Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania Azam Mashangu alisema zaidi ya warembo 20 kutoka mikoa mbalimbali wanaingia kambini leo na watakuwa huko kwa siku 15 kabla ya mashindano hayo kufanyika.
Wakati mashindano hayo ya kila mwaka yakifanyika, hayakupitia njia rahisi kama wengi wanavyodhani. Ni moja kati ya mashindano yaliyopita kwenye njia ngumu hadi kukubalika.
Si kwa wazazi tu kuruhusu mabinti zao, bali hata jamii nayo iliyaona ni ya kimagharibi zaidi na yamekuja kuharibu mila na desturi si za Kitanzania tu, bali za Kiafrika.
Historia ya ulimbwende Tanzania inaonyesha kuwa Miss wa kwanza kabisa ni Theresia Shayo. Huyu ndiye ameweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Miss Tanzania tangu nchi ijipatie Uhuru mwaka 1961.
Aliutwaa umalkia huo mwaka 1967, mashindano yakifanyika kwenye Hoteli ya Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo baada ya mashindano hayo, serikali ya awamu ya kwanza ikayapiga marufuku kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kulinda maadili na utamaduni wa Mtanzania.
Theresia, baada ya kuwa Mbongo wa kwanza kuvalishwa taji la Miss Tanzania, alibahatika kuolewa na Mjerumani aliyeitwa Chrstian Rieger na kwenda kuishi nchini Ujerumani.
Hata hivyo waliachana miaka mingi baadaye na alibaki nchini humo akiwa na mpenzi wake Tonny.
Alikuwa na nyumba yake mtaa wa Schmiedberg namba tisa katikati ya mji wa Augsburg, hadi alipofariki dunia Januari 26 mwaka 2007 kwa kile kilichoelezwa ni kansa ya tumbo akiwa na umri wa miaka 61.
Serikali ya awamu ya pili iliyaruhsu mashindano hayo kuendelea tena na ilisukumwa na utandawazi ambao ulikuwa ukishika kasi kila kukicha.
Mrembo aliyeweka rekodi ya kuwa wa pili kutwaa Umiss Tanzania ni Aina Maeda. Huyu pia ameandika rekodi ya kuwa Mbongo wa kwanza kutwaa taji hilo liliporuhusiwa tena baada ya miaka 27. Ilikuwa ni mwaka 1994 yalipofanyika mashindano ya pili ya urembo nchini, lakini yakiwa ya kwanza baada ya kuruhusiwa tena.

Mwaka uliofuata lilitaka kujitokea kama lile la mwaka 1967, lakini busara ilitumika kwa viongozi, lakini baada ya hapo kulitokea miongozo ambayo inaendelea kutumika hadi leo.
Hii ilitokana na mshindi wa mwaka 1995 ambaye hakuwa mwingine ila ni mrembo Emily Adolf.
Pamoja na furaha ya kutwaa taji hilo, lakini ilitokea kasheshe kwani alikuwa ni Mwafunzi wa Kidato cha Pili shule ya Sekondari Central, Dodoma.
Uongozi wa shule haukufurahia mwanafunzi wake kuingizwa kwenye kinyang'anyiro hicho.
Ushindi wake ulileta malumbano makali pia kwa taasisi mbalimbali kupinga vikali kushirikisha wanafunzi wa shule za sekondari kwenye mashindano hayo ya urembo.
Pia wanaharakati wakapinga warembo kupitishwa majukwaani wakiwa wamevalia nguo fupi.
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) wakati huo ilibidi kuingilia kati kuweka kanuni na taratibu za kuendesha mashindano hayo na wakapiga marufuku wanafunzi wote wa Shule za Msingi na Sekondari kutoshiriki mashindano hayo.

Ndiyo mana hadi leo wanaoruhusiwa kushiriki ni kuanzia ngazi ya vyuo na kwenda juu, au wasichana kutoka mitaani, makazini na hata wafanyabiashara.
BASATA pia ikapiga marufuku warembo kupita jukwaani wakiwa wamevaa nguo fupi maarufu kama vimini. Ikumbukwe wakati huo warembo walikuwa wanapita wamevaa vimini, ikiwemo nguo za ufukweni.
Hii ndiyo sababu hadi leo Mashindano ya Urembo Tanzania huwezi kuona warembo wamevaa hivyo, au kuna wanafunzi wa msingi na sekondari. Ni kutokana na sakata hilo.
Baada ya hapo mambo yalionekana kukaa sawa na mashindano yakawa yanaendelea bila shida yoyote na kuendelea kuwatoa walimbwende ambao hadi leo wameendelea kuwa maarufu.
Shose Sinare aliutwaa umalkia mwaka 1996, kabla ya Saida Kessy kuchukua nafasi yake 1997, na 1998, Tanzania ilimpata malkia wake aliyeitwa Basila Mwanukuzi kutoka Kinondoni, Dar es Salaam.
I999, Dar es Salaam iliweza kutetea taji lake, lakini safari hii ilikuwa kwa mrembo aliyetokea Ilala, Hoyce Temu.
Anajulikana zaidi kama Mrembo wa Karne, au Mrembo wa Millenium, hasa ushindi wake ulikuja wakati dunia ikitoka karne ya 20 na kuingia karne ya 21, Millenium.

Ni mrembo aliyeiletea sifa sana Kamati ya Miss Tanzania na nchi kwa ujumla kwa kufanya kazi nyingi za jamii hata alipomaliza muda wake wa mwaka mmoja aliendelea kufanya kazi za kijamii akitumia jina la Miss Tanzania 1999.
Wakaja pia kina Happiness Magese 2001, Angela Damasi 2002, Slyvia Bahame 2003, Faraja Kotta 2004, na Nancy Sumari 2005, ambaye alifika ngazi ya juu kwenye mashindano ya ubingwa wa dunia, akifika kwenye sita bora, kabla ya Tanzania kumpata mlimbwende maarufu sana, Wema Sepetu mwaka 2006, ambaye baadaye akaja kuwa mchezaji filamu maarufu nchini.









