Kuna mambo kadhaa yamechukua nafasi tangu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuingia madarakani miaka miwili sasa. Inapoangaliwa undani wake, anajikita kuipa biashara uhai, kutanua wigo mpana wa uzalishaji viwandani na nje ya viwanda, kama vile shambani.
Eneo lingine linalofungua mtazamo ni katika kufungua milango ya kibiashara kimataifa. Katika hilo, Dk. Samia amekuwa akichukua juhudi binafsi kuhamasisha mwenyewe kuinua uhamasishaji, ushuhuda wake ukibebwa na ziara kimataifa.
Kwa sura moja, wapo waliompinga dhidi ya hatua hizo za kusafiri kwamba inaibebesha taifa mzigo mkubwa wa gharama ya matumizi ya umma, hatua ikamlazimu wakati fulani kuitolea ufafanuzi manufaa yake katika mustakabali huo wa gharama kitaifa.
Mara zote kwa asilimia kubwa, serikali inabaki kwenye wajibu wake wa asili kuwa mhamasishaji, mratibu na msimamizi mkuu kisheria katika uendeshaji shughuli za kiuchumi kitaifa, huku wawekezaji binafsi katika ngazi mbalimbali kuanzia juu hadi chini wakulima na wajasiriamali ndio washiriki wakuu.
Hata hivyo, kuna baadhi ya miradi ya kiuchumi na maeneo ya kuhudumia taifa, serikali huwa mshiriki wa moja kwa moja, mathalani Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na Shirika la Reli (TRC) zinamilikiwa, pia kuendeshwa na serikali.
Vivyo hivyo, Rais Dk. Samia kuna wakati ukachukua hatua ya kuhamasisha utalii, akashiriki katika kuandaa sinema ya Royal Tour, iliyomlazimu kusafiri hadi kufika ughaibuni katika nchi mbalimbali kurekodi, sasa mafanikio yake yanashuhudiwa kwa kumiminika watalii nchini.
Hayo yote kiuchumi yana mantiki kadhaa: kuamsha shughuli za kiuchumi na biashara zikapata uhai; kupanua wigo wa ajira za ndani; mzunguko wa fedha na pato la moja kwa moja la serikali, vilevile kutunisha chanzo kikuu cha pato la serikali ambayo ni kodi, kama alivyosisitiza Mwalimu Nyerere na hata watangulizi wengi duniani.
MAKUSANYO YANAENDESHWAJE?
Katika mwenendo huo wa maboresho kuandaa mazingira wezeshi kiuchumi na kibiashara nchini, Rais Dk. Samia, akaelekeza kuwapo mabadiliko makubwa katika mfumo wa ukusanyaji kodi kutoka vyanzo na sekta binafsi, ikiwamo kwa wafanyabiashara.
Moja ya mambo ambayo rais akapiga marufuku, ya kufunga biashara na kuzuia akaunti za wafanyabiashara uliokuwa umetawala na badala yake kukaa meza moja kutafutia majibu namna kodi zinazodaiwa zitawasilishwa.
Katika hilo akalitolea ufafanuzi kwamba, biashara na mifumo husika ya kiuchumi inatakiwa kuachiwa mazingira ya kujiendesha, ili kupata uwezo wa kulipa kodi na daima si kufungiwa.
Ni hali iliyojionyesha mara moja kutoka kwa walipa kodi, huku TRA ikianzisha kampeni rafiki katika ukusanyaji kodi, aina ya hatua inayoendelea hadi sasa.
Mnamo, Januari mwaka huu, TRA ikatangaza mafanikio makubwa kupitia mfumo huo, ikikusanya kupitia kodi jumla ya shilingi trilioni 12.4 katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023, ni sawa na asilimia 99 ya lengo la makusanyo ya Sh12.48 trilioni.
Pia, inaelezwa makusanyo ya mwezi Desemba mwaka jana, ambayo ndio maelekezo ya Rais yamekuwa yakiendelea kufanyiwa kazi, yamevunja rekodi tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo mwaka 1996.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, makusanyo hayo ni ongezeko la shilingi trilioni 1.35, ikilinganishwa na shilingi trilioni 11.11 iliyokusanywa kwa kipindi kama hicho mwaka wa fedha uliopita. Ni taarifa inayotaja kuwapo ongezeko la mapato yakikua kwa asilimia 12.2.
Kwa mujibu wa TRA ni kwamba, katika mwenendo huo wa ulipaji kodi kwa hiari kama ilivyoelekezwa na Rais, pia uhusiano baina ya mamlaka na walipakodi, umeendelea kuimarika kwa kiwango cha kuridhisha.
