kama nchi hiyo itabadili katiba yake kumuwezesha kiongozi huyo abakie madarakani kwa maisha yake yote.
Museveni (71), ambaye aliingia madarakani mwaka 1986 na akiwa amejifafanua kwa mataifa ya Magharibi kama mpiganaji dhidi ya Waislamu wenye itikadi kali kwenye eneo hilo, anazuiwa kugombea kwenye uchaguzi ujao mwaka 2021 kwa sababu atakuwa ameshazidi ukomo wa umri unaoruhusiwa kikatiba wa miaka 75 kwa wagombea wa nafasi ya urais.
Lakini mahasimu wake, wataalamu na wapiga kura walisema walikuwa wanategemea Museveni kuondoa ukomo huo wa umri kufuatia uchaguzi wa Februari 18 ambao ulimshuhudia kiongozi huyo akipata ushindi wa asilimia 60 ya kura zilizopigwa.
Tayari upinzani unapinga matokeo hayo, ukisema yalichakachuliwa, lakini mamlaka nchini humo zinayakana madai hayo.
Wakosoaji wa Museveni wanasema anafuata njia inayotumiwa sana na viongozi wa Kiafrika wanaojaribu kubakia madarakani kwa maisha yao yote, wakipuuza miito ya Marekani na mataifa mengine ya Magharibi kwa marais wa nchi za Kiafrika ya kuwataka kuendana na ukomo wa kikatiba wa muda wa kuwa madarakani na kuachia ngazi.
"Wengi kati ya hawa (viongozi) wana hofu moja kubwa sana ya kuachia madaraka, na ambayo haiwezekani kuielezea," alisema Nicholas Sengoba, mwandishi wa makala wa gazeti la Daily Monitor la Uganda.
Kwenye mahojiano yaliyorushwa kwenye televisheni wiki chache nyuma, Museveni alionekana kufungua mlango wa uwezekano huo wa kutokuwepo kwa ukomo wa umri kwa wagombea.
"Hatuamini kwenye masuala ya ukomo," Museveni alilieleza Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
"Kama hamutaki wawepo maisha yao yote, mnawaondoa kwa kura."
Museveni, ambaye aliongoza vita vya msituni kwenye miaka ya mwanzoni ya 1980 ambavyo vilimuingiza madarakani, amekuwa akimwagiwa sifa kwa kuleta amani na ukuaji uchumi nchini Uganda, taifa lililo njiani kuwa mzalishaji wa mafuta lakini hata hivyo likiwa bado linaathiriwa na miundombinu duni.
Wakosoaji wanamlaumu kwa kutoshughulikia kwake kikamilifu kupunguza kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira na kupambana na rushwa, pamoja na kukwamisha maendeleo ya Uganda kwa kuwa na mtazamo wa uongozi wa kutoka juu kwenda chini. Katika hilo, wananyooshea kidole tabia ya Museveni ya kupenda kutumia neno la "mafuta yangu".
Kiongozi wa upinzani, Kizza Besigye, ambaye alipata asilimia 35 ya kura zilizopigwa na alimshutumu Museveni kwa uchakachuaji kwenye uchaguzi huo, alilieleza shirika la habari la Uingereza la Reuters kwamba alikuwa akitegemea rais huyo kujaribu kubaki madarakani.
"Iwe anabadili katiba au sivyo, dikteta ni kitu kisichokaribishwa kwenye nchi yetu," Besigye alisema. "Kampeni hiyo ya kupinga ... haitaachwa hadi pale dikteta huyo atakapoondoka madarakani."
KUWAKILISHA UTULIVU
Kwenye mitaa ya Kampala, wapiga kura walisema watashtushwa sana kama Museveni ataachia ngazi, iwe ni kwa kumtaja mrithi wake au kutangaza mwenyewe kustaafu kwake.Zaidi ya robo tatu ya raia wa Uganda wana umri wa chini ya miaka 30 na hawajawahi kumfahamu rais mwingine kwenye nchi hiyo.
Hata hivyo, kwenye taifa ambalo bado linagubikwa na miongo kadhaa ya vurugu chini ya viongozi kama Idi Amin, ambaye aliongoza dola la kikatili la polisi kwenye miaka ya 1970 ambalo liliua au kutesa watu wanaokadiriwa kufikia 300,000, Museveni bado anawakilisha utulivu kwa walio wengi.
"Uganda inahitaji kiongozi mtulivu," alisema Benjamin Kashilling, 29, meneja wa mgahawa mmoja mjini Kampala.
Wengine walisema sasa ulikuwa ni wakati wa kuachana na kile wanachokiita kujifanya kupiga kura.
"Wanapaswa kuacha kutusumbua kabisa na kutangaza kwamba yeye ana urais wa maisha," alisema Sara, 52, ambaye alitaja jina lake la kwanza tu na kusema uchaguzi uliopita ulichakachuliwa. "Acheni kutupotezea muda wetu kwa hizi chaguzi."
Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, aliwahi kummwagia sifa Museveni akimuelezea kama sehemu ya "kizazi kipya" cha viongozi wa Afrika wanaokumbatia demokrasia.
Hivi sasa, Waganda wengi wanamlinganisha na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, ambaye hivi karibuni alitimiza miaka 92 na hajaonyesha nia ya kuachia ngazi.
Mwaka jana, Rwanda na Jamhuri ya Congo zote mbili zilibadili katiba zao kuwawezesha viongozi wao kugombea awamu za tatu badala ya mbili zilizokuwepo.
Uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi wa kubakia madarakani baada ya kumaliza awamu mbili ulichochea sekeseke ambalo waangalizi wa kimataifa wanahofia linaweza kuirudisha nchi hiyo kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.
"Tumesema kwamba kutakuwepo na upitiwaji wa katiba. Maeneo mengi (kwenye katiba) yanahitajika kuangaliwa," Waziri Mkuu wa Uganda, Ruhakana Rugunda, aliieleza Reuters hivi karibuni. "Kuhusu ni nini kitatokea miaka mitano kuanzia sasa, hilo ni chaguo la watu wa Uganda."
Kwa sasa, Uganda ina ukomo wa umri wa wagombea lakini haina ukomo wa awamu za urais. Wapinzani wanasema Museveni ana uwezekano mkubwa wa kuondoa ukomo huo wa umri, kama alivyoondoa ukomo wa awamu za uongozi muongo mmoja uliopita.
Baada ya uchaguzi wa hivi karibuni, chama cha National Resistance Movement (NRM) cha Meseveni kinadhibiti viti takriban 275 kati ya 381 kwenye bunge la nchi hiyo na hivyo kuwa na sauti kubwa kama ikibidi ya kubadili katiba.










