Mkoani Shinyanga kukosekana elimu na ufahamu sahihi wa kunyonyesha kwa wanawake kunaelezwa kuwa kunachangia kwa kiasi kikubwa tatizo la udumavu kwa watoto, anasema Ofisa Lishe wa Mkoa Yusuph Hamisi,.
Baadhi ya wanawake mkoani Shinyanga bado hawana elimu hiyo ya unyonyeshaji na kusababisha tatizo la udumavu unaotokana na unyonyeshaji duni kwa watoto kuendelea, anaongeza na kukiri kuwa kinamama bado hawana elimu sahihi, anasema katika mahojiano na Nipashe, kuhusu changamoto na mafanikio ya Wiki ya Uhamasishaji mkoani humo.
Kwa mujibu wa utafiti wa taifa wa masuala ya afya na lishe ya mwaka 2022, tatizo la udumavu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano Shinyanga unatajwa kuwa na asilimia 27.5 ambazo zinamaanisha kuwa watoto takribani 28 kwa kila watoto 100 wameathirika na udumavu huo, wakati ukondefu mkoa unafikia asilimia 4.3.
Hamisi, anakiri kwamba kinamama katika mkoa huo wanahitaji elimu kwani bado hawana ufahamu sahihi wa unonyeshaji watoto, na kwamba asilimia 30 pekee ndiyo hunyonyesha watoto wao ndani ya saa moja mara baada ya kujifungua kwa wale wanaojifungulia hospitalini.
Anasema maziwa ya mama kwa mtoto ni muhimu kujenga mustakabali wa afya yake ikiwamo ukuaji kimwili, kiakili, na hata kupunguza tatizo la udumavu ambalo huathiri mwili akili na maisha ya watu.
“Mtoto akizaliwa baada ya saa moja, anapaswa kunyonyeshwa yale maziwa ya kwanza ya njano na siyo kuyakamua na kuyamwaga. Ni kwa sababu yana virutubisho na ni kinga ya mwili ya mtoto na hayana madhara,”anasema Hamisi.
Kadhalika anaeleza kuwa wanawake wengi wasio na ufahamu hawapendi kuwanyonyesha watoto wao maziwa hayo ya njano wakidhani ni machafu na kuwanyima watoto kinga ya asili.
Anasema mtoto akishazaliwa licha ya kunyonya maziwa hayo ya njano pia anapaswa kutolishwa chochote mbali na maziwa ya mama ndani ya miezi sita bila ya kupewa kitu chochote wala maji, ushauri ambao umekuwa ukipuuzwa na wanawake wengi na hata kuwasababishia maradhi mbalimbali.
“Mtoto akishafikisha miezi sita ndipo anapaswa kuanza kupewa vyakula vya ziada kwa kuzingatia lishe bora kwa kufuata makundi matano ya chakula, huku pia akiendelea kunyonyeshwa maziwa ya mama hadi akifikishe miaka miwili hapo lazima awe na afya njema,”anafanua Hamis.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme, anawashauri wanawake popote nchini kuhudhuria kliniki na kujifungulia katika vituo vya huduma za kiafya ili kwanza kujiepusha na hatari zinazoweza kuwapata na watoto wao pia, lakini pia kujifunza elimu ya afya ya uzazi salama, lishe na unyonyeshaji sahihi watoto.
Anasema, tatizo la udumavu kuendelea ni ukosefu wa elimu kwa wazazi, na kutoa maagizo kwa maofisa lishe na wataalamu wa afya, wafanye mikutano ya mara kwa mara na kuelimisha unyonyeshaji na lishe bora hasa maeneo ya vijijini.
“Naelekeza maofisa lishe wote mkoani hapa wasikae ofisini bali waende kutoa elimu ya lishe na uyonyeshaji kwa wananchi, sababu bila kuwapa mafunzo tatizo hili la udumavu kwa watoto linalotokana na kutonyonyeshwa ipasavyo litaendelea kuwepo hapa Shinyanga,” anaonya Christina.
Mkuu wa mkoa anatoa maagizo pia kuwa fedha za lishe ziendelee kutolewa kulingana na mpango kazi uliopo ili kutoathiri utekelezaji wa shughuli zake pamoja na kufanya maadhimisho ya siku ya afya na lishe kila robo mwaka kwa mujibu wa muongozo uliopo ili kufikisha elimu ya unyonyeshaji kwa jamii.
Kadhalika, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile, anasema tatizo la udumavu kwa watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka mitano mkoani hapo limepungua kutoka asilimia 32.1 mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 27.5 mwaka jana.
Anaeleza kuwa udumavu huo umepungua kutokana na elimu ya unyonyeshaji na lishe bora ambayo imekuwa ikitolewa kwa wazazi kupitia huduma za kiafya, na kueleza kwamba bado elimu zaidi ina hitajika kutolewa hasa maeneo ya vijijini.
Mwanamama Careen Jamson, anasema alishapata elimu ya unyonyeshaji katika kituo cha afya Kambarage Manispaa ya Shinyanga, na mtoto wake ambaye kwa sasa ametimiza miezi sita, hakuwahi kumpatia kitu chochote zaidi ya maziwa yake.
Anasema awali hakuwa na elimu hiyo ya unyonyeshaji, lakini sasa hivi elimu anayo na mtoto wake ana afya njema na anaamini hilo limesaidia kumwepusha na maradhi ya mara kwa mara sababu ana kinga ya maziwa ya mama.
Khadija Shabani, anasema baadhi ya wanawake hawataki kunyonyesha watoto wao kwa madai ya kulinda muonekano wa matiti yao wakiamini eti yatapoteza muonekano mzuri.
Anasema elimu bado inahitajika kwa jamii kuhusu faida ya unyonyeshaji watoto ili kuondoa udumavu kwa watoto wao.









