Msingi wake ni mradi mahususi wa kuwawezesha watoto wanaotoka katika mazingira magumu kwenye maeneo tofauti nchini, kwa kuwafadhili kimasomo na kuwapa usimamizi wa kile wakipendacho hadi kuyafikia malengo yao.
Katika kutimiza azma hiyo, wanafunzi waliofadhiliwa na mradi huo, hasa wanaopenda fani ya udaktari, waliwapeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, lengo ni kuwakutanisha na madaktari bingwa wajifunze na kuhoji siri ya mafanikio yao.
Ni aina ya kujifunza kama iliyotumiwa na mwanazuoni, Jerome Bruner, kwamba kuna njia ya kujifunza kwa vitendo na ndio ilitumiwa na wanafunzi, kuwandaa katika njia ya vitendo kuelewa safari yao.
Baada ya kuwasili hospitalini hapo, geni wa wanafunzi hao wakiwa na jopo linaloongozwa na Mkurugenzi wa Shivuta, Andrew Koti, hapo wakapokewa kwa bashasha na vigelegele kutoka kwa madaktari bingwa hospitalini hapo huku vichwani mwao wakifahamu ndio warithi wa baadaye, wakionyesha kuwapenda na kuwapa ushirikiano.
Hapo wakapewa chumba maalumu na punde kidogo akaletwa daktari bingwa wa masuala ya uzazi na mara moja, wanafunzi waliokuwa na bashasha ya kuuliza maswali ya wanachokitamani kuhusu masuala ya afya ya uzazi na uuguzi, wakaanza kuhoji maswali.
Ni mjadala wa majibu na maswali, uliochukua zaidi ya saa nne, wakipewa majibu ya papo kwa hapo na daktari mhusika, ikiwa ni pamoja na kupata simulizi ya maisha aliyopitia daktari huyo mpaka akafanikiwa.
Kimsingi, ni hadhira iliyowavutia wanafunzi hao na hata wakatamani moja kwa moja kusoma kwa bidii, ili kufikia malengo ya kuwa madaktari bingwa, kama ilivyokuwa kwa daktari huyo.
Nipashe iliyokuwa bega kwa bega kwenye tukio hilo, ikashuhudia wanafunzi hao wakifundwa kusoma kwa bidii na kuepuka vishawishi, ikiwamo mimba za utotoni na kuolewa wakiwa na umri mdogo na kwamba wanapaswa kutambua, dunia ya sasa inataka mtoto asome kwa nadharia na vitendo kwa kile anachokipenda.
Mwanafunzi wa Darasa la Sita, ambaye ni miongoni mwa waliohudhuria ziara hiyo mwenye ndoto ya kuwa Daktari Bingwa wa Uzazi, Sonia Chilani, anasema jambo hilo limewatoa tongotongo na kwamba sasa wanapaswa kusoma kwa bidiii ili kufikia hatua hiyo.
Anashauri serikali kuweka mkakati wa kuwapeleka wanafunzi hata walioko ngazi za chini kwenye taasisi ambazo wanatamani kusomea.
“Nimewaona madaktari wa kike zamani nilikuwa ninajua madaktari ni wa kiume tu, hili ziara imeniongezea hali ya kujituma na nitapambana na nitasoma kwa bidii mpaka nije kuwa daktari bingwa” anasema mwanafunzi huyo, kutoka Shule ya Msingi Serengeti ya Dar es Salaam.
MALEZI WAO
Mlezi wa watoto hao kundi la Binti Kinara, ambaye pia ni Mshindi wa Miss Tanzania, Juliana Lugumisa, anasema limekuwa jambo kubwa kwao, kwa kuwa watoto hao wamepokewa vizuri na wamezungushwa maeneo tofauti katika hosipitali hiyo, ili kuyana yote.
Anaeleza imani yake kwamba, jambo hilo litakuwa chachu kwao kujituma kufanya kazi kwa bidii, ili waweze kufikia malengo ya kuwa madaktari bingwa nchini.
“Wenzetu wazungu wana utamaduni wa kumpeleka mtoto kwenye shule ambayo kuna fani anayotaka kusomea na sisi tumeona tuige mfano huo tumewaleta hapa (MNH) Upanga, wamekutana na
madaktari bingwa wameuliza maswali mengi na wamehamasika.
“Tuna imani watasoma kwa bidii, ili wafikie ndoto hiyo, tumetembelea majengo ya dharura, moyo, afya ya uzazi, hii itasaidia mtoto kupata morali ya kusoma kwa bidii,” anasema Juliana.
Anaendelea kubainisha watoto hao walichokiokota akitamka: “Sio kila mwanamke ni nesi, wengine ni madaktari. Kwa hiyo, wamefuta ile dhana kuwa mwanamume ni daktati na mwanamke nesi, kwa sasa wanaelewa kuwa hata mwanamke anaweza kuwa daktari”
Mratibu wa Shivuta, Paulo Chegere anasema mbali na kufadhili wanafunzi wanatoka kwenye maisha magumu pia wanasimamia na kuhamasisha vikundi vya kuweka fedha na kukopa, kutoa elimu ya fikra chanya kitaalamu, hapo anafafanua kuwa walicholengea ni kuwapa watu uwezo wa kujitegemea na kuitumia akili vizuri kutatua changamoto zinazo wakabili.
Anaendela kuwa, jambo jingine wanalolifanya ni kusaidia watu wenye uhitaji maalumu na kuwapa nafasi ya kufikia malengo yao licha ya ulemavu walionao.
“Kazi ya mradi wa binti kinara ni kumuibua mtoto wa kike anayefanya vizuri kwenye masomo, ili aje kutimiza ndoto zake na kuwasaidia wengine. “Tumewaleta hapa hospitalini kwa sababu kuna, madaktari bingwa wengi na wataalamu kwa hiyo tunaamini ziara hii itawafanya watoto wasome kwa bidii na kutimiza malengo,”anasema Chegere.
MKUU WA UKUNGA
Mkuu wa Idara ya Ukunga na Afya ya Uzazi Hospitali ya Muhimbli, Priscilah Kinyamagoha, anayeonyesha kufurahisha na ujio wageni hao ofisini kwake, anasifu jambo hilo kwao imekuwa fursa na furaha kubwa na kwamba, ni hali itakayowajenga na kuwapa morali wanafunzi, wasome kwa bidii zaidi.
Anasema ni jambo linalopaswa kuigwa na shule nyingine, ili watoto wanaotamani kuwa madaktari waweze kufanya maamuzi sahihi wangali wadogo.
“Hii ni chachu kwa wanafunzi wengine na serikali kwa ujumla, waweze kuwapeleka wanafunzi kwenye maeneo ambayo watoto wanatamani kuwa.
“Kujionea kama ni jeshini, wapelekwe kwenye kambi za jeshi, kama ni urubani wapelekwe kwenye viwanja vya ndege, kama ni hospitali waletwe ili wajifunze na waone namna kazi wanayotamani kuwa inavyofanyika,” anashauri mtaalamu huyo.









