Watanzania ni takribani milioni 62 kwa mujibu wa ripoti ya sensa ya watu na makazi ikiwa ni sawa na asilimia 4.5 ya idadi ya watu barani Afrika.
Kimsingi hiyo ni nguvukazi muhimu ya kujiletea maendeleo endelevu iwapo itajengewa uwezo na ikatumika kwa umakini na nidhamu.
Katika ripoti hiyo ya sensa ya 2022, nguvukazi nchini imegawanywa katika makundi mawili. vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 35 ikiwa ni takribani milioni 21 sawa na asilimia 34.5 ya Watanzania wote na kundi la pili ni la wenye umri kati ya miaka 15 na 64.
Hawa ni watu wazima pamoja na umri zaidi ya miaka 60 mpaka 64 wakiwa ni sehemu ya wazee lakini bado wana nguvu ya kufanya kazi. Hivyo idadi yao ni takribani milioni 32 sawa na asilimia 53.4 ya Watanzania wote.
Nimekisia kuwa nguvukazi vijana ni kati ya miaka 15 na chini ya miaka 45 idadi yao ikiwa kama watu milioni 26. Waliobaki, umri chini ya miaka 15 na umri wa zaidi ya miaka 45 ni makundi ya watoto na watu wazima, wazee na vikongwe.
Kwa mantiki hiyo idadi ya vijana katika uhalisia wao, na kama nguvukazi muhimu ya taifa ni wengi na swali ni hili, nini hatima yao katika kuyatimiza malengo ya taifa ya kujiletea maendeleo endelevu?
Iwapo watu zaidi ya milioni 26 watajengewa uwezo wa kasimamiwa ipasavyo na kutumika vizuri na kwa nidhamu kubwa, hakuna shaka taifa litajiletea maendeleo endelevu kupitia sekta mbalimbali ikiwamo kilimo, ufugaji, misitu na nyuki, uvuvi na shughuli kadhaa za utalii, biashara na ujasiriamali.
Kikubwa cha kukisimamia ni hiki kama taifa linaloendelea je, tunatumiaje vijana waliopo ili kuyafanikisha malengo hayo?
Tunaposema nguvukazi ni muunganiko wa maneno mawili nguvu ambao ni uwezo wa kufanya jambo au kitu fulani au kuwa na madaraka kisiasa na kiutawala. Kwa neno kazi linamaanisha utumiaji wa nguvu au nishati ama juhudi, maarifa katika kufanikisha kitu au jambo fulani.
Kwa msingi wa maelezo hayo, taifa linalo uwezo wa kufanya au kutekeleza shughuli zake bila vikwazo vingi kwa mantiki kwamba wapo wa kutosha kuendesha mambo yake kwa lengo la kujitegemea zaidi na kujiletea maendeleo endelevu.
Ndiyo maana baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliweka bayana kuwa ili taifa lijiletee maendeleo linahitaji vitu vya msingi vinne, watu wa kutosha wenye nguvu za kufanya kazi, ardhi, siasa safi na uongozi bora
Suala la vijana nguvukazi ya taifa linahitaji kufanyiwa mikakati ili nchi inufaike nayo na kwanza kuelewa kuwa Tanzania ni taifa linaloinukia kiuchumi na shughuli zake nyingi bado zimeegemea kwenye kilimo, ufugaji, uvuvi, misitu na nyuki na biashara kama usafirishaji na mawasiliano (TEHAMA),
Aidha, kwenye uhifadhi, uendelezaji na usimamizi au utumiaji endelevu wa maliasili zetu na utalii. Maeneo hayo yote yanahusu kufanya kazi kwa kutumia watu ambao ni vijana wengi tulio nao hapa nchini.
Pili, tunahitaji mikakati shirikishi ya kitaifa ili kuhakikisha vijana hao wanaume kwa wanawake, wanatumika ipasavyo, bila ya kutegemea sana misaada kutoka mataifa mengine.
Miaka iliyopita serikali iliweka mkazo kwenye masuala ya kilimo. Tulikuwa na kaulimbiu zilizolenga kuhamasisha na kuboresha shughuli za kilimo. Mathalani, ‘siasa ni kilimo, kilimo cha kufa na kupona, kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi’.
