Dk. Simwaza: Maradhi kinywa yana kila hatari kwa uhai wa mjamzito

24Aug 2023
Beatrice Shayo
Nipashe
Dk. Simwaza: Maradhi kinywa yana kila hatari kwa uhai wa mjamzito
  • •    * Kwa mwanaume; kupooza, moyo, kansa…
  • •    * Ukifungua mdomo; anajua ya leo, yajayo

AFYA ya kinywa na meno hasa kwa wajawazito, inatajwa isipozingatiwa, mtu anaweza kujifungua mtoto njiti.

Mtaalamu Dk. Katanta Simwanza.

Mtaalamu Dk. Katanta Simwanza, anaiambia Nipashe kwamba afya ya kinywa na meno, kila mtu anawajibika kuizingatia kwa usalama wa afya yake kwa jumla.

Anataja, mjamzito kinga yake inakuwa imepungua, hivyo hata mdomoni, afya yake inakuwa dhaifu, wadudu huzaliwa na kushambulia fizi.

“Baada ya kushambulia fizi hizo, fizi hutoa sumu ambayo ikiingia kwenye damu inakwenda kushambulia ‘placenta’ yaani mfuko ambao unamlea mtoto,” anasema Dk Simwanza.

Anataja sababu ya watoto kuzaliwa njiti, ni mama anapokuwa na afya duni kinywani, pia  asipozingatia usafi wake.

“Kuna vimelea vingine vikifika kwenye moyo vinasababisha kinamama wanapata kifafa cha ujauzito na wengine kupoteza maisha,”anasema  Dk Simwanza.

Anaeleza changamoto nyingine ni meno kuoza na kwa wajawazito inakuwa tatizo kubwa, kwani inaweza kusababisha mimba kuharibika au kuzaliwa kabla ya siku zake.

“Kuoza kwa meno kunaweza kumsababishia mama kupata majipu na kupata changamoto nyingi na hatimaye kupata kifafa cha uzazi na hata kupoteza maisha yake,”anasema Dk Simwanza.

KUBAINI SHIDA IJAYO

Dk. Simwanza ambaye ni Mkurugezi Mwandamizi wa Taasisi ya Miracle Corners of World, Tanzania anaeeleza kitaalamu, daktari ana uwezo  wa kukagua kinywa cha mtui akabaini changamoto ya miaka 20 ijayo. 

Pia, anasema kinywa hutoa viashiria vya saratani ya tumbo. Anaendelea: “Daktari wa meno akiangalia meno yako anaweza kujua wakati unapatikana wazazi wako walikuwa na maambukizi ya… (maradhi) kutokana na meno yako yalivyokuwa.”

Kwa mujibu wa Dk. Simmwanza, mtaalamu anamtambua kwenye hatari ya maradhi saratani,  kisukari, shinikizo la damu, au maambukizi ya magonjwa yatokanayo na ngono, au kwa mtoto anayefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Huku akisisitiza kinywa kina magonjwa mengi, anasema baadhi ya vitendo vinavyofanyika kwenye afya ya kinywa vinaweza kusababisha mtu akapata maambukizi ya vimelea akitoa mfano saratani ya shingo ya wa kizazi (HPV), pia saratani ya koromeo.

UMUHIMU WA KINYWA, MENO

Dk. Simwanza anasema, afya ya kinywa na meno ni eneo muhimu kuzingatiwa akihimiza: “Kinywa kinatuwezesha kula chakula na hata mmeng’enyo wa chakula inaanzia hapo. Kinywa pia kinatoa nafasi kinapokuwa salama watu kuwasiliana.”

Anasema Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Shirika la Afya Duniani (WHO) imetenga Machi 20 ya kila mwaka ni siku ya kuhimiza jamii duniani kuchukua hatua za kujikinga na kulinda afya ya kinywa na kwa miaka mitatu ikiwa na kaulimbii”jivunie kinywa chako, kithamini na kukitunza.”

