KESHO IKIADHIMISHWA SIKU YA KIFAFA…

09Feb 2023
Christina Mwakangale
DAR ES SALAAM
Nipashe
KESHO IKIADHIMISHWA SIKU YA KIFAFA…
  • Bingwa Mshegenzi: Vyanzo vyake hivi, kuujua ugonjwa maabara kidogo sana

NI darasa la afya linalotaka utulivu. Inaelezwa kwamba, mfumo wa umeme kwenye ubongo wa binadamu, mara tu ukipata tatizo, huwa kuna sababu ambazo, mojawapo ni sehemu inapokatiza mfumo huo, ama pana uvimbe au kovu.

Ajali ya aina yeyote, ikiwamo barabarani, ambazo kwa mtazamo wa nje athari zake hazibainiki moja kwa moja, huweza kuathiri mfumo wa umeme wa ubongo na mawasiliano, kisha mtu anapoteza au kutopoteza fahamu.

Bingwa wa tiba magonjwa ya mfumo wa fahamu, kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila, Dk. Brighton Mshengezi, anafafanua hayo katika mazungumzo na Nipashe, kuhusu kiini cha ugonjwa kifafa.

Maradhi kifafa duniani huadhimishwa kila wiki ya pili ya mwezi Februari. Nchini Tanzania, siku hiyo inatumika kutoa elimu kwa umma, nchini ikiadhimishwa kesho, Ijumaa.

Bingwa huyo anaeleza namna ugonjwa huo ulivyo na tafsiri yake, ikiwa na taswira tofauti na wakati mwingine ili kuubaini hautegemei vipimo vya kisayansi, bali mahojiano binafsi kati ya mgonjwa na mtaalamu tiba.

“Kwa mfano mtu anayeugua malaria, au presha atakuja hapa utamfanyia vipimo, vitakujibu hapo hapo anaumwa. Ila mgonjwa wa kifafa, anaweza kuja na jamaa au mwenyewe na mwonekano wake ni mzima tu.

“Ila pale unapouliza sababu yao kufika hospitali, jamaa atakwambia huyu ndugu yangu huanguka, hupoteza fahamu, mkono au mguu hukakamaa kwa muda fulani, au mgonjwa mwenyewe akasema, hafamu kinachomtokea, ila anasimuliwa,” anasema.

Anaendelea:“Ugonjwa huu naweza kusema unategemea zaidi mazungumzo kwa asilimia 80 na vipimo vitamaliza kiwango, tofauti na mtu mwenye VVU (Virusi Vya Ukimwi), malaria kipimo kitaonyesha moja kwa moja ana maambukizi,” anafafanua.

VYANZO VYAKE

Bingwa huyo Dk. Brighton Mshengezi, anasema, sababu ya kuadhimisha siku hiyo kesho, ni kukuza elimu kwa umma kwamba ni miongoni mwa magonjwa yenye utata.

“Wapo wanaoamini unaambukizwa na mtu anayeugua, wanamtenga, wanasema ukikoholewa na mwenye kifafa umepata, watu wengi hawaendi hospitali wanadai ni kurogwa,” anasema Dk. Mshengezi.

Anafafanua kwamba ugonjwa huo, pia unatambuliwa na wataalamu wa Chama cha Kudhibiti Kifafa Tanzania (TEA), yeye akiwa mwanachama, yapo wanayoyajadili ikiwamo kutafiti na kuja na suluhisho au mapendekezo.

Bingwa Mshengezi anataja sababu mbili zinazojulikana na zisizojulikana, akirejea athari ni kwenye umeme wa ubongo unapopata hitilafu.

Anasema, chanzo kinaweza kuwa kovu kwenye ubongo kusababishwa na ajali kichwani, mtoto aliyevutwa wakati wa kuzaliwa, au uvimbe hasa kwa wanaougua saratani.

“Mtu anaweza kuwa na dalili ya kukakamaa, apoteze fahamu au asipoteze fahamu. Si kifafa chote unapoteza fahamu, mwingine anayeugua anakusimulia mwenyewe ambacho kinamkumba kwa sekunde au dakika chache,” anasema.

INATOKEAJE?

