Fursa hizo zikitumika ipasavyo na wakati huo huo serikali ikatekeleza kwa dhati ukomeshwaji wa kero za rushwa, upendeleo (udugunaizesheni), katika utoaji wa ajira na fursa za biashara, basi kwa uhakika wajasiriamali wengi hapa nchini watapiga hatua kubwa na hali za wengi kimaisha zitabadilika.
Iwapo kero zinazotajwa hapo juu zinaondoshwa na wakati huo huo, wananchi kuwezeshwa kupata mikopo nafuu na elimu ya kibiahara, basi hakuna sababu kwa nini pato la raia hawa lisiongezeke, biashara kushamiri na pato la nchi kuongezeka kiuchumi.
Nasema hivi kwa sababu Tanzania imejaliwa rasilimali nyingi za asili kama ardhi, bahari, maziwa, madini, gesi na fursa katika utalii. Zaidi hali ya amani na utulivu pamoja na bidii na ubunifu walio nao raia wa Tanzania, ni fursa ambazo si kila nchi hapa duniani inavyo kwa sasa.
Niseme kwamba haya ni mambo yanayojulikana na kila mmoja wetu, lakini safu hii leo tutauibua mtaji mwingine ambao Tanzania inao, lakini haujulikani sana ama haujatumika ipasavyo na wajasiriamali wengi katika kubaini fursa lukuki za kibiashara tunazoendelea kuzilalia.
Bila kupoteza muda, nizungumzie fursa isiyojulikana na wengi, lakini ambayo nataka uitambue pale uhitimishapo kuisoma makala hii. Fursa hii si nyingine bali ni kuwapo kwa sheria mbalimbali ambazo zipo mahsusi kwa ajili ya sekta na makundi muhimu ya kijamii.
Kabla ya kuzitaja sheria hizi nitoe angalizo dogo kwamba baadhi ya sheria hizi zina mapungufu, lakini hili pia lisikuzuie wewe mjasiriamali kutumia sheria hizi hizi kwa sababu ndizo zinazotumika na pia zimetumika kuwatajirisha wale ambao wameiona mianya iliyomo ndani yake wakati zikiendelea kuwapo. Sheria zinazotoa fursa za kibiashara ziko za aina mbili.
Mosi, zile za jumla ambazo zinatumika na mtu ama kundi lolote la watu. Mfano katika kundi hili ni pamoja na Sheria ya Mikataba, Sheria ya Kampuni, Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Sheria za Ardhi (4 na 5 za mwaka 1999), Sheria za Kodi, Sheria za Benki, na kadhalika.
Sheria zinazolenga sekta au kundi fulani la kijamii ziko lukuki na tukiziorodhesha hapa tungeweza kujaza gazeti lote; kwa hiyo nizitaje tu zile ambazo zinahusika na sekta ama makundi yenye kuhusisha watu wengi ama kuchangia kiasi kikubwa katika pato la taifa letu.
Sheria ya Madini ya mwaka 2010, inahusika zaidi katika sekta hii na kila anayetafuta maisha kupitia sekta hii anapaswa aifahamu. Sambamba na sheria hii, ipo pia sheria inayodhibiti biashara ya vito nchini. Sekta ya mifugo inazo sheria zake pia, zikiwamo Sheria yenyewe ya Uvuvi na pia sheria tofauti inayohusika na biashara ya mazao ya ngozi za mifugo.
Zaidi kuna sheria inayojitegemea ya sekta ya maziwa na vitu vitokanavyo mathalani jibini na siagi.
Sheria ya utalii inaongozwa na sheria katika jambo hili iliyotungwa na Bunge mwaka 2008 (Sheria namba 3 ya mwaka 2008). Wavuvi wanapaswa waifahamu sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003, pamoja na kanuni zake, ili kutambua haki, wajibu na fursa zilizomo humo. Wale wanaohusika na uzalishaji wa misitu wanapaswa kuwa karibu na Sheria ya Misitu ya 2002.
Kutokana na kilimo kuwa uti wa mgongo wa nchi hii, Bunge lilitunga sheria mbalimbali kukidhi matakwa tofauti kwa makundi ya wakulima na mazao yanayolimwa hapa nchini, basi iwapo wewe ni mkulima ama mfanyabiashara unayetaka kujua masharti na fursa zilizomo katika sheria hizi utapaswa kuzisoma ama kutafuta mwanasheria akuelimishe.