Katika hilo, TRA kupitia taarifa yake inaendelea kufanyia kazi malekezo na miongozo ya Rais kuhusu namna bora ya kukusanya mapato pasipo kufanyika matumizi ya nguvu na kuendelea kujenga mazingira wezeshi ya uwekezaji na kufanyika biashara nchini.
“Serikali imeendelea kuisaidia Mamlaka katika ujenzi na matumizi ya mifumo inayochangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa ufanisi katika utendaji kazi wetu,” inaeleza mamlaka hiyo, inayoahidi kuboresha huduma kwa walipakodi kwa kuzingatia uadilifu, weledi na uwajibikaji ili kujenga taswira ya kuaminika kijamii
SAFARI YA MAFANIKIO
Mnamo katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba katika mwaka wa fedha, Rais Dk. Samia akiwa hajakamilisha mwaka mmoja katika nafasi ya urais, kukashuhudiwa hatua kubwa ya makusanyo kodi kwa asilimia 98 ya lengo husika, kiasi cha shilingi trilioni 11.11, dhidi ya Sh. trilioni 11.3 zilizolengwa.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, katika kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha 2020/21 zilikusanywa shilingi trilioni 9.24.
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Nyakanazi mkoani Kagera wakati akielekea Mkoani Kigoma leo Jumapili Oktoba 16, 2022.
ATOA ELIMU
Rais Dk. Samia naye hakuwa nyuma katika mizunguko yake kuhamasisha wajibu wa kodi kwa hiari, daima huwaachia umma salamu za wajibu wao katika kulipa kodi kwa hiari, kwani ndio chanzo cha fedha za miradi ya maendeleo kitaifa.
Vilevile akatumia nafasi hiyo, kuwahamasisha viongozi mbalimbali wa serikali, wakiwamo mikoani kuendelea kuuhamasisha umma kuwajibika na ulipaji kodi.
Akiwa ziarani wilayani Biharamulo mkoani Kagera Oktoba mwaka jana, Rais Dk. Samia akawakumbusha wakazi kuwa fedha zinazotangazwa na viongozi kutolewa kwa ajili ya miradi mbalimbali kitaifa, zinatokana na kodi za wananchi.
Rais Dk. Samia ameyasema hayo katika eneo la Nyakanazi wilayani Biharamulo Mkoa wa Kagera akiwa njiani kuelekea mkoani Kigoma, alipokuwa akijibu maswali ya Mbunge wa jimbo hilo.
Huku akiwaonya wanaokaidi kulipa kodi, Rais Dk. Samia anafafanua: “Mkilima vizuri mkauza mazao tunakusanya, mkichimba madini tunakusanya, ukiwa na duka lako ‘kijikodi’ kidogo tunakusanya.”
RC ASHIRIKI
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Yahya Nawanda, baada ya kupokea maelekezo ya rais, viongozi serikalini wakahamasisha ulipaji kodi, Novemba mwaka jana, akawaagiza maofisa TRA mkoani, watoe elimu kwa wafanyabiashara kuhusu ulipaji kodi kwa wakati na hiari.
Akiwa mjini Bariadi, anasema ni lazima maofisa hao wahakikishe wanatengeneza mazingira wezeshi kwa kila mdau alipe kodi.
"Kuweni na lugha nzuri mnapowafuata wateja, wananchi wengi wanahitaji elimu ya mlipa kodi, ili waelewe umuhimu wa kulipa kodi kwa wakati," anasema Nawanda.
KODI ARDHI
Kuhusu kodi ya ardhi nako kumekuwa na kiasi kingi ambacho kimekuwa hakijalipwa, Rais Dk. Samia akatumia nafasi yake kusamehe riba kwa wadai ambao wangekuwa hawajalipa hadi kufika Julai mwaka jana, msamaha huo wa bila riba, umedumu hadi Desemba mwaka jana.
"Wale ambao madeni yao yana miaka mitano kurudi nyuma watalipa bila ile tozo ya riba" akatamka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Dk. Mabula, akiongeza :"Mama Samia ameridhia kupitia Waziri wa Fedha kwa kushirikiana na Waziri wa Ardhi, waweke utaratibu mzuri wa ninyi kuondolewa tozo ile na msamaha ni wa miezi sita tu (hadi Desemba 2022).
“Kama una ndugu mpigie simu mwambie serikali ya awamu ya sita chini ya mama Samia imetoa msamaha kwa wadaiwa sugu ili watoke katika jina baya la wadaiwa sugu kwenda kulipa madeni bila riba."
Wiki hii kupitia uamuzi huo wa Rais Dk. Samia, Serikali imeongeza tena muda wa ulipaji kodi ya pango la ardhi wenye msamaha wa riba hadi kufika Aprili mwaka huu.










