Kutoa huduma bora; utii kwa Serikali; bidii ya kazi; kutoa huduma bila upendeleo; kufanya kazi kwa uadilifu; kuwajibika kwa umma; kuheshimu Sheria za nchi; sambamba na matumizi sahihi ya taarifa za umma; kwa kutaja baadhi tu.
Haya yote kwa ujumla wake, hapo juu, na mengineyo yanaweza kuonekana vizuri kupitia Kifungu cha 6(a)-(j) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, inayotumika hivi sasa nchini, ilitungwa mwaka 1995 na kuanza kutumika rasmi Julai mosi mwaka huo, lengo likiwa ni kudhibiti tabia na mienendo ya viongozi wa umma, kufuatia kukosekana kwa Sheria ya kusimamia maadili ya Viongozi wa Umma tangu mwaka 1992.
Changamoto hii ilitokana na kufutwa kwa ile Sheria ya Kamati ya Kusimamia Utekelezaji wa Miiko ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1973 kufuatia mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa nchini. Viongozi wa Umma, tangu hapo, walikuwa hawazingatii tena suala la uadilifu hivyo basi, ndipo ikapelekea kutolewa pendekezo la kutungwa kwa Sheria mahususi ambayo itasimamia Maadili ya Viongozi wa Umma.
Tafasiri ya neno; "Kiongozi wa Umma"
Kwa mujibu wa Kifungu cha 4 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995, tafasri sahihi ya neno; "Kiongozi wa Umma" inajumuisha watu hawa wafuatao:
Rais wa Jamhuri ya Muungano; Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano; Rais wa Zanzibar; Waziri Mkuu; Waziri Kiongozi wa Zanzibar; Spika na Naibu Spika; Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano; Waziri, Naibu Waziri na Mkuu wa Mkoa;
Mwanasheria Mkuu; Jaji na Hakimu; Mbunge; Balozi Mwakilishi wa Tanzania nchi za nje; Katibu Mkuu Kiongozi; Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu; Katibu Tawala wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya; Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali; Katibu wa Bunge; Mkuu wa Jeshi la Ulinzi; lnspekta Jenerali wa Polisi na Kamanda wa Polisi wa Mkoa; Mkuu wa Jeshi la Kujenga
Taifa; Kamishna Mkuu wa Magereza; Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa; Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa; Meya, Mwenyekiti, Diwani au Mtendaji Mkuu wa Serikali ya Mitaa; Gavana, Naibu Gavana, Mwenyekiti, Mkurugenzi Mwendeshaji, Meneja Mkuu au Mkurugenzi Mkuu wa Shirika ambalo Serikali lina maslahi makubwa; Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume zote walioteuliwa kwa misingi ya kudumu; Viongozi wa Umma wanaosimamia Idara za Serikali zinazojitegemea;
Makamishna wa Kodi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania; Makamishna na Wakurugenzi wa Wizara za Serikali.
Halikadhalika, bila ya kuwasahau na wale Viongozi wa Umma ambao Mhe. Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete aliwaongeza katika Orodha ya Viongozi wa Umma alipokuwa madarakani mnamo mwaka 2013.
Fursa ya Raia kuifahamu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma
Kila mwananchi anatakiwa kuifahamu vema Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, si lazima awe kiongozi. Kwa kuifahamu Sheria hiyo, kwa sehemu kubwa, wataisaidia Mamlaka husika yenye Dhamana (Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma) kwa kutoa taarifa pindi ukiukwaji wa maadili unapofanywa na Viongozi wa Umma katika Taasisi na Sekta mbali mbali za Serikali mahala popote pale ndani na nje ya mipaka ya nchi.
Na kwa kuitumia fursa hii adhimu, kila raia anaweza kupata Elimu kuhusu Maadili ya Viongozi wa Umma kupitia njia mbali mbali kama vile: vipeperushi; redio; luninga; semina na matukio ya kitaifa ambayo kwa kawaida kama ilivyozoeleka hukusanya watu walio wengi kwa wakati mmoja, mfano: maadhimisho ya sherehe za wakulima nchini (nanenane); halikadhalika maonyesho ya biashara (sabasaba), ambapo Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma mara kadhaa imekua ikishiriki kwa kutoa elimu kwa umma katika banda lao maalum, ambalo wao kwa lugha nyepesi huliita "Banda la Maadili".
