NYAMA MBADALA

21Jun 2023
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
NYAMA MBADALA
  • Singapore yawa taifa pekee kinapoliwa kitoweo cha kutengenezwa maabara

ONGEZEKO la hewa ukaa duniani au gesi chafu linachangiwa na kufuga wanyama wengi kienyeji kama inavyofanyika kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa, Manyara na Arusha.

Ni nyama inayotengenezwa maabara. PICHA :FOOD FOR THOUGHT

 

Wafugaji wa ng'ombe na wanyama wengine wanaocheua kama mbuzi na kondoo, wanaarifiwa kuwa mifugo hiyo hutoa ‘methane’, gesi chafu inayoongeza joto angani pale wanapoyeyusha nyasi na mimea.

Mchakato huo huitwa ‘enteric fermentation’ au "uchachushaji wa ndani ya tumbo," ndiyo asili ya kucheua kwa wanyama hao. Gesi ya methane pia hutolewa kutoka kwenye samadi na mkojo wa mifugo vyote huongeza joto duniani.

 

 

 

Ili kukabiliana na hali hiyo wanasayansi wameanza kuzalisha nyama kwenye maabara wakizilisha na kuzikuza seli za vipande vidogo vya minofu.

 

Ndicho kinachoendelea nchini Singapore na wateja huila migahawani bila kikwazo ikisifiwa na kila ailaye, kwa mfano: “Inaonekana kama kuku, ina harufu na ladha ya nyama ya kuku. Huwezi kuhisi kama kipande cha nyama kilicho mbele yako hakikutoka bandani.  Kumbe imetengenezwa katika maabara viwandani…” inaandika BBC Swahili.

 

Ni ndani ya mgahawa wa Huber's Butchery and Bistro nchini Singapore, ambao ndiyo pekee duniani unaouza nyama ya kutengenezwa na maabara katika menu yao. Kitalaamu huitwa minofu inayotengenezwa kutokana na seli za wanyama.

 

Wateja wanaotumia nyama hiyo wana maoni kwa mujibu wa mmiliki wa maelezo ya mmliki wa mgahawa, anayeongea na BBC, akiwanukuu wakisema ni nyama ya kimaadili, ni safi na bila kuathiri au kupunguza ladha.

 

Mabilioni ya dola yanamiminwa kwenye tasnia hiyo, tangu mkate wa nyama au burger ya kwanza ya kitoweo kilichokuzwa katika maabara ambao uligharimu Dola $330,000 au pauni £263,400.

Tangu mkate huo ulipozinduliwa London mwaka 2013, kampuni kadhaa duniani zimejiunga na harakati za kuleta nyama ya bei nafuu sokoni.

 

Kufikia sasa, ni kampuni ya ‘Eat Just’ pekee ambayo imeidhinisha bidhaa yake kuuzwa kwa umma baada ya wasimamizi nchini Singapore ambayo ni taifa pekee duniani kuruhusu nyama iliyokuuzwa kwenye maabara kuuzwa, biashara iliyoanza Desemba 2020.

 

Baada ya miezi michache mwaka huu Huber's imeanza kutoa sandwich au mikate iliyowekewa kuku na sahani ya tambi au pasta ya kuku kwa wateja ingawa ni mara moja pekee kwa wiki na sehemu ndogo za kulia zinapatikana si kila mahali.

 

"Nyama ya kuku ya kukuzwa kwenye maabara ni nyama halisi hivyo siyo lazima kuchinja mnyama," anasema Josh Tetrick, Ofisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya “Eat Just”, akizungumza na BBC kutoka San Francisco. "Njia hii ya kupata kitoweo ina maana na umuhimu kwa siku zijazo," anasema.

 

Tofauti na ile inayotengenezwa na mimea, nyama inayouzwa kwenye maabara ni halisi, mchakato wake unahusisha kutoa seli kutoka kwa mnyama, ambazo hulishwa na virutubisho kama vile protini, sukari na mafuta na hatua kwa hatua huwa minofu.

