Serikali ya awamu ya sita kwa kutambua hilo imeanza kutekeleza mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari kwa njia mbadala (SEQUIP) ukilenga mabinti ambao wameshindwa kusoma kwa sababu mbalimbali.
Lengo serikali inasema ni kumpa fursa ya kupata elimu mtoto wa kike aliyepatwa na madhila ikiwamo mimba za utotoni, maradhi au, shida za wazazi na matatizo ya kifamilia na kushindwa kumaliza kidato cha nne.
Mradi huo unalenga kuwafikia wasichana 12,000 nchi nzima wenye umri wa kati ya miaka 13 hadi 21 katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka jana, anasema Mratibu Msaidizi wa SEQUIP, kutoka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Amina Abubakari.
Ni wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wawezeshaji wa somo la stadi za maisha kutoka vituo vinavyotoa elimu mbadala kupitia mradi huo, Mratibu wa SEQUIP Amina anaeleza kuwa wasichana walioacha masomo kutokana na sababu mbalimbali waende vituoni kwani wanapatiwa elimu bure na serikali.
Anafafanua kuwa katika kufanikisha lengo hilo serikali imeandaa moduli za kufundishia zinazompa urahisi wa kujifunza kwa muda wa miaka miwili mlengwa.
Amina anasema licha ya somo hilo la stadi za maisha, pia kemia na fizikia ambayo awali hayakuwamo sasa yameingizwa katika mfumo huo ambao mwanafunzi anasoma bure wakati serikali ikimlipia hadi ada ya mitihani ya taifa.
Wakati wa mafunzo hayo yanayowakutanisha pamoja wawezeshaji wa somo la stadi za maisha takriban 85 kutoka mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Tabora, Arusha, Manyara, Simiyu, Shinyanga, Dodoma, Mara, Kigoma na Singida, mratibu huyo anabainisha kuwa lengo ni kujengewa uwezo wa kutumia njia shirikishi za ufundishaji zinazozingatia ujengaji wa umahiri kwa wanafunzi.
“TEWW tulijiwekea lengo la kuwafikia wasichana 3,000 kila mwaka kuendelea na masomo ya sekondari, ninayo furaha tuliweza kusajili walengwa 3,333 mwaka uliopita wa 2022 na huu 2023 tumesajili wasichana 3,616 sawa na asilimia 120.5,” anasema Amina.
Anabainisha kuwa mradi huo ulioanza mwaka jana utafikia tamati mwaka 2026 na kwamba katika kipindi cha mwaka jana wasichana 3,333 walisajiliwa katika vituo 131 nchini huku mkoa wa Mbeya ukiongoza kwa kusajili wasichana 472 ukifuatiwa na Mwanza.
“Tangu kuanza kwa mradi huu unaosimamiwa na Wizara ya Elimu na TAMISEMI kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB) tumeanza kwa mafanikio makubwa ambapo vituo kwa ajili ya mradi huo vimeandaliwa moduli za kujifunzia kumwezesha msichana kujifunza kwa urahisi hata akiwa nyumbani. Baada ya kuhitimu na iwapo watafaulu vizuri watachaguliwa kujiunga na vyuo vya kati kote nchini.”
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Pasikasi Muragili, akifungua mafunzo anaipongeza menejimenti ya TEWW na mikakati iliyoleta mradi wa SEQUIP kwa kuandaa na kuendesha mafunzo hayo muhimu katika kutekeleza mradi huo.
Muragili anasema huo ni mwendelezo wa nia njema ya serikali ya awamu ya sita ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, wa kutoa elimu bila malipo na sehemu ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kitaifa na kimataifa.
“Tunampongeza Rais kwa dhamira yake njema ya kumkomboa mtoto wa kike, washiriki zingatieni yale yote yatakayoelekezwa ili kuongeza ufanisi katika ufundishaji wa stadi za maisha kwa wasichana wanaoendelea na masomo katika vituo mbalimbali ambao ndoto zao zilikatishwa,” anasema.
Mkuu wa Wilaya anaongeza kuwa kinachofanywa na serikali ya awamu ya sita ni kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM inayoelekeza kuongeza fursa ya upatikanaji elimu kwa makundi mbalimbali wakiwamo wasichana hao.
