Kikao hicho cha wakuu kinafanyika Johannesburg kuanzia jana hadi kesho kikiwaleta wanachama wa kundi hilo ambao ni Brazil, India, China na Afrika Kusini, wanaoshirikiana kwenye maeneo mbalimbali kuanzia uchumi, teknolojia hadi diplomasia.
Tangazo hilo lilimaliza uvumi wa miezi kadhaa kuhusu iwapo nchi hiyo ingemkaribisha Putin ili kumkamata kwa hati ya kimataifa, kiongozi huyo anayetuhumiwa kuivamia Ukraine.
Afrika Kusini ilikabiliwa na mkanganyiko katika kuandaa mkutano huo kwa sababu, kama mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC), chombo hicho kilitoa hati ya kumkamata Rais Pitin, kwa mujibu wa Reuters.
Hati ikitolewa Machi 2023, Afrika Kusini ingelazimika kumkamata Putin kwa madai ya uhalifu wa kivita unaofanywa na Urusi kwa kuivamia Ukraine.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, ndiye anayeiwakilisha nchi hiyo kwenye mkutano huo wa kilele wa BRICKS Johannesburg , Agosti 22-24 badala ya Putin, inasema Reuters..
Kufungiwa nje Putin kulifuatia mazungumzo kati ya Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa na viongozi wa vyama vya siasa kutoka kundi la nchi zinazoinukia kiuchumi BRICS kuangalia uwezekano wa kumweka kando asije kunasa nyavu za ICC.
Ikulu ya Kremlin wakati huo ilisema Putin atashiriki kwenye mkutano wa kilele wa BRICS kwa njia ya video.
UMUHIMU WA BRICS
Licha ya Putin kubaki nyumbani mataifa hayo ni muhimu kwa Moscow, kwani ni kama sehemu yake ya kujiegemeza. Kwa Urusi, mkutano wa kilele wa BRICS ni muhimu mno. Kwanza ni fursa ya kuonyesha kwamba haihitaji tena nchi za magharibi kufuatia jitihada za kuitenga Moscow katika jukwaa la dunia kutokana na vita vyake huko Ukraine.S
BRICS ni kama jukwaa muhimu la kuikosoa Marekani na kwa njia nyingine mdomo wa kuisema Urusi kutoka na kukandamizwa na nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani.
Kwa hiyo mtandao wa jarida la The Conversation Africa Edition, unaofuatilia mkutano huo Afrika Kusini unasema:” Wakati viongozi wa kundi la BRICS ambalo lina mataifa makubwa kiuchumi yanayoinukia - Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini, wanapokutana Johannesburg kwa siku mbili kuanzia jana, watunga sera za kigeni huko Washington Marekani bila shaka watakuwa wakisikiliza kwa makini kinachoendelea.”
Unaongeza kuwa kundi la BRICS limekuwa likipinga baadhi ya kanuni muhimu za uongozi wa kusimamia mataifa mengine wa Marekani katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa upande wa kidiplomasia, imedhoofisha mkakati wa Ikulu ya White House kuhusu Ukraine kwa kuyakabili maelekezo ya kutumia vikwazo dhidi ya Urusi.
Aidha, kiuchumi, imejaribu kuibana Marekani kwa kuondokana na kuienzi sarafu yao kwa kudhoofisha matumizi jukumu la Dola kama sarafu kuu na ya msingi duniani.
KUONGEZA NGUVU
Na sasa kundi hilo linaangalia kupanuka na kuongeza wanachama rasmi hadi wafike 23, hatua kama hiyo ikiwa BRICS ikiziangalia Iran, Cuba au Venezuela mataifa ambayo yataimarisha upinzani wa kundi hilo dhidi ya Marekani.
Leo Zipo Brazili, Russia, India, China na Afrika Kusini.
Nchi za BRICS zinaungana karibu ili kusimamia maslahi ya pamoja ya maendeleo na jitihada za mpangilio wa kuhakikisha dunia inashikamana kwa pande nyingi siyo kuwa chini ya taifa moja lenye nguvu ili kuepusha kuwa na mbabe mwenye mamlaka anayotawala wote.
Hata hivyo, kuimarika kwa BRICS kunaligeuza kundi hilo kuwa na nguvu ya mazungumzo yenye uzito ambayo sasa inapinga malengo ya kisiasa na kiuchumi ya Washington, linakuwa kama kitu kizito kinachoigonga Marekani kichwani.
Kwa hiyo zama za kuipuuza BRICS kama nguvu kuu ni jambo ambalo Marekani haitalifanya na sasa ni kuwa na mwelekeo wa pengine wa kujijenga upaya, unashauri mtandao wa The Conversation.
KULETA MAPYA
Mwanzoni mwa ushirikiano wa BRIC mwaka 2008, kabla ya Afrika Kusini kujiunga mwaka 2010 na kuongeza "S" kutoka kwenye BRIC- wanachama waliamini kuwa kuwapo kwa kundi hilo kunaweza kusababisha mvutano na watunga sera ambao waliiona Marekani kama "taifa muhimu na la lazima duniani."
Kama Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Brazili, Celso Amorim, alivyosema wakati huo, "Tunapaswa kuendeleza utaratibu wa kidemokrasia zaidi wa kidunia kwa kuhakikisha ushiriki kamili wa nchi zinazoendelea katika vyombo vya maamuzi."
Kwake BRIC ni kama daraja kati ya nchi zilizoendelea kiviwanda na zinazoendelea ili kupata maendeleo endelevu na sera ya uchumi ya kimataifa yenye uwiano na ulinganifu isiyowaache wengine nje.









