Angalizo la TFDA kuhusu mazoea ya kula vichafu

18Feb 2016
Dar
Nipashe
Angalizo la TFDA kuhusu mazoea ya kula vichafu

DAR ES SALAAM ni miongoni mwa miji ambayo katika maeneo yake, chakula kinauzwa katika mazingira yasiyo ya kuridhisha kifaya. Baadhi ya maeneo hayo ni masoko rasmi na yasiyo rasmi.

Ugali wa dona na mboga ikiwa tayari kwa kuliwa Chakula kikiwa tayari kwa kuliwa. ( [PICHA MTANDAO).

Matokeo yake, jiji hilo limegubikwa na chakula kuuzwa katika mazingira machafu, baadhi ya waandaaji wa chakula nao wanakiandaa katika mazingira machafu na yanayohatarisha maisha ya mlaji.

Kutokana na hali hiyo, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), imeamua kufanya kamperni ya kuelimisha Watanzania wote wa jumla, namna bora ya kuandaa chakula katika hali ya usalama na muda wote mnaepuka magonjwa ya kuambukiza, kama vile kipindupindu na homa ya matumbo.

Mtaalam wa Chakula wa TFDA, Immaculata Justine, anaeleza mambo muhimu ya kuzingatia katika utayarishaji wa chakula.

Anakieleza chakula salama kuwa ni kile ambacho hakijachafuliwa na vimelea vya maradhi, kemikali au takataka nyingine kama vile mchanga, majani, wadudu na madini, katika kiasi ambacho kinaweza kusababisha madhara kwa mlaji.

Immachulata anasema kuwa, chakula kisicho salama kina uwezi wa kusababisha magonjwa mbalimbali, kama vile kuhara, kipindupindu na hata kusababisha vifo.

Anasema, hayo ni mazingira yanayoiathiri jamii kiafya na kiuchumi, hivyo kurudisha nyuma jitihada za maendeleo yake. Uchafuzi wa chakula unaweza kusababishwa na vimelea vya maradhi kutoka katika mazingira, wanyama, wadudu au binadamu.

Aidha, uchafuzi wa vyakula unaweza kusababishwa na sumu asili, mayai ya vimelea vya maradhi au mabaki ya viatilifu pamoja na mabaki ya dawa zinazotumika kutibu mifugo.

Madhara yatokanayo na matumizi ya chakula kilichochafuliwa na vimelea vya maradhi, huonyesha dalili kama vile; kuumwa tumbo, kuhara, kuhara damu, kichefuchefu na kutapika.

Uchafuzi wa chakula, husababishwa na kutozingatiwa kwa kanuni bora za utayarishaji chakula salama majumbani, hotelini na katika migahawa.

“Ili kufanikisha utayarishaji wa chakula salama na hivyo kuepuka madhara yatokanayo na kula chakula kisicho salama.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeainisha mambo matano muhimu ya kuzingatiwa,” anasema Immaculata. Anataja mambo hayo yaliyoanishwa na WHO, ni kuzingatia usafi na tabia binafsi wakati wa kutayarisha chakula.

Jambo hilo linajumuisha hali ya usafi na tabia binafsi ya mwandaaji wa chakula, ambayo nayo inajumuisha mambo kadhaa.

Immaculata anasema kuwa, afya binfasi kwa upana wake inahusisha kunawa mikono kwa maji safi na sabuni mara tu baada ya kutoka chooni na kabla ya kuandaa au kula chakula.

Pia anasema hatua hiyo ya usafi inayoainishwa na WHO, inaainisha mambo kama vile baada ya kugusa chakula kibichi, ikiwemo nyama za aina tofauti, ng’ombe, samaki na kuku; kuokota vitu mbalimbali; kugusa takataka; kukohoa; kupiga chafya; kugusa sehemu yoyote ya mwilil kufanya usafi; na kugusa vyombo vichafu.

“Ni muhimu kuepuka kushika kwa mikono chakula kilicho tayari kuliwa, isipokuwa kwa kutumia kijiko au chombo kingine kinachofaa.

Mwandaaji wa chakula anashauriwa kuwa msafi muda wote, kuvaa mavazi safi wakati wa kuandaa chakula na kuepuka kushika sehemu za vyombo ambavyo hugusana na mdomo wa mlaji,” anabainisha.

Anasema, jingine ni kuhakikisha maeneo yote ya kuandalia na kuhifadhi chakula kama vile jokofu na kabati, yanapaswa kutunzwa katika hali ya usafi.

Hiyo inaendana na kudhibiti wadudu kama vile mende na wanyama wadogo kama vile panya, hawapaswi kuwepo katika maeneo ya kutayarishia chakula, kwani inabeba vimelea vya maradhi.

Sharti lingine lialotajwa hapo ni vyombo vya kuandalia chakula kama vile sufuria, sahani, vikombe, visu na meza za kuandalia chakula, vinapaswa kuwa katika hali ya usafi wakati wote wa maandalizi na wakati wa kutoa huduma ya chakula.

WHO inawawajibisha waandaaji wa chakula pia kuzingatia kutenganisha chakula kilichopikwa na kibichi na inahimza chakula kilichopikwa kihifadhiwe katika sehemu safi, ili kuhakikisha kuwa hakichanganyiki na chakula.

Sababu kuu inayowekwa katika dhana ya kujenga mpaka huo ni kwamba, chakula kibichi kina uwezekano mkubwa wa kuwa na vimelea vya magonjwa.

Wakati wa kupanga vyakula katika jokofu, inaaswa vyakula vibichi viwekwe katika safu za chini ili kuzuia majimaji yake kuchuruzika na kuingia kwenye vyakula vilivyopikwa.

“Vifaa vya kukatia nyama mbichi au samaki wabichi, vinapaswa kuoshwa vizuri na kuhifadhiwa katika hali ya usafi. Inashauriwa kutumia vyombo tofauti kwa vyakula vilivyopikwa na vile vibichi,” anabainisha ofisa huyo wa TFDA.

Jingine linalohimizwa katika anjenda hiyo, ni kuhakikisha chakula kinapikwa hadi kuiva vizuri na miongni mwa vyakula anavyovitaja kama mfano kielelezi ni nyama za aina mbalimbali na mayai. Yote hayo hujenga matokeo chanya katika kusimamia mapishi husika.

Anasema, vyakula vilivyopo na viporo, vinatakiwa kuchemshwa kikamilifu ili kuua vimelea vya magonjwa. Hatua nyingine an ataja kuwa ni kuhifadhi chakula kilichopikwa kwa uangalifu ili kiliwe mara baada ya kupikwa kingali cha moto na anatahadharisha kuwa, endapo chakula hicho hakitaliwa mara baada ya kupikwa, mbadala wake ni kiwekwe kwenye chombo kinachohifadhi joto au kwenye jokofu, ili kuzuia kuzaliana vimelea vinavyosababisha maradhi.

“Wakati wa kupanga vyakula katika jokofu, vyakula vibichi viwekwe katika safu za chini ili kuzuia uchafuzi wa vyakula vilivyopikwa,” anasema Immaculata.

Pia, anataja njia nyingine ni kutumia maji na malighafi safi, kwani ni muhimu kuhakikisha maji ya kunywa ni safi na salama, matunda na mboga za majani zimeoshwa kwa maji safi na salama.

Kwa vyakula vilivyofungashwa, angalizo lililopo ni kwamba mlaji anapaswa kuhakikisha kuwa muda wa matumizi haujapita na vifungashio viko katika hali nzuri, bila kupasuka, makopo hayajapata kutu, hayajatoboka, hajapondeka au kutuna.