Katika hatua zote kila mtoto, anasoma kupitia utaratibu wa elimu shirikishi inayogusa watoto wenye mahitaji maalumu na wale wenye viungo na utimilifu wa maumbile ili kuhakikisha wote, wanakwenda pamoja kwa mafanikio.
Mratibu wa Mradi wa Shule Bora Mkoa wa Tanga, Thomas Aikaruwa, anabainisha hayo anapozungumza na Nipashe na kusema kuwa mradi huo unalenga kufanikisha kuwa elimu jumuishi inaboreka na kutolewa kwa watoto wote.
Anasema Mradi wa Shule Bora unafanikishwa kwa pamoja baina ya Uingereza kupitia UK AID na Tanzania ukilenga kuunga mkono miradi ya elimu, ukitekelezwa katika mikoa tisa.
Aikaruwa anasema unapokea utaalamu wa kiufundi kutoka Cambridge Education ikishirikiana na mashirika ya ADD International, International Rescue Committee pamoja na Plan International.
Anasema shule bora pia unalenga kuiunga mkono serikali katika kuinua kiwango cha elimu jumuishi pamoja na kuweka mazingira salama ya kujifunzia kwa wanafunzi wote wa kike na wa kiume kuanzia shule ya awali, msingi na mwanzoni mwa sekondari.
Kwa kushirikiana wadau hao mradi huu utafanya maboresho yatakayowezesha kila mtoto kupata msingi mzuri katika elimu yake ya awali, ili kuzitumia fursa kwa kutoa mchango wake katika ukuaji wa nchi na maendeleo yake.
Aidha, Aikaruwa anataja mikoa tisa ambayo ni Dodoma, Katavi, Kigoma, Mara, Pwani, Rukwa, Simiyu, Singida na Tanga kuwa ndiyo wanufaika wa mradi huo.
"Mradi unalenga katika maeneo manne ambayo ni kujifunza kwa watoto wote shuleni, kufundisha ambapo mfuko wa msaada wa UK utaunga mkono na kuimarisha kazi ya ufundishaji."
"Jumuishi pamoja na kujenga mfumo ambao mfuko wa UK AID utaunga mkono serikali na kuimarisha ili kupata au kuwa na thamani ya fedha katika utoaji wa elimu katika ngazi zote kuanzia chini hadi taifani," anasema
Mratibu wa Mradi wa Shule Bora Mkoa wa Tanga.
Hata hivyo, anasema jumuishi ni kipaumbele cha mradi huo ambao utawatupia macho kwa karibu wanafunzi wenye mahitaji maalumu na wale wanaotoka katika mazingira magumu na kuwawezesha kuwa shuleni katika mazingira bora na salama hadi kufikia elimu ya sekondari.
"Hii ni pamoja na kuwashirikisha wazazi, walezi na jumii katika kuboresha usalama wa shule na kuondoa migogoro, kuhakikisha walimu wanazungumzia mambo ya jinsia na upatikanaji wa mahitaji ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu."
"Pia kutayarisha mazingira salama na kuwaunga mkono wasichana kushiriki pamoja na kujadili mambo yanayowahusu, lakini kuwasaidia katika kipindi cha hedhi," anabainisha Aikaruwa.
Aikaruwa anabainisha kwamba shule bora itafanya kazi moja kwa moja na mamlaka za serikali za mikoa na halmashauri pamoja na shule katika mikoa husika yenye changamoto nyingi kama ilivyopendekezwa na kukubalika na serikali katika kuboresha elimu.
Anasema, inakadiriwa kuwa mradi huu utawafikia watoto takribani 4,000,000 kati yao nusu ni wasichana, mabadiliko na ubunifu yataonekana na kutathminiwa katika ngazi za chini ambazo walengwa muhimu watapatikana katika shule zote za msingi zitakazofikiwa.
Aidha, anasema, wakati watoto wengi wakijiunga na kuendelea na masomo, matokeo ya elimu nchini yamekuwa na changamoto nyingi na kwamba ni asilimia nane ya wanafunzi elimu ya msingi ndiyo wanafikia kiwango cha taifa cha kujua kusoma na kuandika, huku asilimia 12 wanafikia kiwango cha taifa cha kuwa na ujuzi wa kujumlisha na kutoa.
"Kwa kiasi fulani, hii inachangiwa na ongezeko la uhitaji wa elimu msingi sambamba na ongezeko la idadi ya watu, kunakosababisha ongezeko la uwiano wa walimu na wanafunzi ambako kwa sasa ni wastani wa wanafunzi 62 kwa kila mwalimu mmoja katika shule za msingi za serikali," anafafanua.
Wizara ya Elimu inaeleza kuwa mradi wa shule bora unalenga matokeo katika ngazi ya kitaifa ambapo utawezaesha kupata msaada wa kiufundi kwa serikali pamoja na utekelezaji wa mradi wa Lipwa kwa Matokeo (EPforR II).
Inafafanua kwamba malengo ya utekelezaji wa kitaifa yanapangwa kwa pamoja kati ya serikali na wafadhili huku utoaji wa fedha ukihusisha malengo yaliyofikiwa.
Kwa ujumla inasisimua mabadiliko ya kimfumo kama yale ya mawazo sawa wa walimu na kugawa vitabu, lakini pia shule bora pia itafadhili matokeo muhimu yatakayotokana na vigezo vilivyothibitishwa kutoka katika mradi wa EPforR ambavyo vitatumika katika kutoa fedha na wafadhili wengine.
Kwa ufadhili wa serikali ya Uingereza, kupitia mfumo wa UK AID, gharama za mradi zitakuwa na bajeti ya Paundi milioni 89, takribani bilioni 271 na utafanya kazi hadi ifikapo mwaka 2027, kwa mujibu wa Wizara ya Elimu.
Ili kufanikisha na kueneza ufahamu wa mradi huo, mafunzo ya shule bora yanatolewa kwa wanahabari takribani 30 na maofisa habari wa halmashauri za wilaya tisa pamoja na maofisa habari mkoa yanafanyika Korogwe na kusimamiwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).










