Siyo matarajio ya wengi kusomesha watoto halafu wawe wazururaji mtaani na kufanya uhalifu.
Ndivyo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, baada ya kuona kuna vitu vinashusha ufaulu inaweka maazimio ya kuvikabili.
Kibiti ni kati ya halmashauri tisa za mkoa wa Pwani, ni moja ya maeneo yanayohitaji jitihada na mikakati zaidi ili kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Katika kikao cha wadau wa elimu kinachofanyika hivi karibuni kwenye Sekondari ya Kibiti, suala la namna ya kukabiliana na mimba za utotoni, utoro na wanafunzi kujishughulisha na biashara wakati wa masomo linapewa nafasi.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Meja Edward Gowele, akiwa mwenyekiti, anaeleza kuwa msingi wa maendeleo popote ni elimu na kwamba kiwango hafifu cha ufaulu kwenye mitihani ya kitaifa kinachangia maendeleo madogo ya kitaaluma.
Anasema Kibiti inahitaji mabadiliko kuanzia kwa wazazi na walezi ili kuwafuatilia kwa karibu watoto wao na kudhibiti utoro unaosababisha wasifanye vizuri darasani.
Anawataka wazazi na walezi kujenga ushirikiano kuwachukulia hatua watoto wanaokutwa kwenye maeneo ya biashara muda wa masomo.
"Tushirikiane kuwafuatilia tunapoona watoto au mtoto anafanya biashara kipindi cha masomo, hata kama siyo mwanao we chukua hatua na mzazi wake akikujia juu tupate hizo taarifa, bila kufanya hivi elimu Kibiti itaendelea kushuka," anaonya Kaimu Mkuu wa Wilaya.
Aidha, anaeleza kuwa ili kudhibiti ongezeko la mimba shuleni ni vema wazazi kutoa ushirikiano kwa wale wanaowaoa na kuwapa mimba wanafunzi.
Kaimu Mkuu wa Wilaya anawageukia pia viongozi wa dini kuzungumzia suala la elimu wakiwa kwenye nyumba za ibada ambapo kwa kufanya hivyo wataleta tija kwa kuhamasisha waamini watoto hadi wazee.
Anasisitiza suala la wazazi na walezi kuona umuhimu wa kuchangia chakula shuleni ili wanafunzi wasome kwa bidii wakiwa wameshiba badala ya ilivyo sasa kwa shule nyingi ambazo hazijawa na utaratibu huo.
"Tuweke kiasi cha fedha kwa ajili ya watoto wetu, kuwanunulia mahitaji ya shule lakini kuchanga fedha za chakula wasisome huku wakiwa na njaa," anasisitiza.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, anaeleza kuwa kikao cha wadau wa elimu kimekuwa kikifanyika kila mwaka lakini bado kuna mambo yanawarudisha nyuma.
Mavura anasema katika kikao cha mwaka huu wamejikita zaidi kwenye vikwazo vya ufaulu, kujiuliza na kujadili kwanini vinaendelea na nini kifanyike kuviondoa.
Anasema serikali inaweka fedha nyingi katika sekta ya elimu hivyo ni jukumu la jamii kuungana kumwondolea vikwazo na kupambania ufaulu wa mwanafunzi ngazi ya msingi na sekondari.
"Tujifikirie zaidi kuendeleza elimu hapa Kibiti kwa kuwashirikisha wadau, ushirikishwaji ni muhimu kwenye maendeleo ya elimu, nataka niache alama katika sekta hii, ufaulu uongezeke na kila mzazi aone umuhimu wa kusomesha mtoto wake," anasema Mavura.
Aidha, anasema wapo baadhi ya wazazi na walezi wanatakiwa kubadilika kwani wakati mwingine serikali inatumia nguvu kuwarudisha wanafunzi shule lakini baada ya muda wanaonekana mitaani kwenye sehemu za biashara muda wa masomo hali hiyo ni kuendelea kuidumaza elimu.