Anaagiza licha ya kuwafundisha pia wafuatilie nyendo zao baada ya elimu ili kubainisha matokeo mazuri ya wasichana hao kupitia jitihada za Rais Samia kuwarudisha shuleni.
Mmoja wa washiriki Mwalimu Catherine Luwa, kutoka mkoa wa Singida, akizungumza baada ya ufunguzi anamshukuru Rais Samia kwa kufanya jambo hilo kubwa la kuwarudisha shule wasichana waliokatisha masomo ya sekondari kutokana na sababu mbalimbali.
Anaeleza kuwa mafunzo hayo yana mwelekeo wa kuwajengea uwezo zaidi wa namna ya kuwafundisha wasichana hao ambao bila shaka miongoni mwao siku zijazo watakuja kushika nyadhifa mbalimbali serikalini.
Mkufunzi mkazi kutoka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima mkoani hapa, Abtwalibu Salimu, anasema kupitia mradi huo mkoa wa Singida katika kipindi cha mwaka jana ulisajili wasichana 114 waliokubali kurejea shule ambao wanasoma katika vituo vya Iramba, Singida Manispaa na Mkalama.
Ofisa Elimu ya Watu Wazima na Eimu ya Nje ya Mfumo Rasmi, wilayani Manyoni, Emmanuel Mwarabu, anasema moja ya changamoto wanayokutana nayo wasichana hao ni umbali kutoka maeneo wanayoishi na vituo vya kujifunzia vilipo.
Anatoa wito kwa serikali kwamba dhamira njema ya kuwarudisha shule wasichana hao itafikia malengo iwapo watajengewa mabweni akisema: “Kuna wengine wanaweza kuvunjika moyo kutokana na umbali kutoka wanakoishi hadi vituo vyao vya kusomea vilipo.
“Mwongozo wa masomo yao ni mzuri unamwezesha wakati mwingine hata kujisomea mwenyewe nyumbani lakini hili la kukaa karibu na eneo wanalofundishwa ni jambo jema,” anasema Mwarabu.
WAHUSIKA WAMULIKWE
Mwalimu Sospeter Makwaia kutoka Sengerema mkoani Mwanza, anakazia kuwa kuna haja kwa serikali kuweka mazingira ya kusomea wasichana hao ili lengo la kuwarudisha shule liweze kutimia miongoni mwa wengi wao.
Anasema uzoefu unaonyesha wachache miongoni mwa wasichana hao wavulana waliowasababishi ujauzito bado wanaendelea kuwa na uhusiano nao wa kimapenzi hadi sasa hali ambayo kutokana na umri wao inaweza isifanikishe lengo lao kurudi shuleni kwa mara ya pili.
Mwalimu Makwaia pia anashauri hamasa zaidi ya kuwarudisha shule wasichana hao kwani anaamini wengi wa walio majumbani watahusika kurudi shule.
Anatolea mfano katika kituo anachofundisha mwaka jana walisajiliwa wasichana 12 na mwaka huu wameongezeka kufikia 18 idadi ambayo ana uhakika inaweza kuongezeka zaidi mwakani iwapo hamasa itazidishwa.
Zulina Juma mwanafunzi wa kituo cha Shule ya Msingi Ipembe mkoani Singida, anashukuru serikali kwa kuanzisha mradi huo ambao utafufua ndoto za wasichana wengi zilizokufa baada ya kuacha shule kutokana na sababu mbalimbali.
“Niliacha shule mwaka 2021 kutokana na kuugua kifua kwa muda mrefu, nimeanza tena mwaka huu hatua ya kwanza ambayo nataraji kumaliza mwakani,” anasema Zulina.
CHANGAMOTO ZILIZOPO
Zulina anabainisha changamoto wanazokutana nazo kituoni hapo ni kelele za wanafunzi wa shule ya msingi zinazowanyima utulivu wa kujisomea hadi muda wanaporuhusiwa kuondoa ambao na wa shule ya msingi nao wanaondoka.
Anaiomba serikali iwajengee vituo vyao tofauti, pia wawekewe vifaa vya elimu kwa vitendo kwa wanaosoma masomo ya sayansi pamoja na kusaidiwa taulo za kike kwani ni huduma muhimu kwa vile miongoni mwao wamo wasiojiweza kabisa kifedha.