Kanuni za Maadili ya Mtumishi wa Umma
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ipo kwa mujibu wa Ibara ya 132(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, sambamba na Kifungu cha 18(1)-(7) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.
Kwa Viongozi wa Umma, Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inawajibu wa kutoa Semina elekezi za Mafunzo kwa Viongozi husika mara baada tu wanapokuwa wamechaguliwa au kuteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali katika Sekta au Taasisi fulani za Serikali, ili kuwang'amuza misingi ya maadili na mipaka ya utendaji kazi zao kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizowekwa kwa ajili ya mlengwa huyo mbali na wajibu wa Mtumishi wa Umma wa kutoa huduma bora, utii kwa Serikali, bidii ya kazi, kutoa huduma bila upendeleo, kufanya kazi kwa uadilifu, kuwajibika kwa umma, kuheshimu Sheria za nchi, ikiwemo na matumizi sahihi ya taarifa za umma, kama tulivyotangulia kuona hapo awali.
Sheria elekezi, kupitia Kifungu chake cha 9(1)-(6), inakwenda mbali zaidi na kuendelea kutung'amuza kuwa: kila Kiongozi wa Umma analazimika kutoa tamko la rasilimali na madeni.
Na kama haitoshi, Kifungu cha 11(1) na (2) cha Sheria hiyo hiyo ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 kimeainisha wazi mali zinazotakiwa kutajwa kuwa ni: fedha taslimu; fedha zilizopo katika taasisi za kifedha kama vile benki; hisa; nyumba; mashamba; magari; mitambo na mali nyinginezo.
Kiongozi anatakiwa kutoa tamko la mali anazomiliki yeye mwenyewe, mke/mume na watoto wake wote walio chini ya umri wa miaka kumi na nane ambao hawajaoa au kuolewa kama watakuwepo. Hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 9(1)(d) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.
Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni zinatakiwa kujazwa kila mwaka na kiongozi, ambapo hutumiwa fomu hizo na Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambazo pia zinapatikana katika Tovuti ya Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, yaani www.ethicssecretariat.go.tz.
Sheria inamtaka kiongozi kutolea tamko madeni yake ili ing'amuke kuwa kiongozi anamiliki mali zipi na amezipata kwa njia zipi mali hizo ukilinganisha na kipato cha kiongozi husika. Ikumbukwe kuwa, kwa mujibu wa Kifungu cha 12(1)-(2); na hata kile cha 14(1)-(7) vyote vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 ni marufuku kwa Kiongozi wa Umma kujinufaisha kifedha.
Hata hivyo, Kiongozi wa Umma kuwa na mali nyingi si dhambi kwani hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, [kupitia Ibara yake ya 24(1) na (2)], imetamka wazi kuwa kila raia wa Tanzania anayo haki ya kumiliki mali.
Cha msingi tu, kinacholindwa hapa, ziwe zimetokana na vyanzo halali na vyenye kutambulika kwa mujibu wa Sheria husika za nchi na sio mazingira mengine tofauti na hayo.
Sheria elekezi bado inatilia mkazo kwamba, kwa Kiongozi wa Umma kuamua kutojaza Fomu za Tamko la Mali na Madeni au kutoa taarifa za uongo ni kosa kisheria. Hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 15(a)-(b); na kile cha 27(2) na (3) vyote vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.
Baadhi ya hatua za kinidhamu ambazo zitaweza kuchukuliwa dhidi ya Kiongozi wa Umma kutokana na kukiuka Agizo hilo ni kama vile: kiongozi kuonywa na kupewa tahadhari, kushushwa cheo, kusimamishwa kazi, kufukuzwa kazi, kumshauri kiongozi ajiuzuru wadhifa unaohusu ukiukaji huo, sanjari na kupewa adhabu nyingine zinazoruhusiwa kwa mujibu wa sheria za nidhamu kuhusu wadhifa wa kiongozi na kuhimiza kuchukuliwa hatua kwa kiongozi kwa mujibu wa sheria za nchi zilizopo.
