Cheka anavyopania kuwatengeneza ‘Cheka wengine’

22Feb 2016
Dar
Nipashe
Cheka anavyopania kuwatengeneza ‘Cheka wengine’

WAKATI akijiandaa kumvaa bondia wa kimataifa kutoka Uingereza, Jeard Ajetovic katika pambano lililopangwa kufanyika Februari 27, kwenye viwanja vya Leaders,....

Bondia Kalama Nyilawila (kushoto) akionyeshana umwamba na Francis Cheka.

Bondia Francis Cheka amepania kufundisha mabondia chipukizi, ambao anamini watakuja kuziba pengo lake pale atakapoamua kustaafu kucheza mchezo wa ngumi za kulipwa.

Cheka anasema amepania kufundisha chipukizi katika mchezo huo, kwa lengo la kutaka kuwaacha kina Cheka wengine mara umri wa kustaafu kucheza mchezo huo utakapofikia, ili Tanzania iendelee kung'ara katika mchezo wa ngumni za kulipwa.

Anasema ameamua kufanya hivyo baada ya kuona thamani ya mchezo huo pamoja na mashabiki wanavyomthamini kutokana na kila bondia kutaka kucheza naye.

Cheka anasema tayari ameanza kuwafundisha vijana mchezo huo na anaamini baada ya miwili ijayo watapatikana mabondia wazuri zaidi yake. Akizungumzia maandalizi ya pambano lake dhidi ya Ajetovic, amesema yako vizuri na kamwe hatawaangusha wapenzi wa ndondi nchini.

Cheka amesema pambano hilo linalotambuliwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Duniani (WBF), litakuwa na raundi 12 katika uzito wa kati, amepania kumtoa kwa KO mpinzani wake. Cheka amesema anaamini bondia huyo ni mzuri, lakini hamuofii hata kidogo kutokana na kuwa amejiandaa vya kutosha kuhakikisha anaipeperusha vema bendera ya nchi katika pambano hilo la uzito wa kati, ambalo mgeni rasmi anatarajia kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni wasanii na Michezo, Nape Nnauye.

Amesema pambano hilo litatoa hamasa kubwa kwa wapenzi wa mchezo huo kutokana na kuwa yeye kama bondia, amejipanga kuufanya mchezo huo ukubalike na wadhamini. "Nawaomba mabondia wenzangu kuanzisha mashindano kwa ajili ya kutafuta mabondia chipukizi," alisema Cheka.

Amesema kuna mabondia wengi wenye uwezo wanaohitajika kujitolea kuwaandaa wengine ili wao wanapoachia ngazi kusiwepo na pengo.

Changamoto:

Anasema moja ya changamoto zinazowakabili mabondia wengi ni pamoja ni ufinyu wa malipo kutoka kwa mapromota na waandaaji wa mapambano mbalimbali.

Mapendekezo:

Kutokana na hilo, anawaomba waandaaji wa mapambano ya ngumi za kulipwa, ikiwemo mashirikisho yanayosimamia mchezo huo na mapromota kuongeze dau kwa mabondia.
Mbali na hilo, anaiomba Serikali kuuangalia mchezo huo kwa karibu zaidi kwa sababu ni moja ya kati ya inayoweza kuiletea sifa Tanzania.