 

Seli hizo zinaruhusiwa kugawanyika na kukua, kabla ya kuwekwa kwenye chembechembe kubwa ya kibaiolojia ya chuma, ambayo hufanya kama tangi na kuchachusha na kwamba baada ya wiki nne hadi sita, 'huvunwa' kutoka kwenye kinu cha kibaolojia.

 

Protini fulani ya mboga huongezwa, kisha hutengenezwa, kupikwa na kuchapishwa kwa kutumia teknolojia ya 3-D ili kuipa sura na ulaini unaohitajika kama wa nyama halisi ya kuku.

 

"Ni nyama, ni kamilifu!" Anasema Caterina, mteja aliyefika mgahawani hapo ili kujaribu kuku wa kuuzwa kwenye maabara”.

Sahani ya tambi ya kuku huuzwa Dola za Singapore $18.50 au Dola za Marekani $13.70; takribani pauni £11, lakini hiyo imepunguzwa sana ikilinganishwa na gharama ya sasa ya kuzalisha nyama hiyo.

 

Eat Just haitasema ni kiasi gani hasa inachotumia kutengeneza kuku wake wa kukuzwa kwenye maabara, lakini  uzalishaji wa kampuni hiyo unatoa kilo mbili  au paundi 4.4lb au kilo 3.0 kwa wiki nchini Singapore.

 

BBC inasema kwa kulinganisha uzalishaji huo na kilo 4,000 hadi 5,000 za kuku wa kawaida inayouzwa kila wiki huko Huber pekee , inakupa picha ya ukubwa wa kazi iliyo mbele, kwa ufupi, watahitaji kuongeza uzalishaji kwa kiasi kikubwa ili kuepuka kupata hasara kwa kila kipande cha kuku.

 

NI WASIWASI TU

Kinadharia, kupunguza utegemezi wa dunia wa ardhi na mifugo kwa ajili ya kuzalisha nyama kunafaa kupunguza utoaji wa kaboni, lakini kwa sasa teknolojia ya hali ya juu inayohitajika kuunda nyama ya kukuuzwa ni ghali mno kiasi kwamba inatumia faida yote.

 

Utafiti wa Chuo Kikuu cha California, ulikadiria kuwa mchakato huo hutoa kati ya mara 4 na 25 zaidi ya kaboni dioksidi kuliko nyama ya kawaida ya ng'ombe. Hata hivyo, East Just imeuita utafiti huo kuwa una dosari".

 

Anapoulizwa na BBC kama mradi mzima unaweza kuishia bila mafanikio, Josh Tetrick kutoka Eat Just akiijibu: “kwa hakika".Lakini bado hajakata tamaa kutengeneza nyama kwa njia hiyo anayosema  ni muhimu.”

 

"Sio moja kwa moja. Ni vigumu. Haina dhamana na inaweza isifanyike. Lakini chaguo lingine kwetu ni kutofanya chochote. Kwa hivyo tuliamua kuchukua dau na kuichukua hatua hii."

 

Wawekezaji wengi wameamua kufanya dau kama hilo. Kufikia mwaka huu, inakadiriwa Dola za Marekani bilioni 2.8 zimetumika katika kuendeleza nyama ya maabara.

Hata hivyo, ikiwa nyama iliyokuuzwa kwenye maabara itakuwa ni mbadala kwa watu walio na uwezo mkubwa katika dunia au nchi zilizoendelea, basi kutegemea uwekezaji huo kufanywa na watu binafsi kunaweza kukwama.

 

Serikali, zitahitaji kuweka fedha nyingi katika nyama ya kukuuzwa kwa njia hii ili kushindana na kitoweo cha mifugo iliyochinjwa baada ya kutunzwa na kulishwa kwenye mashamba ya wakulima."Hii ni kama mpito au kama ilivyo kwenye kusaka nishati mbadala. Kuna kazi ngumu zaidi.”