Lakini, pamoja na hayo yote, kabla ya kuchukuliwa mojawapo kati ya hatua zilizotajwa hapo juu, kwa kulingana na sababu za kibinadamu, bado kiongozi husika ataruhusiwa kujitetea kwa nini alichelewa kutoa tamko na iwapo sababu zake zitaonekana hazina msingi wowote, tokea hapo sheria husika itafuata mkondo wake dhidi ya kiongozi huyo kwa kupewa adhabu kulingana na uzito wa kosa lenyewe.
Jambo hili linaweza kuonekana kupitia kifungu cha 8(a)-(g) cha Sheria elekezi ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.
Taratibu za Utendaji kazi wa Sekretarieti
Utekelezaji wa Sheria ya Maadili unafuata "Orodha ya Viongozi wa Umma" ambayo imeainishwa katika kifungu 4(1) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Hii ni bila ya kuweka kando orodha ya viongozi ambayo Rais mstaafu wa awamu ya nne aliiongeza mwaka 2013 kipindi alipokuwa madarakani kama ilivyotangulia kuelezwa hapo awali.
Mwananchi yoyote ambaye ana malalamiko dhidi ya Mtumishi wa Umma, atakachotakiwa kufanya ni kupeleka malalamiko yake katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma zilizopo katika kanda husika ambayo hasa mhusika alikumbana na kadhi inayotafsiriwa kama: "uadilifu mbovu wa Kiongozi wa Umma".
Kwa upande wa Dar es Salaam, Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma (Makao Makuu) ipo Mtaa wa Ohio. Mhusika atasikilizwa lalamiko lake bila kutozwa gharama yoyote ile na hatua stahiki zinazofuata zitachukuliwa.
Aidha, mlalamikaji hatolazimika kutaja jina lake wala taarifa zake binafsi, kwa mujibu wa taratibu, hayo yote huwa ni siri kati ya mwananchi na Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Malalamiko yanaweza kuwasilishwa kwa njia ya simu, barua, au hata inapolazimu sana ana kwa ana.
Mara baada ya malalamiko hayo kupokelewa kutoka kwa mlalamikaji, hufanyiwa uchuguzi wa kina na ikibainika kama kweli kuna ukiukwaji wa maadili, kiongozi husika huitwa mbele ya Baraza la Maadili na kuhojiwa kutokana na tuhuma za ukiukaji wa maadili zinazomkabili, kisha Baraza husika hutoa mapendekezo, ambapo mapendekezo hayo hupelekwa moja kwa moja kwa Rais kwa hatua zaidi.
Kwa mujibu wa Ibara ya 5(1) na (2) Rais wa Jamhuri ya Muungano naye kwa nafasi yake ana wajibika kuchukua hatua zitakazoleta mabadiliko ya maadili yenye lengo la kuweka msingi wa kuongeza imani ya wananchi kuhusu Uadilifu wa Viongozi wa Umma na katika utaratibu mzima wa kutoa maamuzi ya Serikali na katika Sekta ya Umma kwa ujumla.
Viongozi ambao hawaguswi na Sheria elekezi, kwa mfano watendaji wa kata na vijiji, wao wanawajibika kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa katika Wilaya husika ambaye naye anawajibika kupitia Sheria elekezi.
Changamoto hii sugu ya Mmomonyoko wa Maadili kwa Viongozi wengi wa Umma, kwa kiasi kikubwa inatokana na viongozi hao kuwa na mgongano wa kimaslahi. Hii ikiwa na maana, tabia ya kupendelea kutanguliza maslahi binafsi badala ya kutanguliza maslahi ya umma mbele.
Hivyo basi, pindi, mwananchi anapokumbana na kadhia hiyo, toka kwa Viongozi wa aina hiyo, anachotakiwa kufanya ni kufika katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na kutoa taarifa kuhusu kiongozi/viongozi husika.
Tahadhari: Kwa mujibu wa Kifungu cha 27(1) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995, mtu yeyote ambaye bila ya sababu halali atatoa tuhuma dhidi ya Kiongozi wa Umma kwa mujibu wa fungu la 22 na lile la 23 huku akitambua ni uongo, atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani, atatozwa faini isiyopungua shilingi laki mbili na isiyozidi shilingi milioni moja au kifungo kisichozidi miaka miwili.
Lakini bado ifahamike kwamba, hakuna kiongozi wa Umma ambaye yuko juu ya sheria. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Ibara yake ya 13(1) na (2) inatamka wazi wazi kuwa: watu wote ni sawa mbele ya Sheria.