Bingwa huyo anaeleza kwamba mtu anatokewa na maradhi kifafa kazini, akicheza, usingizini na akiamka anajikuta mwili, mgongo, viungo vimechoka, kifafa kilimpitia usingizini na mfumo wa umeme ukikatizwa kila mara na inaweza kuleta kifo.”

“Nilipokuwa nasoma shule ya Jumapili (Sunday School), mtoto mwenzangu tukiwa tunaimba akakaa kimya kwa muda mfupi bila ya kufanya chochote, amezubaa, nilimtania sikujua. Baada ya kuwa ‘neurologist’ (bingwa mishipa ya fahamu) nimebaini mtoto huyu kumbe aliugua,” anaeleza bingwa huyo

Dk. Mshengezi anaeleza kwamba kuna wakati huwa sababu pia maambukizi ya minyoo itokanayo na nyama ya nguruwe, ambayo haikuandaliwa vyema, husababisha tatizo hilo.

Kadhalika, anasema mama anapojifungua mtoto akavutwa kwa kutumia vyuma, mfumo wa umeme unaweza kusumbuliwa na kuwa chanzo cha kifafa wakati akikua au ukubwani.

“Uzuri mtoto akipata uvimbe au tatizo utotoni, linaweza jirekebisha kwa kuwa anakua. Ila tatizo kujitokeza ukubwani  utashangaa mbona hakuumwa akiwa mtoto,” anafafanua.

DEGEDEGE vs KIFAFA

Bingwa huyo anasema jamii imejihusisha sana na kifafa, pia degedege, akitaja baadhi ya viashiria vinafanana, hakuna uhusiano kati yao.

“Degedege ni tukio la mtu hupoteza fahamu awe mtoto au mtu mzima. Lakini, degedege ni tukio litokanalo na sababu, aidha anaumwa, mtu hajala chakula, sukari imeshuka mwilini au mgonjwa wa kisukari kazidisha dawa.

“Watu bado hawaamini kwamba degedege huweza kumpata hata mtu mzima, si mtoto tu. Kifafa ni ugonjwa na degedege ni tukio la sababu fulani, ila hata mtu mwenye kiharusi anaweza kupata degedege,” anafafanua bingwa huyo.

Daktari huyo anaiambia Nipashe kuwa, kifafa hakina umri, yeyote huugua na unatibika baada ya historia ya mgonjwa, kipimo cha MRI kubainisha matokeo sahihi.

“Imebainika kwa asilimia 70 waliotumia dawa kwa ufasaha na kwa kufuata dozi ambayo kwa kawaida ni tiba ya miaka mitatu hupona kabisa. Hiyo asilimia 30 ndio wale wasiofuata masharti. Dawa anazitumia, mgonjwa huenda kuirekebisha mfumo wa umeme kwenye ubongo.

“Ingawa kipimo kikionyesha tiba ifaayo ni upasuaji, hufanyiwa upasuaji wa ubongo ili kuirekebisha, kuondoka sehemu iliyo na hitilafu.

“Ni kama umeme wa nyumbani ikitokea hitilafu umeme utakatika, pia umeme kwenye ubongo usiporekebishwa kuna athari, hata kifo,” anasema bingwa huyo.

ATHARI ZAKE

Dk. Mshengezi anaeleza kuwa zipo athari kama za ajali aina tofauti, mathalan kuathirika na moto jirani au barabarani.

“Kuna mtu utakuta anakuja hapa anasema yeye ni dereva, na udereva ndio kila kitu yaani maisha yake, anaenda safari masafa marefu umpe dawa aendelee na kazi. Ingawa mgonjwa huyo huyo wa kifafa asipopata mapumziko, usingizi wa kutosha ni hatari kwake.

“Kwa kifupi, mtu huyo anajiongezea kupata degedege kwenye kifafa. Mwingine atakwambia, anashangaa alijikuta gari ipo kwenye mtaro, hajui ilikuwaje,” anaeleza, huku akihitimisha kwa takwimu za duniani kwamba, wapo wagonjwa wanaougua kifafa milioni 67.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Top of Form

Bottom of Form

Top of Form

Bottom of Form