Wadau mbalimbali nchini wakizungumzia hali ya matokeo matokeo ya kidato cha nne mwaka 2015 yaliyotangazwa hivi karibuni, wameitaka serikali kuchukua hatua za makusudi ili kuhakikisha kuwa mazingira ya kujifunzia na kufunzia yanaboreshwa badala ya kuendelea kubadili mfumo wa upangaji matokeo bila ya kutatua matatizo ya msingi yaliyopo.
Meneja Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa shirika lisilo la kiserikali la HakiElimu, Godfrey Bonivetura, anasema kwa hesabu ya haraka matokeo ya mwaka huu siyo mazuri kutokana na ukweli kuwa waliofeli ni wengi zaidi na shule za umma ambazo ni kimbilio la wengi zimeendelea kufanya vibaya mwaka hadi mwaka.
Tafsiri ya matokeo ya mwaka huu ni kwamba katika kila wanafunzi 100 kati yao 32 wamefeli. Na kila wanafunzi 100 kati yake 25 ndiyo wamepata daraja la kwanza, jambo ambalo linaonyesha kuwa safari bado ni ndefu ili kufikia viwango vizuri vya elimu.
“Ili mwanafunzi afaulu ni lazima kuwa na maandalizi mazuri kwa maana ya vifaa vya kujifunzia kivitendo, madarasa na walimu wenye motisha wa kufanya kazi. Kwa shule za umma hayo hayapo,” alisema.
Meneja huyo anabainisha kuwa ni muhimu changamoto kuu, zinazozikabili shule hizo ni lazima serikali ichukue hatua za haraka kuzikabili ili kuiokoa sekta ya elimu nchini.
Miongoni mwa changamoto hizo ni kwanza, walimu wamekata tamaa. Boniventura anasema walimu wengi katika shule za serikali wanalazimika kufanya shughuli zao binafsi kwa sababu ya kukosa motisha katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku tofauti na wanaofundisha kwenye shule binafsi.
“Mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika shule za umma ni magumu. Walimu hawana mtu anayewajali kwa karibu kama ilivyo shule binafsi. Hakuna maabara na zilizopo zimekamilika majengo lakini hakuna vifaa vya kuhakikisha kuwa wanafunzi wanajifunza kwa vitendo,” alisema na kuongeza:
“Nilitembelea shule tano za sekondari katika mkoa wa Serengeti ambazo ni Nkoma, Kambarage, Machocho, Kitumburuma hazina vifaa na wanafunzi wanaendelea kusoma masomo kama ya Kemia, Fizikia na Jiografia kinadharia zaidi kuliko vitendo.”
Pili ni usimamizi wa walimu ili wamalize mada. Anasema asilimia kubwa ya shule za umma walimu hawamalizi kufundisha mada zinazotakiwa hivyo wanafunzi wanakwenda kufanya mtihani wa taifa wakiwa na nusu ya mada walizopaswa kuzisoma.
Aidha, alisema HakiElimu inatarajia kufanya utafiti wa nini kilichosababisha wanafunzi wengi kuendelea kuboronga hasa katika shule za serikali ili kupata hali halisi katika shule hizo.
“Kila siku tunabadili madaraja ambayo ni mambo ya kisiasa zaidi. Shule nyingi zimechakaa sana hazifai, kadri muda unavyokwenda zinazidi kuchakaa na watoto wataendelea kufeli kama zitaachwa hivyo,” alibainisha.
Alisema katika shule binafsi 100 zote zina mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia, na hakuna changamoto ya ukosefu wa walimu. Mara nyingi utakuta zinashindana kufundisha ili wanafunzi wafanye vizuri na kuvutia wanafunzi wengi zaidi.
“Ukitembelea shule binafsi unaona iko vizuri. Kuna usimamizi mzuri sana. Niliwahi kwenda kufanya utafiti katika shule mojawapo binafsi sikuwa na ratiba nao, lakini sikupata ushirikiano. Kila mwalimu alikuwa kwenye ratiba na wanafunzi pia, niliambiwa nipange ratiba baada ya wiki mbili, inaonyesha kiasi gani wamejipanga tofauti na shule za umma ambazo kwa kiasi kikubwa hakuna uwajibikaji,” alisema.
Katika shule hizo, kila mwalimu akianza kazi anaelezwa kuwa anapimwa kwa jinsi atakavyofaulisha wanafunzi wake na kuna zawadi mbalimbali ikiwamo kuwapa fedha, mambo ambayo serikalini hayapo na yanaongeza motisha wa kufanyakazi.
“Walimu wa shule binafsi wanapewa mahitaji muhimu kama mikopo ya viwanja, magari na zawadi mbalimbali hivyo ni rahisi kwa mwalimu kuongeza bidii ya kufundisha na kuipenda kazi yake, kwa kuwa anajua kuna motisha na kutambulika kwa kile anachokifanya,” anasema.
“Leo ukienda kwenye maabara ya jiografia ya shule binafsi utaona wanafunzi wanavyosoma kwa vitendo na wanajua kile wanachosoma. Lakini kwa shule za umma wanasoma kwa nadharia na mwisho wanakutana kwenye mtihani wa taifa lazima shule binafsi ziendelee kufanya vizuri,” alisema.