Ili kufikia lengo, Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma nayo kwa kulitupia macho ang'avu jukumu hili muhimu kwake haifanyi kazi kana kwamba ipo kisiwani.
Katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria, inashirikiana na Taasisi nyingine za Serikali kama vile Ofisi ya RPC, RPO, Mkuu wa Mkoa na ofisi nyingine nyeti ili kuleta tija kiutendaji.
Kutokana na ukweli usiogeuzika kuwa rushwa ni moja ya zao la vitendo vya ukiukwaji wa maadili, Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma hulazimika kushirikiana pia na Taasisi ya Kuzui na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa ajili ya kukamata viongozi wanaojihusisha na vitendo vya kuomba au kupokea rushwa. Hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 29 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.
Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, watumishi wake kwa ujumla wanapaswa kuzingatia maadili ya kazi, hususani kutunza siri za ofisi kama tulivyotangulia kung'amua hapo awali, kwani sheria elekezi imeipatia Mamlaka hiyo meno kushughulikia malalamiko ambayo, kwa jinsi na namna maudhui yake yalivyo, hayapaswi kuonyesha jina la mlalamikaji kwa sababu za kiusalama zaidi.
Kuna baadhi ya malalamiko ambayo, hata hivyo, kwa jinsi yalivyo ni lazima jina la mlalamikaji lijulikane. Ikitokea mwajiriwa anamlalamikia mwajiri wake kwa kumnyanyasa au kutomlipa haki zakem kwa mfano, hapo lazima jina la mlalamikaji lijulikane ili mwajiri atambue ni nani anayelalamika ili aweze kupata haki yake stahiki kwa mujibu wa Sheria.
Usiri huu wa taarifa za wananchi unaozungumzwa hapa, bado utaendelea kuwepo kwa kiwango cha juu sana, isipokuwa itategemea zaidi na aina ya malalamiko yenyewe yaliyofikishwa mbele ya Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa ajili ya maamuzi.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 20(2) na (3) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995, sambamba na Kanuni ya 6(1)-(2); na ile ya 7(1)-(3) zote za Kanuni za Maadili ya Viongozi wa Umma za mwaka 199, kila mwananchi wa kawaida ana haki ya kuona Daftari la Mali na Madeni ya Viongozi wa Umma ila jambo hili litafanyika kwa kuzingatia masharti muhimu matatu.
Kwanza, ni lazima mwananchi husika awe ana lalamiko dhidi ya kiongozi anayetambulika, Kamishna wa Maadili ajiridhishe kwa kina na lalamiko/shutuma zilizofikishwa mezani kwake, na mara baada ya kujiridhisha mwananchi husika atalipa kiasi cha shilingi 1,000/= kwa ajili ya kuona daftari hilo kama lilivyokuwa kusudi lake la awali.
Baada ya kuangalia taarifa alizotaka juu ya mali za Kiongozi wa Umma, mwananchi huyo katu hatoruhusiwa kutumia taarifa hizo kwa matumizi yake binafsi. Zitabaki kuwa ni siri kati yake na Ofisi ya Mamlaka yenye Dhamana tu na sio tofauti na hivyo.
Kwa kuamua kufanya kinyume na utaratibu huo, mwananchi husika atakuwa anafanya kosa kwa mujibu wa Sheria na mara baada ya kutiwa hatiana atatakiwa kulipa faini ya shilingi 10,000/= au kwenda jela kwa muda usiozidi miaka miwili au ikibidi vyote kwa pamoja.
Kiongozi aliyekiuka maadili naye anaweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria nyingine kama ilivyofafanuliwa hapo awali kupitia kifungu cha 29 cha Sheria ya Maadili ya Utumishi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 kuwa matumizi ya sheria nyingine yanaruhusiwa ikiwemo Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na sheria au kanuni nyinginezo.
Ikumbukwe kuwa wananchi ndiyo wenye nafasi kubwa katika kusaidia Mamlaka yenye Dhamana kutekeleza Sheria hii ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 katika kufichua maovu mbali mbali ya Viongozi wa Umma, kwa kuwasilisha malalamiko hayo katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa hatua zaidi za kiuchunguzi ili nayo ili mwisho wa siku iweze kufanya maamuzi yenye kuleta tija kwa manufaa ya Umma.