"Tunatumia nguvu kumrejesha mwanafunzi shuleni baada ya siku chache wanarudi kuendelea na biashara, wakikamatwa wazazi ndiyo wanaandamana kwenda kwa Mkuu wa Wilaya kuomba watoto waachiwe huru watarudi shule lakini wanarudi tena kule walikotolewa hapa hatuvuki tunatakiwa kubadilika," anasema.
Ili kukabiliana na njaa kwa wanafunzi Mavura anashauri kila shule kutumia mashamba yake kupanda mihogo na mazao mengine ya chakula.
"Watoto wanatembea umbali mrefu, wakifika shule hakuna chakula kwa hali hii hawawezi kufanya vizuri kwenye mitihani yao, tubadilike tuipe elimu kipaumbele tuungane kukabiliana na njaa kwa watoto wetu wawapo shuleni, jiiulize wewe unaweza kushinda bila kula mchana," anasema.
Katika taarifa yake Ofisa Elimu Sekondari Anna Shitindi, anasema bado kuna kikwazo cha elimu kwa wazazi na walezi kuwashawishi wanafunzi kufanya vibaya kwenye mitihani yao ya shule ya msingi kwa lengo la kukwepa majukumu ya kuwasomesha.
Kukosekana kwa chakula cha mchana nacho kinaelezwa kuwa kunashusha ufaulu, wanafunzi kupata ujauzito na upungufu wa miundombinu.
"Tamaduni zilizopitwa na wakati, kukithiri kwa utoro kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari pamoja na ushirikiano hafifu kutoka kwa wazazi na walezi katika kusimamia maendeleo ya taaluma ni kikwazo cha ufaulu," anasema.
Anasema ipo mikakati ya kukabiliana na vikwazo vya elimu ambayo ni pamoja na kuielimisha jamii umuhimu wa elimu kuwa na uelewa kuwa elimu ni haki ya msingi kwa kila mtoto hivyo waache kuwashawishi kufanya vibaya kwenye mitihani.
Anaeleza kuwa mikakati mingine ni pamoja na kuhamasisha jamii kujitoa katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali kulingana na vipaumbele.
"Katika mikakati yetu pia tumeweka suala la kuhamasisha jamii kuhusiana na umuhimu wa kuchangia chakula ili wanafunzi wapate chakula cha mchana, lakini kuhamasisha shule kulima mbogamboga kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi," anabainisha.
Aidha, anasema idara hiyo inaomba wadau wa elimu kushirikiana katika kudhibiti utoro wa wanafunzi na kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na tamaduni zilizopitwa na wakati.
Hamidu Ungando, Diwani wa Kibiti, anasema sababu zinazochangia ufaulu duni kwenye shule zilizopo katika kata yake ni pamoja na msongamano wa wanafunzi darasani.
Aidha, baadhi ya wanafunzi kutembea umbali mrefu ambao wapo kati yao wanaotembea kilometa tano kila siku na wakifika shule wanachoka na hakuna chakula wala maji.
"Kwa mwaka jana katika kata yangu wanafunzi wa kike 18 walikatisha masomo kwa mimba na watuhumiwa wengi wa mimba zao ni madereva wa bodaboda ambao wamekuwa wakiwapa lifti," anaeleza Ungando.
Ungando pia anaeleza kuwa mwamko wa elimu kwa baadhi ya wazazi na walezi ni kikwazo kwani wanapowapeleka watoto shule hawafuatilii maendeleo yao hata wanapoitwa kwenye vikao hawatokei.
"Mfano hiyo ina wanafunzi zaidi ya 2,000 kikiitishwa kikao wanaweza wakafika wazazi 200 kwa hiyo hata utekelezaji wa maazimio haufanyiki kama inavyotakiwa lakini pia hata wakitakiwa kulipa Sh. 1,000 kwa wiki ili mtoto apate hata uji kwa siku akiwa shule nayo hawatoi kama inavyotakiwa na hivyo watoto wasoma wakiwa na njaa na kuhimiza mabadiliko," anasema.










