Zinapokumbushwa kodi, TAKUKURU kuzibana

24Aug 2023
Mashaka Mgeta
TANGA
Nipashe
Zinapokumbushwa kodi, TAKUKURU kuzibana

MIONGONI mwa azma ya kuwapo mashirika au asasi zisizo za kiserikali (AZAKI) nchini ni kusaidia kufikisha huduma za kijamii kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono mipango na jitihada zinazofanywa na serikali kwenye maeneo hayo, hivyo kuchagiza kasi ya maendeleo na ustawi wa watu.

 

Tofauti na mipango ya maendeleo inayotekelezwa na serikali kwa kutumia kiasi kikubwa cha fedha zinazotokana na kodi za wananchi mashirika hayo yanategemea zaidi ufadhili wa ruzuku kutoka kwa taasisi mbalimbali za kikanda na kimataifa.

Hali hiyo, inaibua changamoto ikiwamo ya taasisi hizo kukosa nguvu za kiuchumi katika kubuni, kupanga na kutekeleza miradi inayokidhi mahitaji yaliyopo, badala yake kutegemea maeneo mahususi yanayotangaziwa ruzuku na wafadhili.

 

Kwa hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba, anasema zipo hatua nyingi zinazopaswa kuchukuliwa na AZAKI, ili kuondokana ama kupunguza utegemezi wa ruzuku za wafadhili katika uendeshaji wa taasisi hizo.

Kindamba anatoa rai hiyo wakati akifungua mkutano wa mwaka wa jukwaa la AZAKI wenye kaulimbiu ya Mashirika yetu, Maadili yetu, Tanga yetu unaofanyika mkoani hapa.

 

Anasema zina mchango unaotambuliwa kwa mujibu wa sheria na kanuni, hivyo kuwa na uhalali wa kutoa huduma kutokana na uchache wa rasilimali uliopo kwenye jamii.

 

Akizungumzia utegemezi uliopo sasa kwa AZAKI nyingi, anasema unachangia kuzifungamanisha na malengo ya wanaowapatia fedha za kutekeleza miradi wanayoitangaza, hata pale miongoni mwao inapokiuka misingi ya mila na desturi zilizopo.

 

Kwa mujibu wa Kindamba, wigo wa ukiukwaji wa maadili umefikia hatua kwa baadhi ya AZAKI kujiingiza kwenye kashfa za kuunga mkono, kutangaza na kushiriki vitendo viovu kama vile ushoga, ulawiti, usagaji, kuingilia kinyume cha maumbile na matumizi ya dawa za kulevya.

 ‘’Tunapitia changamoto kubwa ya mmomonyoko wa maadili kwenye jamii yetu, zipo AZAKI zinazotajwa kujihusisha na vitendo hivyo ambavyo kimsingi, ni mambo ambayo hata ibilisi hakuyafanya,’’ anasema.

 

Kindamba anasema, hivi sasa jamii imeathirika kwa kiwango kikubwa kutokana na kukithiri kwa mmomonyoko wa maadili unaohusisha vitendo viovu kama vile ushoga, ulawiti na usagaji.

FEDHA CHAFU

Anaziasa zisitumike kutakatisha fedha chafu, akizionya kuwa wakati ambapo zipo katika hali duni kiuchumi na hivyo kuendelea kuwategemea wafadhili, ziepuke kutumika kama ‘mirija’ ya kutakatisha fedha haramu, zinazotoka kwenye mitandao ikiwemo ya ugaidi na biashara haramu za usafirishaji wa binadamu na dawa za kulevya.

 

Mkuu wa Mkoa anaziasa kuwa na mipango yenye kuwaimarisha katika nyanja za fedha na rasilimali watu hususani wataalamu, badala ya kuwa tegemezi kwa wafadhali, wakiwamo wanaowalazimisha kujihusisha na vinavyokiuka maadili kama masharti ya kupata misaada.

Anaonya, ‘’wakati wa uongozi wangu hapa Tanga, tutakuwa wakali sana. Hatutakuwa na simile dhidi ya vitendo vya mmomonyoko wa maadili na biashara haramu za kutakatisha fedha, kusafirisha binadamu na dawa za kulevya.’’

