Kumbe inawezekana kote kupikia umeme iwapo tu…

28Mar 2023
Christina Mwakangale
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kumbe inawezekana kote kupikia umeme iwapo tu…

YUNITI ya umeme inauzwa Shilingi 357 wakati kipimo kidogo cha mkaa kinagharamu mpaka Shilingi 2,500 kutegemea mahali unapopatikana. Lakini hakiivishi kilo ya maharage.

Mtendaji Mkuu wa SESCOM, Sawe (kulia), pamoja maofisa wa kampuni hiyo wakitambulisha majiko sanifu yanayotumia umeme kidogo. PICHA: SESCOM

Ni ajabu umeme hautumiki kupikia badala yake watu wanapigwa kwenye kuni na mkaa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya SESCOM inayoshughulika na utafiti wa nishati mbadala Estomih Sawe, akizungumza na wanahabari, jijini Dar es Salaam, anasema taifa linaweza kupikia umeme tena kwa tija na unafuu zaidi.

Anasema zinahitajika mbinu na ubunifu kuleta vyanzo nafuu na vyenye ufanisi kwa ajili ya kupikia na SESCOM, imeunda majiko sanifu ya umeme yanayotumia nishati kidogo kupika vyakula vigumu kama maharage na makande kwa muda mfupi na kifanisi.

“Kwa mfano jiko letu linapika kilo ya maharage kwa nusu uniti sawa na Shilingi 146, uniti inauzwa Sh. 357, tena kwa dakika kadhaa. Kama yamelowekwa muda na uniti hupungua zaidi.” Anaeleza.

Analinganisha kuwa endapo mpishi atatumia mkaa utagharimu zaidi ya Sh. 3,000 kwa kuwa atahitaji zaidi ya vipimo viwili na muda mrefu pia.

Anaongeza kuwa juhudi za SESCOM zinalenga kutunza mazingira lakini pia kupunguza gharama za kupikia kuni na mkaa ambazo ni kubwa.

Anasema kampuni hiyo imeunda jiko la presha linalotumia umeme linaloitwa JULEP la teknolojia sanifu linalopunguza utegemezi wa kuni na mkaa.

“Teknolojia hii haijajulikana ingawa ni nafuu kuliko kuni, mkaa, mafuta ya taa na gesi za mtungi,”anasema Sawe.

Akifafanua matumizi ya jiko anasema yanaondoa athari kwenye mazingira na kiafya na kusisitiza umuhimu wa serikali na kuondoa kodi, ili majiko haya yauzike kwa bei nafuu na wananchi wengi zaidi wamudu.

“Wananchi wakiyahitaji yanauzwa kwa bei ya punguzo katika mikoa ya Mwanza, Dodoma na Morogoro na Pwani kutokana na ruzuku iliyotolewa na mradi unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya na EU na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Mitaji (United Nations Capital Development Fund – UNCDF).”

SESCOM inashirikiana na TANESCO wadau wakuu, ili wateja wao watumie jiko hilo, kwa gharama nafuu na linatumia umeme kidogo pia linatunza mazingira, akisema gharama yake inaanzia Shilingi 150,000, anasema.

“Wakati dunia ikipambana kuwapo na ubunifu na matumizi nishati mbadala, ifikapo 2030 lengo namba saba, litatimia tukihakikisha kila mtu anafikiwa na nishati hiyo kwa gharama nafuu,” anaongeza Sawe.

Akitoa ufafanuzi zaidi kuhusu jiko hilo, Albina Minja, ofisa wa kampuni hiyo, anasema ni sanifu lililoundwa kwa ufanisi na wakati wa kupikia linaongeza joto lakini baada ya muda linahifadhi joto kali linaloendelea kupika.

“Haliruhusu mvuke kutoka, hivyo joto halitoki nje na chakula huiva kwa mvuke tena lina usalama wa hali ya juu. Tunatoa mafunzo ya namna ya kulitumia kwa usahihi na tunafundisha mafundi, vikundi mbalimbali na mtu ambaye analitumia,” anasema Albina.

Kadhalika, Meneja wa kampuni hiyo, Shukuru Meena, anaongeza: “Tunaipongeza serikali kwa kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata umeme. Majiko haya yanatumia umeme kidogo na afya inaboreka, uchumi wa nchi unastawi pia.”

Meena anasema wanafanya kampeni za kuelimisha wananchi kuhusu faida za kiuchumi ambazo watapata na kueleza umuhimu wakinababa kuwapa moyo na kuuwaunga mkono kifedha ili kinamama kununua na kutumia jiko hilo, kwa sababu ni rahisi, hawachafuki, wala hawachafui mazingira.