Anasema, kila mtu anashauriwa kuchunguza kinywa chake, pia taasisi na jamii zinahimizwa kuendelea kutoa elimu ya afya ya kinywa, huku matibabu yakitolewa katika vituo vya afya.

“Tunatakiwa kutambua katika masuala ya afya ya kinywa WHO alieleza daktari mmoja afya ya kinywa na meno anatakiwa kuwahudumia watu 75,000, kwa mwaka kwa Tanzania daktari mmoja anahudumia watu 125,000 kutokana na uhaba wa watumishi,”anasema.

KOSA LA MSWAKI ASUBUHI 

Anasema kiafya inashauriwa mtu kupiga mswaki walau mara mbili kwa siku na kama ikiwezekana, mtu apige mswaki mara moja muda wa kwenda kulala.

“Kupiga mswaki asubuhi ni sawa na bure, kwa sababu wadudu wanakuwa wameshameng’enya chakula na kutoa sumu na kusababisha magonjwa ya kinywa,”anasema.

Anaeleza lengo la kupiga mswaki ni kuondoa masalia ya bakteria waliobaki mdomoni wasiyatumie kwa ajili ya kusababisha madhara, akifafanua bakteria wakiyatumia na kushiba, wanajisaidia na ndipo inakuwa sumu iliyolala mdomoni.

“Ukiona mtu ananuka mdomo sio kwamba mdomo unanuka. Mdomo unanuka vinyesi vya masalia yaliyosababishwa na hao bakteria wametoa kinyesi, mkojo, maji na takataka zote wanakuwa wameziweka pale mdomoni ndio maana utakuta mtu ananuka mdomo,”anasema Dk. Simwanza.

Anasema katika kuzuia meno kuoza wanahimizwa kupunguza ulaji wa vyakula na vinywaji vyenye sukari kila mara, pombe na matumizi ya sigara, kwani yana madhara makubwa kwa afya ya kinywa.

KUEPUKA MARADHI 

Dk Simwanza anasema, ili kuepuka maradhi ya kinywa, watu wanapaswa kupiga mswaki walau mara mbili kwa siku.

“Meno yasitumike kama kifaa cha kufungulia vitu vingine, lakini wajitahidi kufanya uchunguzi wa kinywa walau mara mbili kwa mwaka,”anasema Dk Simwanza.

Anasema kwa mzazi au mlezi anatakiwa kuhakikisha mtoto anavyoota meno kuanzia miezi sita jino analisafisha kila mara na mtoto anapokuwa na umri kati ya miaka sita hadi tisa, anaanza kujifanyia usafi wa kinywa.

“Kuna baadhi ya kinamama wana tabia ya kumuacha mtoto amelala na nyonyo mdomoni ,” anatamka na kuendelea: “Asilale akiwa analinyonya nyonyo anaweza kupata changamoto ya afya ya kinywa.”

Anashauri kuna haja ya kuhakikisha kunakotolewa huduma za afya za jumla, suala la kinywa nalo liunganishwe, hata kuwezesha huduma ikiwafikia wengi, pia kupunguza usumbufu katika upatikanaji huduma hiyo.

Anawashauri kinamama wanapokuwa wajawazito, wahakikishe wanapata huduma ya afya ya kinywa na meno na hata baada ya kujifungua, ili kujilinda maambukizi ya magonjwa mbalimbali mdomoni.

Daktari huyo anataja stadi za kidaktari kuna wakati anaweza kuchunguza meno   na kubaini rangi yake ilivyo, mara moja anapata majibu ya usalama wa mtoto katika nyumba anayoishi, ikiwamo wa ukatili wa kijinsia.

Anasema katika afya ya kinywa, baadhi ya wanaume wanaugua magonjwa ya kupooza viungo, mzizi wa tatizo ukiwa katika afya ya kinywa, moyo ukashambuliwa na kusababisha shida kwenye ubongo.

Daktari Simwanza anahitimisha kwa angalizo kitalaamu, kwamba afya ya kinywa na meno, badi imo katika kundi la magonjwa yasiyoambukiza, ambayo hayapati kipaumbele kikubwa.