Yasiyowezakana visiwani yanapoanza kushuhudiwa

23Aug 2023
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Yasiyowezakana visiwani yanapoanza kushuhudiwa
  • *Mahakama Maalumu ya Udhalilishaji yaelekea kunusuru kinamama, watoto

NI miaka mitatu sasa tangu kuanzishwa kwa Mahakama Maalumu ya Udhalilishaji Zanzibar ambapo serikali ilichukua hatua hiyo baada ya kushamiri vitendo vya unyanyasaji na kutoridhishwa na namna kesi zake zilivyoshughulikiwa.

 

 

Uamuzi huo wa serikali ulipata baraka na kuungwa mkono na wadau wa maendeleo pamoja na wanaharakati wa kutetea haki za wanawake na watoto huku wakiwa na imani kwamba ujio wake ni mwarobaini na ndiko kuvifanya vitendo hivyo historia.

Udhalilishaji wanawake na watoto ni tatizo la ukiukwaji wa haki za binadamu, licha ya juhudi zinazoendelea kuchukuliwa kupiga vita tatizo hilo, lakini limekuwa likiendelea Zanzibar na kuathiri maendeleo ya kundi hilo.

 

Kwa mujibu wa Mahakama Kuu Zanzibar, tangu kuazishwa kwa mahakama hiyo mwaka 2021/2022 kesi 122 zimeripotiwa’

za kubaka ni 72, za kulawiti 20 wakati ni mashauri 27 pekee yaliyotolewa hukumu na 25 yanaendelea kusikilizwa na kesi zilizofutwa ni 70 kwa sababu mbalimbali ikiwamo kukosekana ushahidi.

Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kesi zilizofunguliwa katika mahakama maalum ni 432, ubakaji unaongoza kwa kuwa na kesi 191, kulawiti ni 52 hizi ni kesi zinazowahusu watoto wa kiume wakati za kuingiliwa kinyume na maumbile ambazo zinawahusu wasichana ni 60, takwimu za Mahakama Kuu zinabainisha.

Mahakama Kuu inasema kati ya hizo kesi 160 zimefutwa, aidha 74 zimetolewa hukumu na kesi 198 zinaendelea kusikilizwa mahakamani hapo.

“Ilikuwa ni nadra kusikia mshtakiwa wa kesi za udhalilishaji kufungwa miaka 30 au kifungo cha maisha Zanzibar lakini hivi sasa tangu kuazishwa chombo hicho wafungwa wapo. Washtakiwa wanahukumiwa kifungo cha miaka 30 na wengine cha maisha” anasema Fatma Juma.

Fatuma mwanaharakati wa kutetea haki za wanawake na watoto, anaeleza kuwa tangu Serikali ya Zanzibar kuanzisha Mahakama Maalum ya Udhalilishaji, hukumu zinazotolewa kwa baadhi ya kesi hizo zinaridhisha ikilinganishwa na kipindi cha nyuma kabla ya kuwepo kwake.

Anasema imefanikisha kusikilizwa kwa haraka kwa kesi za udhalilishaji na hukumu za vifungo kuongezeka tofauti na hapo awali.

POLISI WAWAJIBIKA

Kuazishwa kwa mahakama hiyo kumechangia kasi ya utendaji kazi wa kushughulikia kesi hizo kwa askari na Jeshi la Polisi, anasema kamishna msaidizi wa polisi na mkuu wa madawati ya jinsia, Egyne Emmanuel.

Anasema kulikuwa na msongamano mkubwa wa kesi katika vituo vya polisi, lakini hivi sasa zinapewa kipaumbele na kuongeza uharaka wa kushughulikia makosa hayo.

Katika kuboresha kazi za dawati la jinsia kwenye vituo vya polisi, kupambana na vitendo hivyo, anasema kuna baadhi ya vitendo haviripotiwi polisi kwa sababu ya waathirika kutishwa kutokana na wadhalilishaji kuwa watu wa karibu na familia.

Kamishna Emmanuel anasema, Jeshi la Polisi limeanzisha utaratibu maalumu wa kuwapeleka polisi shuleni kutoa elimu ya usalama kwanza ili kuibua vitendo vya udhalilishaji ambavyo vimefichwa.

Anasema katika mwaka 2022 jeshi hilo limeibua kesi 57 za udhalilishaji shuleni ambazo hazikuripotiwa polisi na mchakato wa kisheria unaendelea.

“Huu ni mwanzo tu tunaamini mpango huu utasaidia kuibua kesi nyingi ambazo haziripotiwi polisi lakini mkakati mwingine ni kutoa elimu kwa jamii kwa sababu makosa mengi ya udhalilishaji ni kwa watoto kuanzia miaka 14 hadi 18,”anasema Emmanuel.

Anaongeza kuwa elimu hiyo itasaidia kuongeza kiwango cha uelewa ili jamii ielewe ni umri gani wa kushiriki tendo la ndoa badala ya kuwepo kwa kesi nyingi za watoto kujihusisha na kujamiiana wakiwa na umri mdogo.

