Ujio wa Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris ni fursa ya Tanzania kushirikiana na Amerika ambayo inaahidi kuwekeza zaidi Afrika, kama kiongozi huyo anavyonukuliwa akianza safari yake Ghana.
Anakaririwa na wana habari akisema Marekani itaongeza uwekezaji barani Afrika na kusaidia kuchochea kukua uchumi.
Kama hivyo ndivyo, ombi la Tanzania ni kupata utaalamu na teknolojia ili iongezee nyuklia kwenye kapu la nishati au gridi ya taifa.
Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri uzalishaji nishati hasa safi ya maji, aidha gesi, makaa ya mawe na mafuta ni chanzo cha kuchafua anga na kuongeza hewa ukaa, kwa hiyo urani ni moja ya chanzo kinachohitajika sasa kuzalisha nishati salama.
Ni wazi bila umeme wa uhakika uchumi, elimu, afya, kilimo, viwanda na hatima ya Afrika haitafanikiwa. Aidha, uhalifu utakuwa mwingi, mitaa isiyowaka taa usiku si salama, hali kadhalika kazi za hospitalini bila umeme mchana na usiku hazifanyikazi.
Ili Tanzania na Afrika isiwe karakana ya ibilisi Amerika isaidie kupata teknolojia ya umeme salama wa nyuklia, utakaotokana na urani inayopatikana kwa wingi Tanzania na hata Niger.
Dokta Kamugisha Byabato mtaalamu wa uhandisi madini na nishati jadidifu (mining engineering and renewable energy), anashauri kwa namna yoyote ile kuanzisha mradi wa umeme wa nyuklia kwa sababu nishati hiyo ndiyo ufunguo wa maendeleo.
Ujio wa Makamu Harris, uwe mwanzo wa kuandaa mipango na mikakati ya kupata nishati salama kwa kuwa ndicho dunia inachohitaji sasa. Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri mataifa yote, bila kujali ni Afrika au Amerika.
Dokta Byabato, anasisitiza kuwa maendeleo ya Ulaya, Marekani na Japan, yamefanikishwa na nishati ya nyuklia tangu miaka ya 1960 na sasa ni zama za kusaidia Afrika kupata nishati hiyo kwenye kapu la umeme kwa vile hakuna anayelenga kurutubisha nyuklia kuzalisha silaha za maangamizi.
Anataja kampuni ya Ufaransa ya AREVA inayochimba urani nchini Niger Afrika Magharibi na uzalishaji wa nishati ya nyuklia, akishauri madini hayo yaisaidie Afrika kuinua uchumi wake kwa vile ikiinuka itasaidia pia kuzalisha bidhaa kama chakula na kupunguza uhaba wa vitu duniani.
“Ni kweli urani inazalisha nishati salama, japo ni madini yenye mionzi mikali na hatari. Kikubwa ni utaalamu na teknolojia ya usalama kwa kila hatua, ili kuepusha athari za mionzi (radioactive materials). Utaalamu na teknolojia vitazuia kuchafua mazingira yetu na kuleta athari, lakini tujaribu pia tupate nguvu kuzalisha umeme huo.”
Mtaalamu huyo anaeleza kuwa nishati ya nyuklia haiathiri jotoanga wala kuongeza joto duniani kama ilivyo umeme wa visukuku (fossils) wa gesi asilia, mafuta na makaa ya mawe.
Anaongeza kuwa japo kuna changamoto kwenye kutunza mabaki ya nyuklia, nchi za Magharibi zinafanya utafiti wa utunzaji wa uchafu utokanao na uzalishaji wa nishati ya nyuklia na kwamba mabaki yote yanatunzwa kwenye matunzo yaliyoandaliwa, hivyo Tanzania na Afrika washirikiane na mataifa yaliyoendelea kupata ufumbuzi wa kuhifadhi taka urani.
Kamishna mstaafu wa Madini , Dk. Peter Kafumu, akizungumzia uwepo wa urani na kama inaweza kutumiwa kuzalisha umeme, anasema inawezekana kwa kutumia utaalamu ili kuepusha athari za mionzi hatari (radio active material).
Anasema urani ipo kwa wingi nchini na sehemu zilipoanza kuchimbwa ni chache ikilinganishwa na kiasi kikubwa ambacho hakijaguswa, mfano inachimbwa Bahi mkoani Dodoma, Manyoni Singida na machimbo ya Mto Mkuju katika wilaya ya Namtumbo mkoa wa Ruvuma.
Tanzania ni tajiri wa urani ipo maeneo mengi kama Mbeya, Njombe, Monduli Arusha, ukanda wa Tabora na Kigoma lakini pia Gallapo mkoani Manyara, anataja mtaalamu huyo mbobezi wa elimu ya miamba –jiolojia, Kuanzia 2024, Tanzania inategemea kuzalisha megawati 2,115 za umeme wa maji kwenye bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, lakini mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuikwamisha ndiyo maana kuna umuhimu wa kuchanganya nyuklia kwenye kapu la taifa la nishati.
Amerika ni mfalme wa nishati hasa jadidifu (renewable) na Tanzania pamoja na Afrika ina utajiri wa jua, hivyo juhudi za uwekezaji wa Amerika na Afrika zilenge sekta ya nishati ya jua.
Majiji ya Dar, Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya na Tanga yanayotarajiwa kuwa makuu na makubwa (megacities), yataimarika kwa kila hali iwapo yataunganishwa na umemejua.
Majengo makubwa, hospitali za kitaifa, rufani na kanda kama Muhimbili, Bugando, Aga Khan, Regence, Dodoma, Benjamin Mkapa lakini pia vyuo vikuu vyote kama UDSM, UDOM, Mkwawa, SUA, Tumaini pamoja na magereza , kambi za majeshi, wizara na hata vituo vya mabasi viunganishwe na umeme jua.
Ifike wakati taa zote za mitaa mijini zijipatie umeme jua kwa vile Tanzania na Afrika zimebarikiwa na jua jingi, karibu kila mkoa una saa takribani 10 za jua kali kila siku achilia mbali upepo ambao ni sehemu ya nishati jadidifu inayopatikana kwa wingi nchini.
Karibu Makamu wa Rais Kamala Harris, Afrika inaposhukuru nchi yako kwa misaada kuanzia ya kiafya kama dawa, kilimo, ufugaji, ujenzi wa miundombinu kupitia taasisi kama USAID, PEPFAR na Millennium Challenge Corporation , ni vyema Marekani irefushe mkono wake na kuisaidia sekta ya nishati ili Afrika isibaki gizani ambako ni karakana ya shetani.










