Nishati safi jikoni kwa kila Mtanzania inawezekana,

21Jun 2023
Restuta Damian
DAR ES SALAAM
Nipashe
Nishati safi jikoni kwa kila Mtanzania inawezekana,
  • Umoja wa Ulaya wajitosa *Kitakachotumika kupikia gesi, bioethanol, mkaa wa mimea

MOJA kati ya malengo endelevu ya dunia (SDGs) ni kuona kuwa ifikapo 2033, karibu kaya zote zitumie nishati safi na salama kupikia.

 

 

Malengo yanataka itakapofika mwaka huo, asilimia 80 ya kaya zote jiko lake liwe linatumia maijiko banifu ya kuni au mkaa kupika kwa ufanisi au kimiminika kinachowaka cha bioethanol kinachozalishwa kutokana na mimea yenye sukari nyingi ikiwamo miwa.

Majiko mengine yanayolengwa ni yale yanayotumia gesi ya kwenye mitungi LPG na hata umeme lakini kiasi kidogo, tena yakiivisha vyakula kwa ufanisi.

Ni kazi inayofanikishwa na mageuzi ya kiteknolojia ya uvumbuzi wa majiko yanayotumia nishati kidogo kupikia na kuhakikisha upatikanaji wake kwa wananchi ni wa gharama nafuu ili watu wa hali zote mijini na vijijini wamudu.

Katika kufikia azma hiyo Ofisi ya Umoja wa Ulaya (EU), nchini imetenga Euro milioni 17, takribani Shilingi bilioni 47.6, kuzisaidia kampuni zinazojishughulisha na uzalishaji na usambazaji wa nishati pamoja na majiko hayo ya kisasa, ili kufikia azma ya dunia ya kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira, unaotokana na nishati chafu.

Mtaalamu wa masuala ya Fedha wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji ya Maendeleo (UNCDF), linalosimamia utekelezaji wa Mradi wa Cookfund, Imanuel Muro, anasema mageuzi ya kiteknolojia ni muhimu ili kupunguza matumizi ya nishati zote za kupikia.

Anasema kupunguza matumizi kutawezekana kwa kuruhusu uvumbuzi wa majiko yanayotumia kiasi kidogo cha nishati, bila kuathiri upishi ili kaya nyingi zione umuhimu wa kutumia teknolojia mpya.

Muro ambaye ni meneja mradi wa Cookfund, anasema mageuzi ya kiteknolojia yaliyoleta majiko banifu ya mkaa na kuni, ya gesi yanayotumia gesi kidogo, bioethanol na ya umeme yanayotumia umeme kidogo, yameshafanyika.

Anasema katika hilo, kuna mkaa na kuni rafiki wa mazingira (green charcoal), ambao unatokana na mimea ikiwamo miti inayoweza kukuzwa kwa kipindi kifupi, ambao ukipatikana kwa wingi utapunguza ukataji wa miti ya asili kutengeneza mkaa na kuni.

Anasema uvumbuzi mwingine umeleta majiko yanayotumia kuni na mkaa kidogo: “Unaweza kuona kwamba pamoja na kuwa na mkaa rafiki wa mazingira, teknolojia imetuletea majiko yanayotumia nishati hii kwa kiasi kidogo sana. Majiko haya yanapunguza matumizi ya mkaa kwa asilimia 60 na yamethibitishwa,” anasema Muro.

Aidha, anataja jiko linalotumia gesi kidogo, umeme, bioethanol na gesi kidogo ambayo yakipatikana kwa wingi yatafanikisha kukabili athari za uharibifu wa misitu kwa kukata kuni na mkaa.

“Tunachopaswa kufanya ni kubadilisha mitazamo yetu na kutumia nishati hizi rafiki, ili tuweze kuokoa mazingira yetu na hili ndilo suluhisho,” anasema.

Ili kuweza kubadili mtazamo, UNCDF imezindua kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ya ‘Anzia Jikoni-mabadiliko ya hewa safi ya baadaye yanaanzia jikoni.’