Aidha, anasema mkakati mwingine ni kuongeza idadi ya madawati kwa sababu yaliyopo ni machache na hayapo katika kiwango bora na kwa sasa kuna idadi ya madawati matatu ambayo yamefikia kiwango cha kuwa dawati hivyo wanahitaji kuwa na madawati 57 yenye viwango.

“Ili dawati liwe na kiwango kwanza linatakiwa kuwa nje ya kituo cha polisi kuwe na vyumba maalum kwa ajili ya kumhoji mtoto, viwepo na vitendea kazi ikiwamo usafiri,”anasema

Aidha, mkakati mwingine ni kuboresha ukusanyaji wa taarifa kwa sababu utaratibu wanaotumia hivi sasa umepitwa na wakati, wawe na vifaa vya kieletroniki badala ya kusubiri kesi itokea wilayani hadi makao makuu.

“Mpango mwingine ni kuboresha usafiri kwa watendaji wetu hasa kuwa na pikipiki kwa watendaji wa dawati ili kuharakisha ufuatiliaji wa kesi ikiwemo kufanya uchunguzi wa haraka,”anasema.

KUCHUNGUZA DNA

Amina Said Abdallah, mchunguzi wa maabara katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Zanzibar, anasema kwa mwaka 2021/2022 wamepokea kesi 95 za udhalilishaji kwa ajili ya kuchunguza vinasaba (DNA).

Halikadhalika, kesi nyingi zinazofikishwa hapo baada ya kufanyiwa uchunguzi mhusika anatambulika na asilimia 80 ya washukiwa hupatikana wakati asilimia 20 ya washukiwa wanabainika kubambikizwa kesi, anasema.

Ushahidi wa vinasaba unapokuwa mahiri kazi ya uchunguzi huwa nzuri na huchukuwa muda wa wiki mbili kukamilika, anaongeza.

Aidha, anaitaka jamii kutowasafisha watoto waliofanyiwa vitendo vya udhalilishaji ili kuzuia kupoteza ushahidi na watuhumiwa kutotiwa hatiani.

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) inasema utendaji wa mahama ya udhalilishaji ni mahiri na umesaidia katika uendeshaji wa kesi hizo kwa haraka.

Huda Khamis wakili wa serikali kutoka ofisi ya DPP, anasema jalada la kesi za udhalilishaji linapofika katika ofisi ya Mkurungenzi wa Mashtaka halichukui muda mrefu kama ushahidi utajitosheleza na si zaidi ya wiki mbili kesi hushughulikiwa na kufikishwa mahakamani.

Huda anasema licha ya uwepo wa mafanikio baada ya kuanzishwa kwa mahakama hizo lakini bado jamii inamuhali na baadhi yao hukataa kufika mahakamani kutoa ushaidi.

“Bila ya ushahidi hakuna hatia wakati mwingine tunalaumu kuwa washitakiwa wanaachiwa huru lakini kwa upande mwingine kesi zinakosa ushahidi jamii bado ina muhali au kuoneana aibu kwa sababu wafanyanyaji wa vitendo hivyo ni watu wa karibu katika familia za wahanga,”anasema.

SAUTI ZA WAHANGA

Wahanga wa vitendo vya udhalilishaji wanasema bado hawaridhiki na uendeshwaji wa kesi wa mahakama ya udhalilishaji na miongoni mwa sababu wanazozitaja, ni kuchukuwa muda mrefu kutoa hukumu.

Amina Juma (sio jina halisi) mzazi wa mtoto aliyebakwa anasema washitakiwa wanadanganya mahakamani kwa kudai wana umri mdogo kuzuia haki kutendeka.

 “Mtoto wangu wa miaka 12 alifanyiwa kitendo cha udhalilishaji lakini nashangaa baada ya mtuhumiwa kufikishwa mahakamani alidanganya umri kuwa ana miaka 16 wakati taarifa zake za mwanzo za kituo cha polisi zinaeleza ana miaka 19,”anasema.

Aidha, anasema watuhumiwa wamekuwa na njama hiyo ya kujipunguzia umri kwa kisingizio cha kuitumia sheria ya mtoto ambayo inamlinda ya kutohukumiwa kifungo jela hata kama ana hatia.

 

Anasema kesi yake ilipofikishwa mahakamani hakuna shahidi aliyeitwa kwenda kutoa ushahidi na hatimaye mshitakiwa kuachiwa huru.

 

Wakizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo katika kufuatilia kesi hizo wanasema, ni kuahirishwa mara kwa mara, mahakama kutotenda haki, kutengwa na jamii, kuathirika kisaikolojia, kupata aibu hata kusemwa vibaya mitaani.

Licha ya uwepo wa changamoto hizo lakini wahanga hao, waliitaka jamii inayokumbwa na vitendo vya udhalilishaji kuacha kumaliza kesi hizo katika ngazi za familia na badala yake kuzipeleka katika vyombo vya sheria.

Aidha, wanawataka wanaosimamia haki katika kesi hizo za udhalilishaji kutenda haki kwa mujibu wa sheria.

MWISHO

 

PICHA

Wanafunzi wa shule mbalimbali za serikali wakishiriki Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu Mjini Zanzibar.