Mgosi: Mzee wa bao la video Simba vs Yanga

22Feb 2016
Adam Fungamwango
Dar
Nipashe
Mgosi: Mzee wa bao la video Simba vs Yanga

MECHI ya watani wa jadi imechezwa jana ikishuhudia Simba ikichapwa mabao 2-0 na Yanga.

Mgosi.

Yalikuwa magoli ya Donald Ngoma na Amissi Tambwe Simba yalioiweka Yanga kileleni
Mshambuliaji Mussa Hassan Mgosi hakucheza mechi hiyo, lakini ndiye mchezaji pekee kwenye historia ya watani hao kuweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyefunga magoli mengi kwenye mechi za watani za Ligi Kuu tangu kuingia karne ya 21 kuendelea kuwepo kwenye moja ya vikosi hivyo.

Lakini anaweka rekodi nyingine ya kuwa mchezaji pekee kwenye historia ya timu hizo kufunga goli lililokubaliwa kutokana na teknolojia ya televisheni uwanjani.

Mgosin alirudishwa tena kwenye kikosi cha Simba msimu huu, ingawa kwa sasa hana namba ya kudumu.
Mchezaji mwenzake aliyefunga magoli manne tangu mwaka 2000 ni Jerry Tegete wa Yanga kwa sasa amehamia Mwadui FC ya Shinyanga.

Magoli ya straika huyo yalianza mwaka 2009 alipofunga goli pekee dakika ya 26, Simba ikishinda bao 1-0, Oktoba 31.
Alifunga magoli mawili 2010, Simba ikiifunga Yanga mabao 4-3 mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa Aprili 18 Ligi Kuu msimu wa 2009/10.

Msimu wa 2010/11 alifunga tena goli kwenye mechi ya watani wa jadi iliyochezwa Machi 2, 2011 timu hizo zilipotoka sare ya bao 1-1.

Bao hilo alilifunga dakika ya 73 likiwa ni la kusawazisha lile la Stefano Mwasyika alilolifunga kwa mkwaju wa penalti dakika ya 59.

Ni bao lililoingia kwenye rekodi ya kukubaliwa kutokana na mwamuzi Orden Mbaga kuangalia marudio ya televisheni kubwa iliyokuwa uwanjani. Awali alikuwa amelikataa.

Pia, straika huyo ni miongoni mwa wachezaji watatu waliofunga magoli kwenye mechi za watani hao wanaoendelea kuwemo kwenye vikosi, hivyo akiwa pamoja na Hamisi Kiiza na Simon Msuva.
Hata hivyo, Kiiza ambaye alifunga magoli matatu akiwa Yanga, aliichezea Simba kwa mara ya pili kwenye pambano la mahasimu hao jana.

Amerejeshwa tena mara ya pili akitokea Mtibwa Sugar, timu ambayo Simba ndiko ilikomsajili kwa mara ya kwanza.
Kwa mujibu wa viongozi wa Simba ni kwamba, alirejeshwa kutokana na timu yao kuwa na wachezaji wengi vijana ambao bado hajakomaa na wanahitaji uzoefu.

Hata hivyo, msimu huu hayupo kwenye kiwango chake cha kawaida kiasi kwamba kabla ya mechi ya jana alikuwa hajafunga goli lolote.

Pia amekuwa hana namba ya kudumu kwenye kikosi hicho na mara chache ama amekuwa hamalizi mechi, au kuingia kipindi cha pili
Septemba 20, 2014 kwenye mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu msimu uliopita kati ya Mtibwa dhidi ya Yanga, alifunga bao na kuibeba timu yake kushinda mabao 2-0 kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Novemba Mosi, 2014 kwenye Uwanja huo huo aliiokoa Mtibwa isizame mbele ya Simba alipofunga bao dakika ya 59 na kuzifanya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1. Aprili 11 kwenye Uwanja wa Manungu alipachika bao dakika ya 20 akiisaidia Mtibwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC.

Aliibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2009/10 kwa kufunga mabao 18, akiisaidia Simba kutwaa ubingwa msimu huo bila kufungwa mechi yoyote ile.

Mwaka 2011, alikwenda kucheza soka la kulipwa nchini DR Congo kwenye klabu ya DC Motema Pembe.
Alirejea na kujiunga na JKT Ruvu msimu uliofuata, kabla ya kutimkia Mtibwa na kurejea Simba msimu huu.