Anasema kupitia kampeni hiyo, mradi wa Cookfund unalenga kufadhili kampuni na wajasiriamali wanaojihusisha na uzalishaji na usambazaji wa nishati safi.

“Huwezi kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa bila kuleta mabadiliko ya nishati ya kupikia. Ufadhili wa EU unalenga ubunifu wa teknolojia ya kisasa ya kupata majiko yanayotumia mkaa, gesi na kuni kidogo. Tunatoa ruzuku kwa kampuni ili mtumiaji wa mwisho aweze kupata nishati na jiko kwa bei ndogo,” anasema.

Muro anasema kampeni ya ‘Anzia Jikoni’ inalenga kuueleza umma umuhimu wa matumizi ya teknolojia za kupikia zinazopunguza madhara ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Anatoa mfano kwamba kwa kaya zinazotumia kuni kwa ajili ya kupikia, mageuzi ya teknolojia yanaziwezesha kuendelea kutumia nishati hiyo kwa kiasi kidogo, wakiwa na jiko sanifu badala ya kutumia mafiga yanayohitaji kuni nyingi na kupoteza pia moto.

“Huwezi kumwambia mtu ambaye yuko kijijini anayepata kuni za bure atumie umeme au anunue gesi akakuelewa. Jiko sanifu linaweza kumshawishi kwa sababu linamsaidia kupunguza matumizi ya kuni na wakati huo huo, chakula chake kinaiva kwa wakati,” anasema.

Muro anaongeza: “Ufadhili wa EU unalenga kuongeza utaalamu wa kifedha katika uwekezaji ili kuchochea uwezo wa kampuni katika kuvumbua teknolojia safi za kupikia.”

Anasema mradi unalenga kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa za kupikia kwa kuhakikisha upatikanaji wake kwa urahisi.

Maelezo ya Muro yanaungwa mkono na Mratibu wa Kitaifa wa Mradi ya Nishati na Mazingira wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), Victor Akim, ambaye anasema matumizi ya nishati yanaendelea sambamba na majiko yanayotumia nishati kidogo.

“Tunahimiza matumizi ya majiko yanayopunguza matumizi ya nishati ili kila kaya ipate unafuu. Hili litasaidia kukabili athari za kimazingira,” anasema.

Anasema UNIDO inafadhili viwanda vinavyozalisha majiko na nishati mbadala ya kupikia, ili kuwezesha upatikanaji wake kwa wingi.

Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa Cookfund, Elizabeth Ngoye, anasema ndani ya miezi mitatu, watumiaji wapya 3,373 wamefikiwa na nishati safi ya kupikia, katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma na Mwanza, inayohusika kwenye mradi huo.

Kadhalika anasema mradi unalenga kuzifikia kaya mpya 580,000 na kuzalisha ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, kupitia kampuni 295 zinazokusudiwa kufadhiliwa kifedha na kiufundi.

“Tunategemea kupunguza matumizi ya mkaa zaidi ya tani 185,000 na kuokoa hekari 23,000 za msitu,” anasema Elizabeth.

Mvumbuzi wa jiko linalotumia umeme kidogo, Shukuru Meena, anasema jiko hilo sanifu linapika kwa kutumia presha ya mvuke unaokusanywa ndani ya sufuria.

“Linatumia nishati kidogo kuivisha chakula kwa muda mfupi na kuhifadhi virutubisho hivyo kuokoa muda, fedha, afya na mazingira; unaweza kuivisha maharage kwa umeme wa Sh. 200,” anasema Meena.

Anasema jiko hilo ambalo linamuundo kama lile la kupikia wali, linauwezo wa kupika vyakula vya aina mbalimbali kama maharage, ndizi, kande, mchemsho, ugali na pilau kwa njia ya kuchemsha, kurosti, kukaanga, kupika kwa mvuke na kuoka.