makavu, hayazalishi rutuba ya mboji, lakini baya zaidi huzuia uoto mwingine kustawi hasa mazao ya chakula, biashara na nyasi za asili. Mfano halisi ni maparachichi ambayo yanatajwa na wanavijiji kuwa licha ya kuangusha majani mengi ni makavu, hayachanganyikana na ardhi kutengeneza mboji na rutuba.

Kwa kifupi majani haya hayaozi, muda wote ni makavu na hata kama mvua ikinyesha yanachukua muda mrefu kujishindilia ardhini na mara nyingi hayachanganyiki na udongo.

UHIFADHI MAJI ASILIA

Wanavijiji wengi wanaathiriwa na ukame unaokausha maji na kulazimika kuyachota kwenye visima asilia au mitoni. Kisimani hutumia pawa ama vyombo hasa bakuli au vikombe.J

ukumu hili gumu linalowatesa zaidi wanawake ambao hulazimika kuamka usiku wa manane kufuatilia maji hayo. Ndiyo maana wananchi wanatumia mbinu za asilia kulinda maji hayo hasa kuchimba na kukijengea chanzo na kukizungushia ukuta wa masale, majia au mikuyu.Miti hii wataalamu wa asili wa hifadhi ya ardhi wanasema inavuta maji hata kama jua litakuwa kali kupindukia.

Ni kwa mtizamo huu kwamba serikali ichanganye mbinu za asili na elimu ya kijadi ya wananchi na taarifa za kitafiti na teknolojia ya kisasa kuhifadhi maji na kukabiliana na ukame unaotokana na ongezeko la joto duniani. Habari ya kupanda miti au kampeni za panda mti kata mti ziangalie pia uelewa wa kiasili walio nao Watanzania wa vijijini kwani kuna hazina kubwa ya ufahamu iliyo ndani ya utamaduni wa kila kabila. PICHA IN DA FOLDA ‘T’ MITI