Zanzibar yahamisha soko la utalii kwa Wachina, Wahindi

19Feb 2016
Mwinyi Sadallah
Zanzibar
Nipashe
Zanzibar yahamisha soko la utalii kwa Wachina, Wahindi

BAADA ya karafuu kusuasua sokoni, sehemu kubwa ya egemeo la uchumi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), limeelekezwa kwenye utalii.

WATALII Ulaya, wakipata maelezo kuhusu historia ya Kituo cha Biashara ya Utumwa, walipotembelea sehemu waliokuwa wakihifadhiwa watumwa kabla ya kusafirishwa nje ya nchi, huko Mkunazini Mjini Zanzibar. (Picha zote na Mwinyi Sadallah).

Ni mabadiliko yaliyoendana na kupanuliwa huduma za utalii, ikiwemo uwekezaji mkubwa wa hoteli za namna tofauti, pia huduma za waongoza watalii wenye viwango.

Utalii ni sekta iliyofufua matumaini mapya ya Wazanzibari katika kuinua kipato chao, ikihusisha wananchi wa kada mbalimbali kama vile wakulima, wafugaji, wavuvi na wafanyabiashara.

Mageuzi ya kuhamisha uchumi wa Zanzibar kutoka kuegemea karafuu, zao ambalo soko lake lilikuwa linafifia hadi kwenye utalii ni kazi iliyofanyika chini ya Rais
Dk.Salmin Amour katika zama za utawala wake.

Ndani ya muda mfupi, matunda ya kuuinua utalii yalijitokeza kwa kufanikisha Mpango wa Serikali wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini kwa Wananchi (MKUZA).

Wakati Zanzibar inang’ara kupitia utalii, soko lake kubwa la watalii waliozuru visiwani humo ni wanaotoka nchi za Uingereza, Ujerumani, Italia, Marekani na Afrika ya Kusini.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Issa Mlingoti anasema SMZ sasa imefungua milango mipya ya masoko ya watalii, ikiwa sehemu ya mkakati mpya wa kujineemesha kibiashara.

Anasema sasa kuna soko jipya la watalii kutoka mataifa ya China, India, Israel, Russia na Ukraine.

Katika mtandao wa soko hilo jipya, watalii kutoka ukanda huo hawakuwa maarufu sana katika wingu jipya la biashara ya utalii kimataifa.

Mlingoti anasema soko la India lina umuhimu mkubwa na ndiyo maana wameamua kufungua Ofisi mjini Mumbai, lengo ni kutangaza utalii wa Zanzibar kwa karibu.

Anasema wameweka mkakati wa kuwavuta watalii kutoka China kutembelea Visiwa vya Unguja na Pemba.

“Tangu kuasisiwa rasmi ofisi hiyo, tayari imeshaandaa ziara za wakala wa kampuni za kusafirisha watalii kutoka India, kuja Zanzibar kuona vivutio vya utalii, mbali na fukwe na mji mkongwe wa Zanzibar ambao ni urithi wa dunia,” anasema.

Anasema kampuni za uwakala wa utalii zimefika kuona vivutio na fursa ziliopo Zanzibar, lengo ni kuangalia iwapo vivutio hivyo vinakidhi hamu na kiu ya wateja wao.

WATALII WA ISRAEAL

Kwa mujibu wa Mlingoti, huo ni utekelezaji sera wa za utalii Zanzibar iliyoasisiwa mwaka 2010, ni kwamba kila mwananchi anufaike nayo katika kipato binafsi.

Anasema omesadia kuongeza masoko mapya ya utalii, baada ya watalii wa Israel kuongezeka kufikia 7,546 mwaka 2014 kutoka 3818 mwaka 2013.

Anaongeza kuwa wakati soko la Poland lilifikia watalii 4,083 mwaka jana kutoka watalii 3163 mwaka juzi, kuna hatua nyingine mpya za kuwepo watalii 150 wanaoingia ndege ya moja kwa kila wiki Zanzibar, utaratibu ulioanza wiki moja iliyopita.

Mlingoti anasema ni matunda ya mpango wa serikali wa kuongeza masoko katika sekta hiyo, kwa kushirikiana na kampuni ya kimataifa ya kusafirisha watalii.

“Kupanuka kwa wigo wa masoko ya utalii, kutaondoa utegemezi wa soko la Ulaya ambalo kwa sasa linakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kutetereka kwa uchumi,” anasema Mlingoti.

KAMISHENI YA UTALII

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Saleh Ramadhan Feruz, anasema mafanikio hayo yanakwaza na changamoto kubwa ya kuhakikisha usalama kwa wageni wanaotembelea Zanzibar.

Anasema kuwepo kero kubwa ya watembeza watalii wasiosajiliwa na mamlaka zao na kusababisha kujipenyeza watu wasiokuwa waaminifu na kudokoa vitu vya wageni na kuleta picha mbaya kwa wageni wanaotembelea Zanzibar.

Feruzi anasema mkakati wa kupambana na tatizo hilo umeanza kufanyika, baada ya SMZ kupitisha sheria ya kuanzisha kikosi cha ulinzi katika sekta ya utalii, ikishrikiana na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) na Polisi Zanzibar.

Anasema maeneo yanayolengwa ni hoteli na fukwe za kitalii, ili kuhakikisha zinakuwa salama na kufanikisha mpango wa kuwavutia wawekezaji katika sekta ya utalii Zanzibar.

Feruzi anasema hadi sasa utalii Zanzibar unchangia asilimia 27 ya Pato la Taifa na kutoa ajira kwa watu 13,000 mbali na watu 44,000 wanaonufaika na sekta hiyo katika namna tofuati.

MAONI YA WAKAZI

Wakazi wa Mji Mkongwe eneo lililoko Unguja, wanalalamika kwamba pamoja na mafanikio ya sekta hiyo, bado kuna changamoto iiliyopo ya uhaba wa maji.

Mji Mkongwe ni kivutio kikubwa cha utalii Zanzibar na wamiliki wengi wa hoteli katika ene hilo wanalalamika kuwa, mitaa mingi iko katika mazingira ya giza na kuhatarisha usalama wa wageni.

Malalamiko mengine yaliyopo ni kwamba Chuo cha Maendeleo ya Utalii cha Maruhubi Zanzibar, bado hakijajengea uwezo wa kutisha kutoa wataalam mahiri, jambo linaloifanya Zanzibar kutegemea wataalam wa utalii kutoka nchi jirani.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendeleza Mji Mkongwe, Issa Saliboko, anasema SMZ imeanza kufanya uchambuzi yakinifu wa mradi wa kuondoa tatizo la maji, kufunga taa za mionzi ya jua na kuondoa msogamano wa magari.