Waibua vifaa kuboresha oksijeni kunusuru wanaopumulia mashine

14Feb 2023
Christina Mwakangale
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waibua vifaa kuboresha oksijeni kunusuru wanaopumulia mashine
  • Vipo vya kusimamia moyo wa watoto njiti

UBUNIFU wa vitu kuanzia bidhaa na huduma mbalimbali ni miongoni mwa vipaji ambavyo kila binadamu huzaliwa navyo.

Ingawa kazi za ubunifu na ugunduzi zinafanyika, changamoto ni namna ya kuziendeleza, kuzibadili kuwa fursa na kuleta suluhisho kwenye matatizo ya jamii na taifa lenye hazina ya wataalamu hao.

Godfrey Sospeter (22) na Neema James (21), wanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar–Es-Salaam (DIT), kwa nyakati tofauti wanaonyesha namna elimu waliyoipata inavyoendeleza ubunifu na ugunduzi wao kuelekea kupata suluhisho kwenye matatizo ya jamii hasa sekta ya afya.

Kwenye mahojiano na Nipashe hivi karibuni, wanaeleza namna walivyobuni njia ya kuboresha afya kwa kuunda kifaa cha kupima ubora wa oksijeni iliyomo kwenye mitungi inayotumiwa na wagonjwa wenye changamoto za kupumua.

 

KIPIMA OKSIJENI

Godfrey mwanafunzi wa mwaka wa tatu anayesoma shahada ya uhandisi umeme akijiunga na chuo baada ya kumaliza kidato cha sita, alikosoma Fizikia, Kemia na Hisabati.

“Niliyamudu masomo ya sayansi ambayo yanasemekana kuwa magumu. Ninaamini kuwa hakuna kigumu kilichovumbuliwa, kuundwa na mwanadamu nikiwamo mimi.”

“Hivyo fikra ndizo zimenipa mwongozo mpaka hatua niliyopo. Natarajia kuwa kiongozi bora katika kutetea utumiaji wa nishati safi kwa mazingira kwa Tanzania na Afrika,” anasema Godfrey.

“Tulianza na tafiti katika hospitali mbili za wilaya, Kigamboni na Amana, Agosti 2022. Tangu kufanya tafiti mpaka kutengeneza vifaa tumetumia takribani siku 30. Tumefanya kazi zote hizi ndani ya DIT kwenye ‘design studio. Lakini hatujafanikiwa kuvifikisha kwenye hospitali hadi sasa."

Anasema kifaa walichobuni kinaitwa kifuatilia ubora wa oksijeni. Na kwamba kina king’ora kinachotoa sauti endapo kiwango cha oksijeni si kile kinachotakiwa kuwekewa kwa mgonjwa, kulingana na viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO).

Anaeleza kuwa lazima kiwe cha asilimia 91 hadi 99 na si chini ya hapo, anaeleza mbunifu, anayeongeza kuwa walitafiti

na kugundua kuwa kuna vifaa vingi vya kuzalishaji oksijeni lakini havifanyiwi ukarabati au vina hitilafu na kuzalisha hewa iliyo chini ya kiwango cha WHO

Anaeleza kuwa baada ya kutengeneza kifaa hicho, wanaendelea kukifanyia maboresho na kwamba wamebaini kuwa kifaa hicho, hakipo kwenye hospitali nyingi nchini zikiwamo yalikofanyika majaribio licha ya kwamba katika nchi zilizoendelea ni muhimu na hutumiwa kwenye hospitali kuupima ubora wa oksjeni kabla ya kumwekea mgonjwa.

“Tunaona kuwa kinahitajika kifaa cha bei nafuu chenye ubora wa hali ya juu kupima ubora wa kiwango cha oksijeni kwa ajili ya wagonjwa wenye mahitaji hayo,” anaongeza.

Anasema uwepo wake ndani DIT, umemfanya ajifunze mengi na kufanya ubunifu wa kifaa cha kupimia ubora wa oksijeni inayotumiwa na wagonjwa wodini.

Aidha, kifaa hicho kinaweza pia kupima kiwango na ubora wa oksijeni kwenye mtungi, kabla ya kuwekea mgonjwa wodini, lakini hata eneo alipolazwa pia kufahamu ubora wa hewa anayovuta.

Godfrey anasema kitalaamu okisjeni inayotumiwa huzalishwa kwa njia tofauti na kutaja teknolojia ya kuchuja hewa iliyoko kwenye mazingira watu wanayoishi kupata kiwango kinachohitajika.

Anasema hewa ina gesi za nitrojeni, oksijeni, kaboni na hydorojeni na hivyo huchujwa kupata kiwango cha okisjeni anayotumia mgonjwa.

Akizungumzia malighafi zinazotumika kukiunda anasema vinapatikana nchini ambavyo ni plastiki, lakini vifaa kama ‘sensors,’ ving’ora vinavyotoa mlio, ‘displays’ na ‘control unit’ ambayo hufanya maamuzi na kutoa ripoti ya ubora vyote huagizwa nje.

 

WANAPOKWAMA

“Changamoto kubwa iliyopo kwa wabunifu ni kuwezeshwa ili kuendeleza kazi iliyogunduliwa ikamilike na kukidhi viwango,” anasema Godfrey.

 

KIPIMO CHA NJITI

Neema, kama Godfrey amesoma sayansi Fizikia, Jiografia na Hisabati- PGM akisoma shahada ya Electronics na Mawasiliano ya Angani, mwaka wa tatu chuoni DIT.

Anasema amesoma sayansi akitamani kuwa na mchango katika jamii akibuni vifaa kupunguza matatizo kwenye sekta mbalimbali.

 

Neema na wenzake Gilbert Msumba, Nasekile Fungo na Kheri Kajuna, walitembelea

hospitali za Kigamboni na Amana , ziara iliyowawezesha kungundua kifaa cha kufuatilia mapigo ya moyo na joto la mtoto njiti.

“Ni baada ya kutembelea wodi ya uangalizi maalumu ya watoto njiti au ICU ya njiti wenye umri wa siku 0 hadi 28,” anasema Neema.

“Tuligundua kuwa ufuatiliaji au monitoring kwa watoto njiti unafanyika kwa ugumu sana hasa kwa hospitali zilizoko kijijni. Hivyo, ubunifu wetu unaoitwa ‘portable neonatal monitor' ni kifaa kitatumika kufuatilia mapigo hayo ya moyo na joto la mtoto njiti. Ni chepesi, bei nafuu ya Sh. 140,000 na kina mifumo ya ving’ora inayomjulisha muuguzi kumhudumia mtoto na pia kinaweza kuchajiwa na kutumiwa eneo lisilo na umeme,” anasema Neema.

WANAPOSHINDWA

“Changamoto kubwa wabunifu tunayopata kukosa ‘jukwaa la kutuandaa au kutupa mwongozo sahihi wa kufanikisha ubunifu wetu. Lakini, pia wabunifu wengi kukata tamaa mapema wanaposhindwa kuendeleza kazi zao wakikosa uwekezaji,” anasema msomi huyo.

“Ninaamini hiki kifaa kitaboresha afya ya mtoto njiti kwa hatua kubwa kwani kinaweza tumika katika vijiji na pia na Mtanzania yeyote anayehumia motto huyo hata kama hana ujuzi wa hali juu,” anaongeza Neema.