Lulu ya pamba inanyemelea kuwa historia katika Kanda ya Ziwa

19Feb 2016
Anceth Nyahore
Kahama
Nipashe
Lulu ya pamba inanyemelea kuwa historia katika Kanda ya Ziwa

MBALI na utajiri wa madini ya dhahabu na almasi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa nchini, kuna kundi kubwa la wakazi wake wanaojikita katika sekta isiyo rasmi.

Katika sura ya pili, kuna kundi kubwa la wakazi wake ni wakulima wa zao Pamba. Takwimu za Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), zinaonyesha Simiyu ndiyo inayoongoza kwa kuzalisha Pamba.

Uzalishaji chakula katika eneo hilo pia umejikita katika zao la mpunga na uvuvi wa samaki Ziwani. Kanda ya Ziwa ni eneo lililojulikana sana huko nyuma katika umahiri wa uzalishaji mazao ya shambani.

Kilio hasa kinachogusa hisia za umma kiuchumi ni kundi kubwa la ‘washika jembe’ amabao ni vijana, wanakimbilia katika shughuli mbalimbali za sekta isiyo rasmi na kutelekeza kilimo, ikiwemo zao maarufu la Pamba.

Baadhi ya sekta hizo zisizo rasmi katika Kanda ya Ziwa ni uchimbaji madini, kuendesha bodaboda na baiskeli maarufu
kama daladala.

KULIKONI SEKTA ISIYO RASMI?

Katika mazingirta yasiyo rasmi, inatokana na zai la pamba bei yake kushuka, licha ya kuwepo utitiri wa kampuni zinazonunua zao hilo huko Simiyu, Mwanza, Mara Shinyanga, Geita, Kagera na Tabora.

Awali katika miaka ya 1970 kulisheheni vyama vingi vya ushirika wa zao la Pamba na viwanda vya kuchambua nyuzi za kukamua mafuta, vilijengwa na kubadili hali halisi ya kipato cha wananchi wa maeneo hayo.

Yegela Fumbuka, ni mkazi wa kijiji cha Luguru wilaya ya Itilima, mkoani Simiyu. Anasema Kanda ya Ziwa ilianza kuwa na vyama vya ushirika tangu miaka ya 1950 chini ya kivuli cha Victoria Federation Co poration (VFC).

Wanaushirika hao walimudu kujenga viwanda na vinu vya pamba katika mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga na Tabora chini ya vyama vyao vya Ushirika. Miongoni mwa vyama vya ushirika vilivyovuma wakati huo ni Shirecu, Nyanza Cooparative Union (NCU) na Maracop.

Mzee Jongela Jibusa ni mkulima wa kijiji cha Bunambiyu katika wilaya ya Kishapu, anasema hivi karibuni sera ya soko huria na kuwepo utitiri wa wa kampuni zinazonunua zao hilo kumeshindwa kumnufaisha mkulima

Jibusa anatahadharisha kuwa, kuna balaa la kuwakatisha tamaa kutokana na pamba kuuzwa katika bei isiyomridhisha mkulima sokoni.

“Katika miaka hiyo (1970 na 1960) ilikuwa ni kawaida bei kutangazwa mapema mara tu, mkulima anapoanza kuuza pamba yake katika chama cha msingi hasa ile ya daraja la kwanza iliyokuwa ikifahamika Pamba ya Daraja A iliyokuwa na
bei ya juu ikilinganishwa na Pamba ya Daraja la Pili.

“Utasikia kupitia redioni au mkutano mkuu wa chama cha msingi kuwa msimu ujao bei ya pamba imepanda na itanunuliwa kwa
shilingi kadhaa kwa kilo,” anasema Jibusa.

Anaongeza kuwa kutangazwa bei hiyo kulikuwa kunawapa hamasa wakulima kuanza kuandaa shamba mapema, huku wakizingatia kanuni
10 za kilimo chao, ikiwemo kukata miti ya pamba shambani na kuteketeza kwa kuichoma moto.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa kuhusiana na soko la ndani la Pamba, hivi sasa huuzwa ikiwa chafu bila ya kujali madaraja yaliyopo na wanunuzi wake si makini.

Chama cha Wanunuzi wa Pamba na
Bodi ya Pamba (TCB) wanasema kuwa nchini bei yao imekuwa ikidorora pindi wanapokuwa katika soko la kimataifa, kwani ubora wa sasa una tofauti kubwa na ule wa miaka ya 1960 na 1970.

“Hivi sasa pamba ya Tanzania inapoingia katika soko la dunia kila ratili moja hukatwa centi 60 ya dola ya Marekani kwa madai ubora wake kuwa chini ikilinganishwa na ile ya nchi zingine kama vile Sudan, Misri na nchi za Mashariki ya mbali za Pakstan,India na Marekani,” anasema William Matonange kutokakampuni ya Kahama Oil Mill ya mjini Kahama.

NINI KIFANYIKE?

Muhammad Qureshi ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya kuzaslisha nguo ya Nida anayeshauri:”Ili kurejesha heshima ya Pamba ya Tanzania katika soko la ndani na lile la dunia sharti serikali ya awamu ya tano bila lelemama kuhakikisha wataalam wa kilimo wanawajibika kusimamia kanuni 10 za kilimo cha pamba, ili iwe na bei nzuri katika soko la dunia na kuinua uchumi wa taifa letu.”

Anasema kuna haja ya serikali kuona umuhimu wa kuwa na viwanda vya nyuzi kwa kilichokuwepo Tabora, jambo litakalohakikisha kunufaisha mkulima nchini.

Kuwepo kwa nstofahamu juu ya hatima ya bei ya mkulima takribani kila mwaka inaweza kuwa historia pale tu serikali,itakapoona umuhimu wakufufua ari ya mkulima kuendelea na kilimo hicho kwa kuwepo na bei nzuri huku wanunuzi nao wakinufaika na bei iliyopo katika soko la nje na kuinua uchumi wa taifa.