Taasisi hiyo iitwayo Sikika, ambayo inafanya kazi katika wilaya 10 nchini, ikiwamo Kondoa mkoani Dodoma ilikoanza mwaka 2011.
Mkurugenzi wa Sikika, Irinei Kiria, anasema mwaka huu wamepanga kuzifikia wilaya 20 nchini na ilianza kutekeleza shughuli zake katika kata tano za wilaya ya Kondoa, ikijumuisha pamoja na kata zilizokuwepo kwenye wilaya mpya ya Chemba.
Mwaka 2012 Sikika ilianza na jukumu la kuhamasisha uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi wanaowahudumia.
Kiria anasema hilo walilitekeleza kwa kufanya mkutano na wadau wa afya wilayani Kondoa, wakiwemo wananchi, Watendaji wa Kata, Watendaji wa Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya Kondoa, asasi za kiraia, madiwani, Mkuu wa Wilaya na ofisi yake na watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.
Anasema baada ya kutoa ripoti mbalimbali za utendaji zilizofichua uovu wa watumishi wasiyo waadili, Sikika lilizuiliwa kufanya kazi katika wilaya hiyo.
Kiria anasema kuwa walipingwa na Baraza la Madiwani wa wilaya hiyo kwa madai wanatoa taarifa za uongo.
Kupitia barua waliyoandikiwa walipewa tuhuma nne za kuwadhalilisha madiwani kwa kuwaambia hawajasoma na hivyo kushindwa kusimamia halmashauri
Tuhuma ya pili ni kusambaza vijarida kwa wananchi vyenye taarifa isiyo sahihi vya ripoti ya mwaka 2012.
Pia walituhumiwa kufundisha katika mafunzo kuwa kamati ya ukaguzi wa ndani inapaswa kuwa na mwenyekiti ambaye hatokani na uteuzi wa halmashauri
Anasema walituhumiwa kutumia lugha za kejeli dhidi ya viongozi.
KAULI YA MADIWANI
Wakati Sikika wakiendelea na shughuli zao katika wilaya nyingine nchini, bila kuondoa ofisi zao katika wilaya ya Kondoa, Baraza la Madiwani lililochaguliwa Oktoba mwaka jana, lolipendekeza Sikika kurudi.
Wakiwa kwenye kikao cha Baraza hilo kilichoketi Februari 5 mwaka huu, madiwani hao kwa kauli moja waliazimia lkulirudisha shirika hilo kwa madai kuwa lilikuwa likiisaidia serikali kutekeleza majukumu yake.
Pia walieleza masikitiko yao juu ya uamuzi wa kuliondoa Sikika na kuahidi kuendelea kufanya nalo kazi ili kuinua sekta ya afya katika wilaya hiyo.
RC AWAUNGA MKONO
Katika kikao hicho cha Baraza ambacho mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa, ameahidi mkoa wake kushirikiana na shirika hilo na kutoa wito kwa mashirika mengine kushiriki kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Anasema kufanya kazi katika wilaya hiyo kutasaidia kuboresha sekta hiyo na kubaini ubadhilifu wa fedha unaofanywa na watendaji wasio waadilifu.
"Niwapongeza madiwani kwa uamuzi wenu wa kulirudisha Sikika baada ya kuwafukuza pale mlipobaini wanafichia ubadhilifu wa fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya afya pamoja na huduma zinazotolewa katika sekta hiyo, "anasema Chiku.
Anawataka madiwani hao kuzipokea taasisi nyingine za kiraia zinazofanya kazi kama za Sikika ili kuboresha utendaji katika halmashauri hiyo ili wananchi wapate huduma bora.
"Sikika ni kama kioo kwetu sisi serikali. Mpishi hawezi kujikosoa pale anapopika ila anayeko nje anaweza kuyaona mapungufu yetu.
“ Tunawashukuru Sikika kwa kufanya kazi pamoja nasi na hata pale mlipohitajika tena baada ya kufukuzwa hamkusita kuitikia wito," anasema.
Hamida Asharafu, mkazi wa Kondoa anasema Sikika lilikuwa likisaidia kuisukuma serikali kutekeleza wajibu wake katika sekta ya afya na kwamba walikuwa wakipatiwa huduma bora lakini baada ya kufukuzwa utendaji wa serikali ulishuka.
Anasema walikuwa wakipatiwa huduma bora na watumishi wakihofiwa kuripotiwa na Sikika anaongeza:“Baada ya Sikika kufukuzwa tu watumishi wa serikali walianza kuzembea kazi na kutujibu vibaya wateja hasa hospitalini.”
Naye Juma Hashim, anasema walichukizwa na kitendo cha madiwani kuwafukuza madiwani na kulazimika kuwatahadharisha viongozi waliowachagua kwenye uchaguzi uliopita.









