Afrika Mashariki imo mbioni kuvuna utajiri ndani ya taka za kielektron

28Mar 2023
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Afrika Mashariki imo mbioni kuvuna utajiri ndani ya taka za kielektron

BIDHAA za kielektroniki kama kompyuta, simu, rimoti, ving’amuzi, televisheni kamera na betri zina viambato na vifaa ambavyo vinapofikia mwisho wa matumizi vinazalisha taka za kielektroniki.

‘E waste’ na taka za plastiki si salama kwa mazingira, ni hatari kwa ustawi wa viumbe na mfumo mzima wa ikolojia unaomaanisha maingiliano ya binadamu na mazingira yake wakiwamo viumbe hai walioko angani, ardhini na baharini au majini .

Hata hivyo, utaalamu unawezesha taka hizi za kielektroniki baada ya muda wa matumizi kumalizika tofauti na nyingine zilizozoeleka kwenye mazingira zinaendelea kurejelezwa na hata kutumiwa na mafundi wengine kama vipuri au spea kwa ajili ya kuunda vifaa vingine.

Ripoti ya taifa ya masuala ya taka za kielektroniki ya Tanzania Bara ya mwaka 2019 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa 2007 zilizalishwa tani 12,500 na miaka 10 baadaye ziliongezeka mara mbili zaidi na kwamba ilipofika 2017 zilizalishwa tani 35,800.

Kwa mujibu wa ripoti ya taarifa kwa umma kuhusu kanuni za udhibiti na usimamizi wa taka hatarishi ya mwaka 2019 iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, ongezeko la taka za kielektroniki linachochewa na matumizi ya bidhaa za kielektroniki hasa simu, kompyuta, runinga na redio.

Kwa mujibu wa Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP), kila mwaka tani milioni 50 za taka za kielektroniki huzalishwa duniani zikiwa na thamani ya Dola za Marekani bilioni 62 takribani Shilingi trilioni 142.4.

Hata hivyo ni asilimia 20 pekee ya taka hizo za kielektroniki ndiyo hurejelezwa katika mazingira rasmi ili kupata bidhaa mpya bora na zisizo na athari kwa ikolojia.

Katibu Mkuu wa Taasisi ya Mawasiliano Afrika Mashariki (EACO), Dk. Ally Simba, anabainisha hayo katika kongamano lililojumuisha wadau kutoka nchi saba wanachama, wenye lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kumaliza tatizo hilo, kuwa wananchi hawana uelewa nini maana ya taka za kielektroniki na madhara yake.

Anasema pia kuna ongezeko la taka nchini kiasi cha tani 17,000 kwa miaka 21 kunakotakana na kungezeka matumizi ya vifaa vya kieletroniki kunakochagizwa na matumizi ya teknolojia ya mawasiliano.

Anafafanua kuwa vifaa hivyo vinaingia nchini kama misaada lakini kumbe vimekwisha muda wa matumizi hivyo kuwa sehemu ya dampo ya taka hizo.

Katibu Mkuu wa EACO, anataja sababu nyingine kuwa ni vifaa vya kielektroniki vilivyonunuliwa na muda wake wa matumizi kumalizika.

“Kuna ongezeko la kasi, tunaingiza taka za kieletroniki tani milioni 60 kwa mwaka, hivyo mnaona ni nyingi sana kama hakutakuwa na mkakati wa kuzidhibiti,” anasema Dk. Simba.

Anafafanua kuwa takwimu za mwaka 1998 zinaonyesha kuwa nchini kulikuwa na tani 2,000 za taka zitokanazo na vifaa vya kielektroniki na hadi kufika mwaka 2019 ziliongezeka na kufika tani 19,000.

Anataja athari za kuwapo kwa taka hizo ni kugeuka kuwa sumu kwa watumiaji wakiwamo watoto wanaozichezea betri na simu za kuchezea.

Anaeleza kuwa kuchanganya taka za kielektroniki na za kawaida kunachafua maji, ardhi na mazingira kwa ujumla kwa sababu zina kemikali hatarishi nyingi na kuongeza kuwa watu bilioni 7.7 duniani hutumia simu za mkononi ambazo zinadumu kwa mwaka mmoja hadi miwili na kugeuka kuwa taka.

Anasema taka za kieletroniki siyo tatizo peke yake bali ni fursa kwa sababu zina madini mengi na kama ukipatikana utaratibu mzuri wa kuzichakata na zinakuwa fursa kwenye biashara.

UELEWA WA MAFUNDI

Fundi vifaa vya umeme Jumanne Issa wa Mabibo jijini Dar es Salaam, anazungumza na Nipashe akisema anapokea vifaa kama majagi ya kuchemshia maji, redio na feni, pasi na draya za kukausha nywele saluni.

