Ukienda katika sherehe za harusi, wakati wazazi wa maharusi wanatoa nasaha kwa vijana wao, binti huwa anaambiwa na wazazi wake;
Binti yangu, ninakutakia maisha mema katika ndoa yako. Mpende mumeo na elewa kwamba wazazi wake ni wazazi wako pia, uwaheshimu, uwapende na kuwatii…”
Yapo mambo mengi huwatamkia kwa lengo la kuimarisha ndoa yao. Lakini kinachotokea baadaye ni tofauti na maagizo hayo, hivyo kuleta mtikisiko mkubwa katika ndoa nyingi.
Kama nilivyoeleza wiki iliyopita, wanawake wengi wanashindwa kuishi katika ndoa zao kwa sababu ya kutoishi kwa akili na wakwe.
Kwa mfano, wanasahau kuwa mama mkwe hana tofauti na mama yake mzazi. Lakini anamfanyia mzaha na dharau, jambo ambalo huamsha hasira na kuamua kile anachoweza kufanya.
Leo msomaji wangu nikupitishe katika baadhi ya sababu zinazomsukuma mama mkwe kukuchukia. Wivu ni moja ya sababu. Fahamu kuwa baadhi ya mama wakwe hawafurahii kile ambacho wake wa vijana wao wanafurahia.
Hii inaweza kuwafanya baadhi waone wivu na matokeo yake wanajenga chuki baina yao na wake za watoto wao. Hofu ni sababu nyingine. Baadhi ya mama wakwe wanahofu kuwa wake wa watoto wao wanaweza kubadilisha mawazo ya kijana wao wa kiume ili wasiendelee kuwahudumia kama zamani.
Hofu hii niliitolea mfano wiki iliyopita kwa wale wanaochukia waume zao wasihudumie tena familia zao. Eti mumuwe asitoe tena matumizi kwa wazazi au asisomeshe ndugu. Hivyo, hufanya juu chini kuhakikisha watoto wao hawawapi wake zao upendo halisi.
Tabia yako ni sababu nyingine. Kama nilivyotangulia kusema kuwa baadhi ya wake wana tabia zinazoweza kuwasukuma wakwe kuwachukia. Baadhi ya wake ni wachafu, wagomvi, wakorofi, wana wivu uliopitiliza na wengine siyo waaminifu katika ndoa zao.
Kama tabia yako ni mbaya, usitarajie kupendwa na mama mkwe wako! Hata kama mama mkwe wako hajasoma hupaswi kumdhihaki na kumdharau. Anapaswa kuheshimiwa na kama humpendi, mtoto wake naye hatokupenda.
Na kama siyo mwaminifu katika ndoa yako, unaweza kumwona kama ni “muuaji” maana atakuchukia sana kwa sababu anamlinda mtoto wake!
Sababu nyingine ni utasa. Kama ndoa haina watoto, mara nyingi ni rahisi sana kulaumiwa. Wanaweza kuanza kusema, “huyu mwanamke ni jangwa”. Hakuna mtu anaweza kumlaumu mwanamume. Utasa ni moja ya sababu inayowafanya wakwe wengi wawachukie wake wa wana wao.
Ujinga ni sababu nyingine. Wakwe wengi hawajatambua nafasi yao. Huamini nyumba ya watoto wao ni yao na kwamba wao ni wamiliki wa mali za watoto wao.
Hii mara nyingi husababisha migongano kati ya wakwe na wake wa wana wao, walio warithi halali wa mali za waume zao. Pia wazazi wa kale (wa kizamani) hawaelewi aina ya uhusiano unaofanya kazi siku hizi kati ya mke na mume!
Sababu nyingine ni upendo uliopitiliza juu ya watoto wao wa kiume. Mama wakwe wengine wapo karibu sana na watoto wao wa kiume. Hivyo, inakuwa ngumu kuvunja uhusiano wao pale watoto wao wanapoamua kuoa. Wakwe huanza kuona mke kama ni tishio!
Pia mama mkwe anaweza kukuchukia kwa sababu haukuwa chaguo lake kwa mtoto wake kuoa. Anaweza kukuchukia kwa sababu ya kabila lako kuwa tofauti na la kwao. Hata kama anakuchukiaje, unapaswa kuwa na hekima jinsi ya kuchukuliana naye.
Hii ya kabila tofauti katika ndoa zingine imesababisha mitikisiko mingi hata wengine kufikia hatua ya kuachana kabisa kwa talaka mahakamani. Ipo familia moja ndoa ilishavunjika kufuatia mikwara mingi.
Wazazi wa kijana hawakutaka mke amemzidi elimu kijana wao, wala awe na kazi nzuri. Ni familia iliyokuwa inataka mwanamke awe tu mama wa nyumbani kuhudumia watoto na wao wakwe.
Hata pale mke alipopambana kwa msaada wa wazazi wake na kupata digrii, bado hakuruhusiwa kufanya kazi. Mwanaume akawa anampiga mara kwa mara. Mke akakimbia, mume akadai talaka, ndoa ikavunjika.
Wiki ijayo tutaangalia namna kumfanya mama mkwe akufurahie. Ujumbe 0715268581.









