ROSETTLE LOWHIM

21Jun 2023
Pilly Kigome
DAR ES SALAAM
Nipashe
ROSETTLE LOWHIM
  • Injinia aliyeshinda usaili lakini akatoswa ajira, kisa mwanamke, Ni mgunduzi mahiri akihusika na jiko sanifu

ROSETTLE Lowhim ni mwanafunzi wa shahada ya uzamivu ya uhandisi katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam [DIT], ambaye amekuwa pambo na chachu kwa wengine kwa namna anavyojitahidi kuitumia teknolojia kubadilisha maisha yake na ya wengine.

Mhandisi Rosettle Lowhim wa DIT akiwa kazini kutengeneza mashine ya kubangulia karanga. PICHA: MWANDISHI WETU

 

Akiwa bado masomoni ameunda mashine kadhaa zinazotumiwa na mafundi vyuma anaposema mwaka 2021 hadi 2022 akiwa mwaka wa tatu wa shahada ya kwanza ya Uhandisi Mitambo (mechanical engineering) alibuni na kutengeneza mashine za urembo unaotokana na kukunja vyuma.

Anaitambulisha kama ‘semi automatic metal scrolling and twisting machine’ inayotumiwa kukunja vyuma kutengeneza urembo kwenye madirisha ya grili, milango, mageti na mapambo mbalimbali.

Mara nyingi urembo wa madirisha, vitanda, milango, meza, uzio na mapambo mengine hutengenezwa kwa kukunja na kusuka nondo au ‘square pipes na flat bars na pengine hakukuwa na mashine ya kuzikunja kupata maumbo mbalimbali bali kazi hizo hufanyika kienyeji.

Rosettle anasema mbali na mashine hiyo pia amegundua na kutengeneza nyingine ya kubangua karanga [groundnut cracking machine] ambayo tayari iko sokoni.

Kadhalika anasema amebuni jiko maalum la umeme la kukaangia crips na chips linalotumia nishati kidogo lakini likifanyakazi kwa ufanisi mkubwa na kusaidia kupunguza matumizi ya mkaa na kuni yanayochangia kuharibu misitu na kuchochea mabadiliko ya tabianchi.

ANATAJA PAGUMU

Msomi anakumbushia kuwa licha ya juhudi na jitihada za kufanikisha maendeleo ya sayansi na teknolojia, anakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kutoaminika kwenye ajira kwa vile ni mwanamke, hivyo kukosa kazi.

Anasema kutokana na jinsi yake mbali na kuwa na uwezo mkubwa kufanya vizuri katika kazi lakini inamuwia vigumu kuaminika kikazi jambo linalomshangaza na kumuumiza msomi huyo.

Anaendelea kuiambia Nipashe kuwa, amewahi kukosa kazi kutokana na jinsi yake (KE) katika moja ya kampuni kubwa nchini (jina tunalihifadhi) alipokwenda kufanya usaili.

Anasema aliambiwa kuwa amefaulu kwenye usaili lakini baadaye mkuu wa kampuni alipogundua ni mwanamke, akamkataa akakosa kazi hiyo, japokuwa alifanya vizuri katika usaili na kuibuka kidedea.

Rosettle anafafanua kuwa ndoto zake kubwa ni kuja kumiliki karakana ama kampuni kubwa ya kisasa nchini itakayoweza kuhudumu ndani na nje ya mipaka kwenye masuala ya teknolojia na uhandisi.

KUCHOCHEA WANAWAKE

Ubunifu na mabadiliko ya teknolojia ni chachu ya kuleta usawa wa kijinsia, ni kauli mbiu ya kitaifa inayotumiwa kuwachochea wanawake kama sio kuwatoa kimasomaso mijini na vijijini katika kujihusisha na kunufaika na teknolojia.

Lengo ni ili usawa unapatikane kupitia nyanja hiyo, na kuwaamsha wanawake wengi ambao wamebaki nyuma na kukosekana usawa kiteknoloji na hata kijinsia.

Mtandao wa Jinsia Tanzania [TGNP] na Chuo cha DIT, wanaingia ubia kusaidia kufanikisha kazi za ubunifu za kiteknolojia na kutatua changamoto za kijinsia kama sehemu ya kuwapa fursa na hamasa wasichana wanafunzi kufanya vizuri katika eneo hilo 76la sayansi na teknolojia.

Taasisi hizi zimetengeneza kanzi data inayoitwa Tanzania Women Connect Portal inayohifadhi kazi za wanawake katika nyanja mbalimbali itakayowezesha kupata na kunufaika na fursa mbalimbali kwenye harakati za kuleta usawa wa kijinsia nchini.

Mwenyekiti wa Bodi TGNP, Gemma Akilimali, anaiambia Nipashe kuwa kuwawezesha wanawake na makundi mengine katika teknolojia kuna matokeo chanya hasa katika ubunifu ili kupata suluhisho kwa shida za kijamii na uvumbuzi mwingine unaowasaidia wanawake na watoto wa kike kupata mahitaji ili kuchochea ufikiwaji wa usawa wa kijinsia.

Anafafanua kuwa suala kuu mwaka huu lilijikita katika kuwatambua wanawake na wasichana wanaochochea maendeleo chanya ya kidijitali na teknolojia pamoja na kuwaandalia nafasi ya ugunduzi na ubunifu katika kuchochea usawa wa kijinsia na kuleta mwendelezo yenye tijja kwa wanawake na wasichana.

Akilimali aliainisha kauli mbiu hiyo itatoa fursa ya kutathmini athari za pengo la kijinsia la kiteknolojia katika kuzuia upatikanaji wa usawa katika fursa za kijamii na kiuchumi.

Anabainisha takwimu zinazoonyesha kuwa uwepo mdogo wa kundi hili la wanawake katika sekta ya teknolojia unaleta hasara kubwa akikariri taarifa ya Shirika la Umoja ya UN Women Gender Snapshots 2022, anasema kukosekana wanawake katika ulimwengu wa kidijitali kumepoteza dola za Marekani trilioni moja katika pato la taifa kwa nchi zenye uchumi wa chini.

Hasara hiyo inatarajiwa kukua hadi kufikia dola za Marekani trilioni 1.5 ifikapo 2025 ikiwa hakuna hatua zitakazochukuliwa kuleta  ujumuishi wa kundi hilo la wanawake katika masuala ya teknolojia.

Takwimu za Internatinal Telecommunication Union (ITU) kwa mwaka 2019 zinaonyesha kuwepo kwa pengo la kijinsia katika matumizi ya mitandao duniani kwa asilimia 10, wanawake ni asilimia 48 wakati wanaume ni aslimia 58.

Aidha, takwimu za GSMA Intelligence Tanzania zinaeleza pengo la kijinsia kwa asilimia 11 ambapo wanawake ni asilimia 77 na wanaume ni asilimia 86.

Kutokana na hali hii michango, simulizi na mafanikio ya wanaume yanaonekana au kusikika zaidi kuliko ya wanawake na umaskini umekuwa ni kikwazo kikubwa kwa kinamama.