Miongoni mwa sheria zinazohusika na fursa katika kilimo na mazao yake ni pamona na Sheria ya sekta ndogo ya kilimo cha miwa na mazao ya sukari, sheria ya sekta ndogo ya kilimo cha pamba ya mwaka 2001, sheria ya sekta ndogo ya kilimo cha kahawa ya mwaka 2001, sheria ya sekta ndogo ya chai ya mwaka 1997, Sheria ya sekta ndogo ya tumbaku ya mwaka 2001, na pia sheria ya mkonge na mazao yake ya mwaka 1997.
Biashara ya vinywaji vya pombe na pombe kali (vileo), pia inazo sheria zake kama zilivyo biashara za mabaa, kumbi za muziki, michezo ya kubahatisha, kumbi za sinema na uonyeshaji filamu na kadhalika.
Biashara ya usafirishaji barabarani, baharini na pia kwa njia ya reli ina sheria yake inayosimamiwa na Sumatra ambayo ni Mamlaka iliyopewa jukumu la kuisimamia.
Mafuta ya petroli, dizeli, mafuta ya taa na nishati kama hizo ina sheria yake ambayo ni Sheria ya Petroli ya Mwaka 1988. Sheria hii inayohusika pia na uingizwaji nchini mafuta ghafi na pia biashara za vituo vya petroli na gesi ya mitungi, inadhibitiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), ambayo ndiyo iliyopewa jukumu hilo kisheria.
Mathalani, kama unataka kuanzisha kituo cha mafuta basi sheria hii inakuhusu na ni lazima upitie katika mamlaka hii husika ili kuidhinishwa.
Wapo waliojaliwa uwezo au mitaji mikubwa wanayoweza kutumia kuanzishia Benki au angalau duka la kubadilishia fedha (Bureau de Change). Msimamizi mkuu wa sekta hii ni Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na ndiyo inayotunga kanuni na kuhusika na utoaji wa leseni za biashara katika sekta hii.
Hapa basi unapaswa kuifahamu sheria inayounda BoT ya mwaka 2005 na pia Sheria ya mabenki na taasisi za kifedha. Chini ya Sheria ya Benki Kuu zipo kanuni mbalimbali, mathalani zile zinazohusika na biashara ya maduka ya ubadilishwaji fedha. Hivyo, hapo ni mahali kwa kuanzia kama unataka kupata mwanga zaidi na ufanye maamuzi ya hekima.
Makundi ya kitaalamu nayo yanazo sheria zake ambazo zinadhibiti taaluma husika ili kulinda hadhi za makundi hayo na wananchi pia.
Hivyo basi, walimu, wahasibu, mawakili, madaktari, wafamasia, wauguzi, wahandisi, waandishi wa habari, wacheza filamu, watangazaji, madereva, marubani na wote wanaongozwa na sheria zilizopo hapa nchini na ni vema sana kila mmoja ajue sheria husika ili afanye kazi yake kwa kujiamini zaidi, kutovunja sheria, lakini pia kuzitambua fursa zilizomo ndani yake.
Changamoto yangu kwako leo ni moja tu; itafute sheria inayohusu kazi au matarajio yako, jaribu kuipitia, pata maoni ya walio na uzoefu katika kazi inayohusika na sheria hiyo ama mawakili na utashangaa yale utakayoyatambua na hukuwa unayajua jana yake.
Lakini pia, zaidi ya hapo, uelewa wa sheria unakusaidia kuishi kwa amani kwa sababu pengine umekuwa ukifanya jambo ama biashara ambayo hujui kama sheria inaruhusu ama kukataza, mathalani kucheza kamari ama biashara ya ngono. Ukijua iwapo mambo haya yanakubalika ama la, itakusaidia sana kwa sababu kwa kawaida pale mkono wa dola ukikufikia na ukajikuta uko mahakamani, siku zote inafahamika kwamba ujinga wa kutojua sheria kwa kawaida si utetezi unaokubalika mahakamani.
Tuhitimishie hapa kwa kukuasa uzitafute sheria husika. Kazihakiki zaidi ili kupata marekebisho yaliyofanywa katika sheria tajwa kwa sababu sheria zinabadilika kila leo, zikiwamo hizi nilizozitaja hapo juu.
Ijumaa ijayo tutaizungumzia moja ya mada muhimu kuhusiana na sheria za mikataba.
*Denis Maringo ni Mwanasheria/Wakili aliyeko Dar es Salaam. Mawasiliano ni: 0719270067. Barua-pepe: dnmaringo@gmail.com










