Anasema miaka ya nyuma kidogo, hospitali hiyo haikuwa na uwezo wa kufanya vipimo vya aina yoyote kwa wagonjwa wake, na hivyo walilazimika kuwapeleka wagonjwa wao Morogoro au Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Kwa sasa mambo yamebadilika, ile historia mbaya ya Hospitali ya Rufaa ya Dodoma imefutika, kwa sasa tuna vifaa vizuri vya kisasa ambavyo hata katika hospitali nyingine hawana, na kazi hii nzuri imefanywa na MSD,”anasema Dk.Ernest.
“Mashine zote za kisasa za kupimia zilizopo katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma tumepata MSD, zamani vipimo tulikuwa tunalazimika kuvituma mpaka Dar es Salaam ndio vikapimwe halafu turudishiwe tena, lakini kwa sasa kila kitu tunafanya sisi wenyewe baada ya kupata vifaa hivi.
“Kama ni maboresho, kati ya asilimia 10, sisi tumefikia asilimia 9.8 ukilinganisha na kule tulikotoka, yaani tumebadilika pakubwa sana, ilikuwa ni aibu mwanzoni, mgonjwa alikuwa akija hapa kumpima unapima wingi wa damu tu.
Anasema kabla ya kupata vifaa hivyo, walikuwa na uwezo kuhudumia wagonjwa watatu tu waliozidiwa kwenye chumba cha dharura, kwa sasa baada ya kupata vifaa kutoka MSD wanahudumia wagonjwa waliozidiwa 36 na kila mgonjwa anakuwa na kifaa chake.
“Sasa hivi ukienda maabara unashangaa tu, maana vifaa vilivyopo kwa sasa hatujawahi kuwa navyo. Miaka ya 2014 kurudi nyuma wagonjwa wengi walikuwa wakija hapa hospitalini na kuangalia mazingira walikuwa hawakubali kutibiwa, lakini leo tunazungumza historia mpya.
“Tuna mashine za kisasa ambazo ukifanya vipimo, ndani ya dakika moja tu zimeshatoa majibu kwa sababu zimeunganishwa na intaneti, majibu huwa yanaenda moja kwa moja kwa daktari. Zamani kabla ya kupata mashine hizi, tulikuwa tunapiga picha kwenye mashine za kizamani halafu tunazibeba kwenda kuzianika wakati mwingine hadi saa tatu ndio majibu yaanze kusoma.
“Kwa hiyo imerahisisha sana majibu yanatoka haraka, yanafika kwa daktari haraka, lakini pia imepunguza gharama na vitu vingine kama hivyo. Zamani tulikuwa ukipiga ‘exlay’ mgonjwa mmoja mpaka ukae tena dakika 15 ndio umpige mwingine, lakini mashine za sasa hivi ni unapadisha mgonjwa mmoja na unamshusha hapo hapo na unampandisha mwingine, kwa hiyo ndani ya saa moja unaweza kupiga hata ‘x-ray’ 100.”
Dk. Ernest anadems, miaka ya nyuma mashine zilikuwa mbili tu kwa mkoa wa Dodoma, moja katika hospitali ya Dodoma na nyingine Hospitali ya Mirembe.
“Kwa hiyo ikiharibika, wagonjwa tulikuwa tunawaambia wakapige Dar es Salaam au Morogoro. Tunashukuru sana uwekezaji ambao umefanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, hospitali yetu inavyoonekana kwa sasa si kama ilivyokuwa zamani, tulikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, lakini kwa sasa tunapata dawa nyingi na vifaa tiba vya kutosha kutoka MSD,”anasema.
“Zamani ulikuwa ukifika hapa ukiangalia mazingira unawaza hivi nitapona kweli, lakini kwa sasa ukifika unaona tayari una nafasi kubwa ya kupona. Hivi vifaa tiba vilivyopo hapa kwa sasa zamani tulikuwa tunaviona tukienda kwenye hospitali za wenzetu.”
