Dudubaya: Shetta ajiite Kenge

01Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Dudubaya: Shetta ajiite Kenge

MSANII mkongwe wa muziki wa kizazi kipya, Dudubaya, amemtangazia vita msanii mwenzake Shetta, akimtuhumu kutumia jina la kisanii la 'Mamba'.

MSANII mkongwe wa muziki wa kizazi kipya, Dudubaya

Dudubaya anadai yeye ndiye 'Mamba' na amekuwa akilitumia jina hilo tangu mwaka 2007 na sasa analitumia pia katika biashara zake mbalimbali anazofanya.

"Imeniudhi sana Shetta kutumia jina langu la 'Mamba', hawezi kujiita Mamba wakati ni jina langu toka 2007, hawa watoto 'sometimes' (wakati mwingine) wanakosa adabu, sitaki atumie jina langu na akiendelea kutumia, asinirudishe kwenye enzi za Mr. Nice, nitamfanya zaidi ya Mr. Nice", alitamba Dudubaya.

Msanii huyo aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Planet Bongo cha East Africa Radio na kufafanua kuwa ameshampigia simu Shetta na kumtaka ajiite Kenge.

"Mamba ni jina langu, na ndiyo maana biashara zangu hata nikifungua 'Pub', itaitwa Mambaz, nikifungua chochote kitaitwa Mamba, hivyo hawezi yeye (Shetta) kujiita Mamba, kwanza umbo lake lenyewe siyo Mamba," alisema.

Alipotafutwa na Nipashe kuzungumzia suala hilo, Shetta alisema ameshangaa kumsikia msanii mkongwe huyo akiendelea na tabia yake ya zamani ya kutaka mambo ya ugomvi ambayo hayana faida yoyote kwa sasa.

"Ilichukua muda kidogo kuamini kwamba ni Dudubaya ndiye alikuwa akisema hayo, nilidhani baada ya kimya cha muda mrefu katika muziki, atakuwa amebadilika na kuwa mtu mwema, kumbe mambo ni yaleyale," alisema.

Shetta alisema amekuwa akitumia jina hilo kwa vile ni jambo la kawaida katika sanaa, lakini anashangaa kuona Dudubaya akiibuka na kutoa vitisho huku akijua kuwa hiyo ni sanaa tu.