Anaongeza kuwa Tanzania inaweza kuacha kutumia kuni na mkaa na kutumia jiko linalotumia nishati ya jua na kwamba kuna mbadala wa uhakika na endelevu, gharama nafuu kwa kila Mtanzania, kwani taifa linayo nishati na kwamba ukiwa na JULEP huna haja ya kuhangaika kutafuta mkaa na kuni ambazo si salama kwa afya wala mazingira.

HALI NI MBAYA

Kwa mujibu wa takwimu zinazotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira,

asilimia 85 ya Watanzania wanategemea kuni na mkaa  kupikia hatua

inayochangia upotevu wa hekta 372,000 za misitu kila mwaka.

 

Iwapo asilimia hiyo inayofikia watu milioni 52 hupikia kuni na mkaa kupika, ni wazi itafika siku hakutakuwa na mti wala kichaka baada ya miti yote kuwa majivu kwenye majiko ya mijini na vjijini.

Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ya mwaka 2020, inaonyesha kuwa asilimia 63.5 ya kaya zote hutegemea kupikia.

UMUHIMU WA MAJIKO

Ili kuishi kula ni lazima na mlo hupikwa kwa nishati safi na kwa teknolojia sanifu na endelevu ambayo ni muhimu kwa maisha bora.

Lengo namba saba la malengo ya maendeleo endelevu (SDGs-2030) ya Umoja wa Mataifa (UN), ambayo pia ni makubaliano ya mkutano wa Paris, kuhusu kutunza mazingira, huku ripoti mbalimbali zikisema nchi zenye wakazi zaidi ya milioni 55.6 hawatumii nishati na teknolojia za kisasa kupikia.

Sawe analizungumzia hilo akisema walikuja na jiko hilo baada ya kubaini, sehemu kubwa ya kuni na mkaa huwashwa kwenye majiko yasiyo sanifu, mfano kwenye jiko la mafiga matatu kwenye ufanisi wa chini ya asilimia 10.

Jiko hilo ndilo linalotumiwa na asilimia 95 ya Watanzania waishio vijijini na kwamba asilimia 26.2 ya kaya hutegemea mkaa na asilimia 5.1 huitegemea gesi ya mtungi au LPG wakati asilimia tatu pekee hutegemea umeme. Sehemu za mijini kaya nyingi hutumia jiko la bati la mkaa, lenye ufanisi wa chini ya asilimia 15.

HATUA ZA NCHI

Wastani wa Watanzania 33,000 hufariki kila mwaka, kutokana na moshi wa kupikia, kwa mujibu wa Waziri wa Nishati, January Makamba, anayeeleza hayo jijini Dodoma, Septemba, mwaka jana.

Anatoa takwimu kwenye semina ya kuwajengea uwezo wabunge wanawake kuhusu matumizi ya nishati mbadala nyumbani.

Kwa sasa umeme umefikia asilimia 78.4 ya kaya zote nchini, ingawa kiasi cha watu kinachotumia bado ni kidogo kwa asilimia 37.7, anasema Waziri Makamba.

Kadhalika, umeme katika kaya nyingi unatumika zaidi kwa ajili ya mwanga, kuchaji simu, kuwasha redio, kuangalia televisheni na matumizi mengine madogo, lakini si kupika Makamba anasema.

Aidha, anasema kaya zenye umeme, hununua nishati kama LPG, mkaa na kuni, kwa ajili ya kupikia.

CHANGAMOTO

Pamoja na faida nyingi zitokanazo na kupika kwa nishati safi ikiwamo ya kiafya, mazingira na uchumi, bado kuna kukwama kufanikisha matumizi mapya.

Ni kutokana na sababu kadhaa kama sera, wafanyabiashara na watumiaji. Sera na mikakati ya kuendeleza nishati na teknolojia za kupika zinapewa kipaumbele kidogo na kutokuwapo bajeti, uwekezaji wa kutosha wa kukuza upatikanaji na matumizi, nacho kikwazo.

Baadhi ya teknolojia za kisasa za kupikia zinaagizwa kutoka nje na kutozwa kodi ya zaidi ya asilimia 40 ya bei ya kununulia na kuzifanya bidhaa hizo, kuwa ghali na kaya nyingi kushindwa kuzimudu.

Zipo teknolojia sanifu kama majiko sanifu ya umeme yenye presha kama vile JULEP, ambayo hayajajulikana sana ingawa ni nafuu kuliko kuni, mkaa, mafuta ya taa na LPG.

Kikwazo ni teknolojia na gharama ya kununulia jiko lenyewe, ambayo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na kuwapo kwa kodi kubwa inayofikia asilimia 46 (VAT 18% kwa mwagizaji na VAT asilimia 18 kwa msambazaji na ushuru wa kuagiza  asilimia 10).