Anasema: “Baada ya kutengeneza vinavyofaa, vifaa visivyotengenezeka navikusanya na taka nyingine na kuzitupwa dampo. Sijui kama natakiwa kuzipeleka wapi zaidi ya kuzitupa, nyingine zinaonekana lakini zinahitajika kwa sababu kuna vifaa ninavyoweza kutumia kwenye kazi yangu.”

Kwa mujibu wa Dk. Simba vifaa vya kielektroniki vilivyotumika vinaweza kwa mara nyingine tena kutumiwa, kuuzwa, kuokolewa, kuchakatwa na kutupwa.

JUHUDI ZA TCRA

Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) inayosimamia huduma za mawasiliano inasema kutokana na changamoto hiyo imeweka mikakati ya pamoja ya kuikabili, ni kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari.

Anasema wamekutana wadau mbalimbali wakiwamo watafiti, wataalamu wa mazingira ili kujadili kwa namna gani wanaweza kumaliza tatizo hilo.

Mei mwaka huu, TRCA itaanzisha utaratibu rasmi wa kushughulika na tatizo hilo wakati ambao kampuni binafsi ndizo zinazokusanya na kuziteketeza katika utaratibu bora, anasema na kuongeza kuwa wanashirikiana na nchi wanachama kujadili na kupanga mikakati ya kudhibiti usambaaji kiholela wa e-wastes.

MSIMAMO WA WIZARA

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, akizungumza baada ya kufungua kongamano la wadau wa nchi saba  wanachama wa EACO, kujadili na kuweka mikakati ya kumaliza tatizo hilo, anasema ni kubwa linaloendelea kukua ingawa watu wa kawaida hawaoni kwa haraka kwa sababu hawajui pa kuzipeleka.

“Teknolojia inavyoendelea kukua kwa kasi ndivyo vifaa vinavyoonekana vinaanza kupitwa na wakati na kuwa taka, kwa hiyo tunadhani ni muhimu kukutana pamoja na wadau na kuweka namna bora ya kukabili jambo hili,” anasisitiza Nape na kuongeza kuwa serikali ina wajibu wa kuweka mikakati ya kumaliza changamoto hiyo.

Anasema pamoja na njia zinazotumika nchini kuharibu taka hizo kupitia kampuni binafsi, bado kuna umuhimu wa kupata nyenzo za kulimaliza tatizo hilo.

MIKAKATI YA EACO

Katika kongamano la EACO lililotanguliwa na mingine minne, umeweka mkakati wa miaka mitano wa kupunguza uwapo wa taka zinazotokana na vifaa vya kielektroniki, anasema Dk. Simba, akisema mojawapo ni kuangalia namna ya kushirikisha watu na kampuni zinazozalisha bidhaa za kielektroniki ambazo vifaa vyake vinakuwa taka kwa kuwatengenezea miongozo na majukumu maalum.

"Pia tumekubadiliana kuendelea kutoa taarifa kwa wananchi, nchi za Afrika Mashariki, zina kamati ya taka za kielektroniki, kupitia hao watakuwa na jukumu la kutoa elimu kwa jamii hasa ya nini wanapaswa kufanya kudhibiti madhara yake ambayo ni hatari kama hazitahifadhiwa kikamilifu," anasema.

Anasema wananchi wanapaswa kutambua kuwa taka za kielektroniki si sahihi kukaa nazo nyumbani, hivyo amewataka kuzipeleka kwenye kampuni na watu wanaokusanya vitu vyote vya kielektroniki ambavyo havifanyi kazi.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Khamis Hamza anasema kupitia EACO, TCRA na Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), wamewakutanisha pamoja wadau kwa lengo la kuelimishana juu ya namna bora ya kupunguza na kuondoa taka hizo.

"Kutokana na mikataba mbalimbali ambayo serikali imesaini kudhibiti tulipofikia si pabaya sana kwa maana tumeweka msisitizo katika kuelimisha jamii ili kuzuia uwapo wa taka hizi pia kuwafundisha namna bora za kuzihifadhi," anasema.

ANGALIZO UNEP

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), linasema taka za kielektroniki ni mbaya na hatari kwasababu haziyeyuki na zinachafua mazingira. Hata hivyo, hivi sasa baadhi ya vijana katika nchi mbalimbali ikiwamo Nigeria wameamua kuwa wabunifu na kugeuza taka hizo kuwa mali.

Jiji kuu la kibiashara la Nigeria taka za elektroniki kwa miaka mingi lilikuwa tatizo sugu, leo zimepata thamani kwa kuchakatwa na kuwa na tija kiuchumi.