Wakazi wa kijiji cha Miima waliaanza kutekeleza azma ya kutumbua majipu mapema mwaka jana, baada ya kubaini uongozi wa Mwenyekiti wa kijiji hicho kuwa sehemu ya wahalifu wa mazao ya misitu na matumizi mabaya ya madaraka.
Kijiji hicho kinamiliki msitu wa hifadhi wenye hekta 2,662 ambao mapato yatokanayo na mavuno ya mazao yake, yanategemewa kuboresha huduma za kijamii na kuleta maendeleo kijijini hapo.
KUTUMBULIWA
Desemba 18, mwaka jana wanakijiji hao walifanya mkutano wa dharura na kumtimua mwenyekiti Thomas Michael na wajumbe wa serikali ya kijiji hicho.
Miongoni mwa sababu ya kufikia hatua hiyo ni kushindwa kuusimamia na kuulinda msitu wa kijiji hicho pia kushirikiana na wahalifu kuvuna mazao ya msitu huo kiholela.
Kabla ya kuchukuliwa hatua hiyo wakisimamiwa na viongozi wa ngazi ya kata, dosari kadhaa za uongozi wa kijiji hicho zilibainika, ikiwa ni pamoja na kutoitisha mkutano wa wananachi kuzungumzia udhibiti wa uhalifu kwenye msitu wa Miima.
“Taarifa zilitolewa kuhusu uharibifu wa misitu ulioshuhudiwa na wananchi lakini, uongozi wa kijiji haukujali ulipotakiwa kuitisha mkutano ili kujadili hali hiyo, hawakufanya hivyo,” anasema Said Kihanga, mkazi wa kijiji hicho.
Ingawa hakuna kiongozi ama mjumbe wa serikali ya kijiji wa uongozi ulioondoshwa madarakani aliyepatikana kuzungumzia tuhuma hizo, ilibainika kuwa kama ilivyokuwa kwa wajumbe wa kamati ya maliasili, viongozi wa kijiji walikiri kuwapo kwa upungufu mengi ndani ya uongozi wao.
Wanakijiji walimuamini na kumteua aliyewahi kushika wadhifa huo kwa awamu mbili, Omar Katende, kuwa Kaimu Mwenyekiti wa kijiji.
Kihanga anasema baada ya mabadiliko hayo, uongozi uliongia madarakani ukabaini udhaifu zaidi na hujuma zilizochochewa na uongozi uliotumbuliwa.
KASHFA
Kiongozi wa Mtandao wa Tunza Misitu Asilia, Said Mwambe, anataja baadhi ya tuhuma kuwa ni pamoja na mbao 900 zilizochanwa kwa ajili ya ujenzi wa maabara, 120 kati ya hizo zikatumiwa huku 680 zikidaiwa kuungua hadi kuteketea kwa moto.
Viongozi wapya kwa kushirikiana na wanakijiji walichunguza na kubaini kuwa mbao hizo hazikuungua, bali zilihujumiwa na kukisababishia kijiji hicho hasara.
Pia ulibaini kuwapo mfanyabiashara aliyekuwa na leseni ya kuvuna mbao eneo la wazi, akazuiliwa lakini baada ya wiki mbili alirejea kuendelea kuvuna.
Alifanya kazi ndani ya msitu huo kwa wiki nzima pasipo ufuatiliaji na kamati ya maliasili ilipokwenda kukagua ilikuta ana mbao 840 badala ya 700 alizoruhusiwa kupasua.
Kwa mujibu wa vyanzo tofauti vya habari kijijini hapo, mbao zilizozidi zilichukuliwa na uongozi mpya wa serikali ya kijiji hicho huku mfanyabiashara huyu (jina halikujulikana) akisalia na mbao 700.
Mwanakijiji Mohamed Bakari, anasema usimamizi wa misitu ulipewa kipaumbele kijijini hapo lakini uongozi ulioondolewa madarakani uliuhujumu.
Wakati masuala hayo yakijitokeza, wakazi tofauti wa kijiji hicho wanaelezea kuhusu kushamiri kwa uvunaji miti wa kutumia msumeno wa moto, hali iliyochangia uhabiribu wa msitu huo.
NJIA MBADALA
Uendelezaji bora wa msitu utafanikiwa ikiwa wadau walio katika mnyororo wa usimamizi watashiriki ipasavyo.
Miongoni mwa wadau wa misitu wilayani Lindi Vijijini ni Issa Abadan, ambaye ni mfanyabiashara anasema, miongoni mwa changamoto zinazo wakabili katika biashara ya mazao ya misitu ni wingi wa kodi wanazotozwa na mamlaka tofauti.
Anatoa mfano kuwa analipa Sh 387,000 za leseni ya kufanya biashara kwa mwaka, Mamlaka ya Mapato (TRA) inamtoza Sh 125,000 wakati leseni ya halmashauri ya wilaya inamgharimu Sh 50,000.
Katende, Kaimu Mwenyekiti wa kijiji cha Miima, anasema wahalifu wanapokamatwa na wajumbe wa kamati ya masiasili, wanafikishwa kwa uongozi wa kijiji kwa ajili ya kuadhibiwa.
Athuman Hamisi, Kaimu Afisa Mtendaji wa Miima anasema baada ya kamati ya maliasili kuondolewa madarakani, walitakiwa kufuatilia fedha zilizopaswa kulipwa na wafanyabiashara wa mazao ya misitu wanaodaiwa lakini uongozi uliokuwapo ukashindwa kuzifuatilia.
Hata hivyo, kwa kipindi cha karibu mwezi mmoja na nusu, serikali mpya ya kijiji hicho ilifanikiwa kukusanya Shilingi milioni 1.5 kutokana na tozo za msitu na ushurutofauti.
Hamis anasema wakati kijiji hicho kikisubiri mamlaka za wilaya kusimamia uchaguzi rasmi wa viongozi wao, wamebainisha vipaumbele vyao kuwa ni ukarabati wa barabara inayoingia kijijini humo, ofisi ya kijiji, visima vya maji salama na ghala la kuhifadhia chakula.
Jamii Miima inazidi kupata mwamko na manufaa ya kuhifadhi misitu ya vijiji, hivyo kuwalazimu kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha rasilimali hiyo inakuwa endelevu kwa kizazi cha sasa na kinachokuja.