WASHIRIKA SERIKALI

Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa AZAKI nchini, Mwantumu Mahiza, anasema taasisi hizo zinapaswa kufuata sheria, kanuni na taratibu ili kujiimarisha zaidi na kuepuka kufutiwa usajili.

 

Aidha, miongoni mwa matakwa ya kisheria ni kulipa kodi zinazotambulika na mamlaka za serikali hususani ofisi za Wakuu wa Wilaya wanapotekeleza miradi yao.

 

‘’Kila DC anapaswa kuyatambua mashirika yanayofanya kazi wilayani kwake na jamii iyajue mambo yanayofanywa kwenye maeneo yao, hivyo hakikisheni mnashirikiana na serikali ipasavyo,’’ anasema.

 

TAKUKURU KUCHUNGUZA

Kuhusu kodi, anasema uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kudhibiti Rushwa (TAKUKURU) unabaini kuwapo AZAKI zinazokwepa kodi.

 

Hata hivyo, anasema mpango umeandaliwa ili kuziwezesha kujua kwa kina maeneo mahususi ambayo TAKUKURU inazichunguza  taasisi hizo, hali itakayoondoa mtazamo na hisia hasi zinazoweza kujitokeza.

 

Mwantumu anasema huduma za AZAKI zinapaswa kuelekezwa zaidi katika kero kubwa zinazowakabili wananchi kama migogoro ya ardhi na msaada wa kisheria hasa kwa watu wanaokabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.

 

Hata hivyo, Mwantumu anaonya kuwa zipo zinazotekeleza majukumu yasiyoendana na malengo yaliyoanishwa kwenye katiba zao na kuzionya kuwa jambo hilo halikubaliki,

 

Anasema serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu utendaji kazi kujiridhisha kuwa zinafuata misingi ya ukweli na uwazi.

 

Kadhalika, ufuatiliaji shughuli na uendeshaji wake ufanywe kwa njia ya mfumo, hivyo kuondoa dhana kwamba inafanywa na mtu binafsi.

 

Anaziasa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, ili kufikia malengo ya kuisaidia serikali kupata suluhu ya kero zilizopo kwenye jamii na siyo kujinufaisha binafsi.

 

Mwantumu aliyewahi kushika nyadhifa tofauti za uongozi serikalini na ubunge, anasema ili kuboresha utengamano miongoni mwa taasisi hizo, uongozi wake ulianzisha mfumo wa kuwepo majukwaa ya taasisi hizo kuanzia ngazi za chini kwenye jamii hadi kitaifa.

 

‘’Zamani majukwaa ya AZAKI yalifanyika ngazi ya kitaifa, lakini niliagiza yaanzie kwenye ngazi za chini katika jamii. Ndio maana hata leo mnaofanya kazi wilayani mnajuana, na kushirikiana kwa kina tofauti na ilivyokuwa awali,’’akasema.

 

KUWASILISHA TAARIFA

Katibu Tawala wa Mkoa, Pili Mnyema anaziagiza kuwasilisha taarifa zao serikalini ili kufanikisha azma ya utaratibu na usimamizi wa shughuli zao, kwa mujibu wa sheria.

 

‘’Hatuwezi kuwasimamia na kuwaratibu kama hatuwafahamu. Bila sisi kuwajua, itakuwa vigumu kutoa huduma mnapohitaji. Hivyo timizeni wajibu wa kisheria kuwasilisha taarifa zenu kwa ukweli na uwazi’’, anasema.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la AZAKI (NACONGO), Miraji Malinda, anasema pamoja na ufanisi wake, taasisi hizo zinakabiliwa na changamoto mbalimbali ukiwemo mtazamo hasi kwenye jamii kwamba wana fedha zinazoweza kutumika hata kinyume cha utaratibu.

 

Aidha, anasema ipo haja kwa AZAKI za kikanda na kimataifa zinazofika kwenye maeneo yao kufanya kazi, yakajitambulisha kwenye baraza katika ngazi husika, ili kuweka kumbukumbu na rekodi zinazojulikana kwa serikali na NACONGO.

PICHA
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba (kulia), akikabidhi hati kwa mshiriki wa Mkutano Mkuu wa AZAKI PICHA: EMMA KIGOMBE.

 

Mwandishi ni Ofisa Habari Mkuu Mkoa wa Tanga.

Mawasiliano: 0754 691540, email mgeta2000@yahoo.com.