Ndivyo mawasiliano kielektroniki yanavyowaachia watu historia

14Feb 2023
Christina Mwakangale
BUKOBA
Nipashe
Ndivyo mawasiliano kielektroniki yanavyowaachia watu historia
  • Ni kuongeza uwajibikaji bila kuwasahau waliotumbuliwa

KUKUA kwa matumizi ya teknolojia ya kidijitali duniani kuanzia miaka ya 2000 hususan kwa nchi zinazoendelea yameleta mafanikio chanya japo si kwa sekta zote na kuchochea uwajibikaji na kuwachukulia walalamikiwa hatua.

Haya yanadhihirika baada ya taarifa za malalamiko kusambaa mitandao na kuwaibua viongozi na mamlaka zinazowasimamia na hata wakati mwingine kuongeza woga wa kufanya vitendo vya uhalifu vikiwamo kudai mlungula hasa barabarani.

Teknolojia ya kidijitali inaipa jamii uwezo wa kufikisha ujumbe na malalamiko moja kwa moja kwa viongozi wa serikali na wa kisiasa kwa kutumia mitandao ya kijamii.

Kasi ni kubwa sasa mawaziri hata viongozi wa mikoa, wilaya na taasisi za umma, kuonekana wakitoa maamuzi ya moja kwa moja, ya papo hapo mara wapatapo taarifa kuwahusu wao imekuwa ni kawaida japo pia kwa kurekodi na kuufahamisha umma.

Mfumo wa kimtandao na idadi ya watumiaji wa intaneti duniani imezidi kuongezeka huku bara la Afrika likishika nafasi ya tatu kwa wingi wa watumiaji, Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya hadi Desemba 2017, imeonyesha kuwa idadi ya watumiaji wa intaneti inaongezeka kufikia watu milioni 23 ambayo ni sawa na asilimia 45 ya Watanzania wote.

Inaongeza kuwa mwaka 2013 wateja walifikia milioni 9.31 sawa na asilimia 21, ikimaanisha kuwa kila mwaka kuna watumiaji wapya na uwanja hupanuka zaidi.

KUWAIBUA VIONGOZI

Matukio kadhaa yaliyojitokeza mapema mwaka huu, mwishoni mwa mwaka jana na hata mwaka 2021, ni dhahiri teknolojia inawafikisha wananchi karibu na viongozi wao.

Mfano, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kakanja wilayani Kyerwa mkoani Kagera anasimamishwa kazi akituhumiwa kuwachapa viboko kikatili wanafunzi wa darasa la nne.

Mkuu wa Mkoa Kagera, Albert Chalamila, anasema hatua hizo zinachukuliwa na uongozi baada ya video inayomwonyesha Mwalimu Mkuu Isaya Emmanuel, akiwapiga viboko watoto wawili, kusambaa mitandaoni.

 “Kama ambavyo tumekuwa tukiona kwenye mitandao ya kijamii imekuwa ikisambaa video hiyo ikimwonyesha mwalimu Isaya, akiwachapa watoto hao huku pembeni wakiwamo walimu wanne wakicheka na kufurahia tukio hilo," anasema Chalamila akiwaeleza wanahabari.

Tukio hilo, lililotokea Januari, mwaka huu siku chache kabla ya kuanza kwa masomo ya mwaka huu, mwalimu huyo anawaadhibu watoto hao kwa kosa la kutofanya kazi ya ziada ‘home work' aliyokuwa amewapa wakati wa likizo.

Mwaka huu unashuhudia video ya watumishi wawili wa afya inayosambaa mitandaoni ikionyesha mabishano kuhusu vipimo vya malaria (MRDT), muuguzi akimlazimisha kijana wa maabara kutumia vipimo hivyo kwa mjamzito na kijana huyo akigoma akichodai kuwa vimekwisha muda wa matumizi.

Taarifa hiyo inayosambaa Januari 5, mwaka huu, inahusu watumishi hao wa zahanati huko Uyui mkoani Tabora, Rose Shirima muuguzi mkunga na James Chuchu mteknolojia wa maabara ambao wanasimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kwa mujibu wa kanuni ya 37 ya utumishi wa umma ya mwaka 2003.

Aidha, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, anaagiza mamlaka kufuatilia suala hilo na kuchukua hatua huku akidai kuwa hakuna vitendanishi vya malaria vilivyoisha muda wa matumizi.

Baada ya kauli hiyo ya Waziri Ummy, Halmashauri ya Wilaya ya Uyui ikatangaza kuwasimamisha kazi watumishi hao wawili taarifa ikitolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Uyui, Dk. Kija Maige.

Mwaka 2021, TAMISEMI inabainisha video inayosambaa mitandaoni ikimwonyesha daktari aliyemshona jeraha mgonjwa na kufumua mshono kwa madai ya kushindwa kulipa gharama.

Likitokea katika kituo cha afya Kerenge kilichoko Tarafa ya Magoma Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, linapata ufafanuzi wa ofisi hiyo, Septemba 4, 2021 baada ya kusambaa kwa video hiyo na kuzua mjadala mtandaoni huku Wizara ya Afya ikitoa tamko na kwamba yeyote mwenye kufahamu eneo hilo kwa kutoa taarifa na kisha kuweka namba ya simu. Taarifa zilifanikisha daktari huyo kusimamishwa kazi.

Licha ya gharama za vifurushi mwishoni mwaka jana kulalamikiwa na wananchi kudai kiwango kikubwa kwa muda mfupi, wengi wao wanajikita mitandaoni kubadilishana taarifa zikiwamo za matukio hayo ambayo yametia fora.

Tanzania imeshika nafasi ya 10 katika orodha ya nchi zenye idadi kubwa za watumiaji wa intaneti Afrika kwa mwaka 2022 kwa mujibu wa taarifa zinazotolewa na Data Reportal.

Na kwamba nchi inayoongoza ni Nigeria ambako kuna wateja milioni 109.2 wa intaneti nchini humo hadi Januari 2022.

Misri ina wateja wa intaneti milioni 75.66 ni ya pili, Afrika Kusini ya tatu ikiwa na watumiaji milioni 41.19 wa intaneti mpaka Januari 2022, ya nne, ni Morocco yenye watumiaji milioni 31.59 wa intaneti hadi mpaka Januari 2022, wakati Ethiopia iliyo na wateja milioni 29.83 wa intaneti mpaka Januari 2022 ni ya tano.