Pamoja na hayo yote, kiuhalisia utekelezaji haukuendana na mitazamo hiyo. Hivyo, masuala ya kilimo hayakupewa kipaumbele na msukumo halisi kama ilivyotarajiwa.
Kwa mfano, shughuli za ugani zikawa zinasuasua na upatikanaji wa vifaa kazi kama matrekta au majembe ya kukokotwa na wanyama na pembejeo zikiwamo mbegu bora, viwatilifu, huduma za kusindika mazao na masoko, ikawa changamoto zaidi.
Hali kama hiyo iliwakumba pia wavuvi, wafugaji na wakulima wa mazao ya misitu/ufugaji nyuki.
Pamoja na ukweli kwamba, kwa miaka mingi tulikosea, serikali iliyopo madarakani inastahili pongezi kwa kuziona changamoto za nguvukazi ya vijana.
Aidha, imeongeza bajeti ya kilimo kwa nia njema ya kuziwezesha shughuli za kilimo kuwa zenye manufaa makubwa kwa Watanzania na zaidi vijana wenye utayari wa kutaka kujiendeleza kiuchumi na kwa manufaa ya taifa.
Iwapo umuhimu wa kilimo, ufugaji na uvuvi katika kufanikisha lengo la kujiletea maendeleo endelevu utazingatiwa na fedha zilizotengwa takribani trilioni moja katika mwaka wa fedha 2023/2024 na kuelekezwa kwenye sekta ya kilimo; zitapatikana kwa wakati muafaka na kusimamiwa tena kutumika kwa malengo yaliyowekwa na kwa umakini mkubwa hatimaye kuwasaidia vijana wengi kumudu changamoto za kimaisha litakuwa jambo jema.
Pamoja na kuongeza bajeti kubwa ni kuhakikisha kuwepo na mikakati mahususi ili kiasi kilichotengwa kitumike kuboresha uzalishaji wa mali na mazao kupitia rasilimali ardhi hususani huko wilayani na vijijini kwa kutumia sehemu ndogo ya ardhi na kupata mazao mengi kwa ekari au hekta moja.
Iwapo kutatokea changamoto, jitihada zifanyike haraka kuzitafutia ufumbuzi kupitia wataalam na washauri na vyombo vingine kama vyama vya ushirika na serikali za mitaa katika halmashauri zinazohusika.
Kwa sasa changamoto kubwa kwa vijana ni wengi kutoka vijijini na kuhamia mijini na kwenye majiji kama Dar-es-Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha na Mbeya. Hali hii huhamisha nguvu kazi hiyo kutoka vijijini kwa lengo la ‘kutafuta maisha’ bora zaidi kwenye miji, manispaa na majiji.
Hali hiyo, inaonyesha kuwa kuna mtazamo kwamba kwenye miji na majiji kuna uwezekano wa kupata fedha za harakaharaka bila kujali mazingira watakayokumbana nayo.
Mtazamo kama huo siyo dalili njema kwa mustakabali wa taifa na watu wake kujiletea maendeleo.
Kwa miaka miwili iliyopita kasi ya vijana kujipatia fedha za haraka au chapuchapu imeongezeka sana na sasa sehemu kubwa wamejiingiza kwenye michezo ya kupata fedha kupitia kubet, wakibashiri timu za mipira zitakazo shinda mechi mbalimbali kwa kuziwekea matokeo.
Mathalani, kubashiri timu gani itashinda, idadi ya magoli, muda yatakayofungwa na wafungaji kadhalika ipo michezo mingine mingi kupitia mitandao na vyombo mbalimbali vinavyohimiza Watanzania kucheza ili kujipatia fedha kirahisi.
Haya yote yanafanyika kwa misingi ya kamari na vijana wengi wamevutwa na hali hiyo mambo hayo yanayoongeza tafakauri na kuandaa mbinu bora za kusaidia nguvu kazi hiyo iwe na tija kwa taifa.