Anasema upatikanaji wa dawa kwa sasa katika hospitali hiyo ni asilimia 96 kutoka asilimia 40 ya mwanzo.
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano MSD, Etty Kusiluka, anasema asilimia 95 ya vitu vilivyopo katika hospitali hiyo vinatoka MSD ukitoa meza, kompyuta na viti wanavyotumia wafanyakazi.
“Lakini kuanzia vitu wanavyovaa, yaani vitambaa vya sare zao za kazi, mashine, vitanda, magodoro, kadi za wagonjwa, kalamu, dawa, vifaa vya maabara, na kila kitu kilichopo katika hospitali hii kimetoka MSD,”anasema Kusiluka.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Tukae Mavere anasema Bohari hiyo hufanya usambazaji wa bidhaa za afya hadi mlangoni mwa vituo vya afya kila baada ya miezi miwili mara sita kwa mwaka na kuvifikia vituo vya kutolea huduma za afya vya ngazi zote.
“Usambazaji wa bidhaa za afya unafanyika kwa kutumia magari 185 ambapo bidhaa hupakiwa kwa mujibu wa mahitaji ya wateja na hupokelewa kwa kutumia mfumo wa kielektroniki unaotunza takwimu za upokeaji (Proof of Delivery).
Kuhusu maboresho wanayofanya, Mavere anasema ili kuendana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, MSD inafanya mapitio ya mnyororo wa ugavi ili kuimarisha ununuzi wenye tija, kuepuka upotevu na kupata bidhaa kwa bei nzuri.
Kufunga mashine zaidi katika maabara na usambazaji wa vitendanishi ili kusogeza huduma kwa wananchi, kupunguza gharama za uchunguzi, na kuongeza upatikanaji wa huduma kwenye vituo.
Pia, anasema wamejipanga zaidi kwa usimamizi na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa vihatarishi, kuwezesha kazi zote za mnyororo wa ugavi kufanyika kijiditali.
Nyingine anasema ni kuimarisha usimamizi wa watumishi kwa kuboresha mifumo ya upimaji utendaji kwa kutumia mifumo ya kidigitali, kuboresha usimamizi wa shughuli za taasisi kupitia ofisi ya kimkakati.
Kuhusu uboreshaji wa miundombinu ya kuhifadhia bidhaa za afya, Mavere anasema MSD imeendelea kuwekeza pia katika eneo hilo kwa kuhakikisha inakuwa na maghara ya kutosha kwa ajili ya kuhifadhia.
Anasema wanayo maghala ya kuhifadhia katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwamo yenye ukubwa wa mita za mraba 69,758.57, ambayo mengine huwezesha kuhifadhi bidhaa toshelevu za miezi tisa.
“Maghala yamejengwa kwa kufuata vigezo vinavyokubalika vya ubora ili kuhifadhi bidhaa za afya kwa kufuata miongozo ya watengenezaji. Bidhaa zote zinapokelewa, zinatunzwa na kutolewa ghalani kwa kutumia mfumo,”anasema.
Kuhusu mkakati wa MSD katika kuendana na ukuaji wa sekta ya afya nchini, Mavere anasema ni kuhakikisha wananunua bidhaa kutoka kwa wazalishaji nchini ili kupunguza muda wa uagizaji na kuwajengea uwezo wazalishaji, kufanya ununuzi moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji wa nje kwa bidhaa zisizokuwapo nchini ili kupunguza bei na kupata bidhaa kwa wingi.
Jinginme anasema ni kutumia mifumo ya ununuzi ya kidigitali na kuwa na mikataba ya muda mrefu, kukamilisha uanzishwaji wa kampuni tanzu itakayosimamia uendeshaji wa viwanda, kuendelea kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya ashiria kufikia asilimia 90, kufuatia matumizi ya bidhaa za afya, kupunguza upotevu na kuboresha upatikanaji.