Tatu, ukaguzi katika shule binafsi unafanyika mara kwa mara lakini katika shule za serikali haufanyiki na kwa mwaka jana asilimia 25 pekee ya shule zake ndizo zilikaguliwa.
Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo visivyo vya kiserikali Tanzania (Tamongsco), Benjamin Nkonya, anasema shule za serikali wakaguzi wanaogopa kuzikagua na kutoa mapendekezo yao kwa kuwa watafukuzwa kazi na imeshajitokeza mara kadhaa.
“Wakaguzi wakienda kwenye shule binafsi wanazikagua na kutoa mapendekezo yanayofanyiwa kazi. Lakini kwa shule binafsi wanawaogopa waajiri wao, hasa kwa shule zenye majina ya viongozi wa kitaifa, kuzitangaza kuwa zimefanya vibaya au zinatakiwa kufungiwa. Hili linaziua shule hizi na ni lazima serikali ijichunguze,” anasema.
Nne, anasema nidhamu na ukaguzi wa kweli, ndiyo unasaidia shule kuwa katika ubora muda wote, vifaa na mahitaji yote yanapatikana tofauti na serikali.
Aidha, anampongeza Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, kwa kufuta mfumo wa GPA ambao ulidanganya kwa kuongeza idadi ya waliofaulu na kurejesha mfumo wa madaraja ambao ndiyo suluhisho la tatizo.
“Tatizo lilikuwapo lakini wanafunzi wanaonekana wanafanya vizuri kumbe wanafanya vibaya. Limetumbuliwa jipu la GPA kwani wengi walielezwa wana mafua kumbe wanasaratani, Prof. Ndalichako kaeleza ukweli kuwa, hiyo ni saratani na sasa tiba itapatikana,” alibainisha.
Anasema kuwa, hali iliyokuwapo ni kwamba wanafunzi walikuwa hawasomi kwa kuwa wanajua kufaulu kumerahisishwa. Na wengi walikuwa wakimaliza chuo kikuu hawaajiriwi kwa kuwa hawana uelewa wa mambo na walifaulu kwa ujanja, lakini kwa sasa inawalazimu wanafunzi kusoma kwa bidii kwa kuwa wanajua kuna kufeli.
Nkonya anasema, hali ilivyokuwa inaendelea ingefikia mahali nchi ingeendeshwa na wageni, ambao wangeajiriwa katika nafasi mbalimbali, lakini kwa mabadiliko ya sasa yanapaswa kuhakikisha kuwa heshima ya elimu nchini inarejea.
“Tangu matokeo yatoke hata bili za umeme zimeongezeka na wanaheshimu walimu wao, amefanya jambo la kuokoa nchi, hatua siyo kutamka iangalie namna gani itaboresha elimu yake,” anasema.
Aidha, anamuomba Prof. Ndalichako kukutana na walimu na kuzungumza nao kwa kina, kwa kuwa ndiyo wana majibu ya tatizo lililopo katika sekta ya elimu nchini.
Awali alisema kinachotakiwa kufanyika ni wazazi kuruhusiwa kuchagua shule za kuwapeleka watoto wao na kuwa vocha anayopewa mzazi ikiwa na ada ambayo serikali italipa jambo ambalo litaongeza ushindani.
“Ikiwa kutakuwa na ushindani baina ya shule na walimu wataongeza bidii na wale shule zao zitakazoendelea kuboronga wachukuliwe hatua na bodi za shule,” anasema.
Katibu huyo anasema, utafiti wa Benki ya Dunia (WB) mwaka 2008/2011 ambao alishiriki, ulifanyika kwenye nchi za Afrika Tanzania ikiwamo na kubaini mfumo wa vocha kuwa utapandisha ubora wa elimu huku gharama katika shule binafsi ukishuka.
Anatolea mfano wa nchi ya Uholanzi ambayo asilimia 87 ya shule za sekondari zinamilikiwa na watu binafsi, lakini serikali inatoa mchango wake kwa mfumo wa vocha na kwa shule za msingi pia umeleta mafanikio makubwa.
Sababu nyingine kwa mujibu wa Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (UDSM), Prof. Kitila Mkumbo, inayochochangia kushuka kwa ufaulu nchini ni matokeo ya kutowekeza katika elimu, kwa maana ya kuwa na walimu wa kutosha, wenye motisha na vifaa vya kujifunzia na kufundishia.
Anasema ni lazima serikali ijipange vizuri kwa kuwa mkazo umekuwa kwenye kuongeza idadi ya wanafunzi kuliko kuboresha shule na maslahi ya walimu kwa ujumla, hivyo safari ni ndefu ya kuanzia miaka 10 hadi 15 kufikia viwango vizuri katika sekta hiyo.
Prof. Mkumbo anasisitiza kuwa, lazima serikali ya awamu ya tano kulichukua suala hilo kama moja ya changamoto kubwa zilizopo na kuweka mipango endelevu ya kutatua ili kuondoa aibu iliyopo katika sekta ya elimu nchini.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) hivi karibuni, takriban asilimia 75 ya watahiniwa wamefanya vibaya. Wanafunzi waliopata daraja la kwanza ni asilimia 25 na asilimia 74.66 wamepata daraja la nne na sifuri.










