Yanga ndiyo basi tena

20Jan 2016
Lete Raha
Yanga ndiyo basi tena

BAADA ya kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga imewaambia wapinzani kwamba ndiyo basi tena, lori limeshakatika breki.

Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm,kushoto

Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema hataki kushuka tena kileleni hapo kwani amedhamiria kushinda mechi zote zinazofuata.
Yanga itawavaa Majimaji kwenye Uwanja wa Taifa kesho na Mholanzi huyo ametaka mvua ya mabao.
Majimaji ni kati ya timu zilizipokea vipigo vikubwa zaidi msimu kikiwamo cha 6-1 kutoka kwa Simba kwenye Uwanja wa Taifa Oktoba 31 na cha 5-1 dhidi ya Toto Africans Desemba 12 mwaka jana.
“Nimewaandaa vizuri wachezaji wangu, nataka pointi tatu ili niendelee kukaa kileleni mwa Ligi. Nafahamu vizuri nafasi tuliyopo ina ushindani mkubwa, lakini tutahakikisha tunaendelea kuongoza," alisema Pluijm.
Mholanzi huyo alisema pia kwa sasa hana hofu na upigaji penalti kwenye kikosi hicho kwa kuwa majukumu hayo amemuachia beki Kelvin Yondani tangu mwaka jana.
“Hatuna wasiwasi na upigaji wa penalti iwapo zitatokea, zaidi nimepanga kila mchezo timu yangu ishinde. Iwe kwa penalti au kwa kawaida, ushindi lazima kwenye kila mchezo,” alitamba.
Kocha wa Majimaji, Ongala, ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Yanga na kocha msaidizi wa zamani wa Azam, huo utakuwa mchezo wake wa pili tangu apewe timu hiyo, baada ya mwishoni mwa wiki kupata sare ya ugenini ya 1-1 dhidi ya Coastal kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Yanga ambayo haikucheza soka ya kuvutia katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Ndanda mwishoni mwa wiki, itakutana na majaribu ya wachezaji wake wa zamani kesho, beki Lulanga Mapunda na mshambuliaji Danny Mrwanda ambao wapo Majimaji kwa sasa.
Yanga inaongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 36 zinazolingana na Azam iliyopo kwenye nafasi ya pili, wakati Simba inafuatia ikiwa na pointi 30 kwenye nafasi ya tatu.

Azam v Mgambo JKT
Azam baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya vibonde African Sports kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam wanasafiri hadi Tanga kuwafuata Mgambo JKT.
Mchezo huo unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua utafanyika leo kwenye Uwanja wa Mkwakwani na Azam watahitaji ushindi ili kuendelea ‘kula sahani moja’ na Yanga katika mbio za ubingwa.
Azam ambayo haijaweza kufanya vizuri msimu huu itakuwa na kibarua kigumu mbele ya Mgambo ambayo wikiendi iliyopita iliichakaza JKT Ruvu kwa mabao 5-1.

Simba vs JKT Ruvu
Simba wao watakuwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo kumenyana na JKT Ruvu katika mchezo ambao utawakutanisha makocha wa zamani wa Kagera Sugar, Abdallah Athumani na Mganda Jackson Mayanja.
Kibadeni, kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, kwa sasa anaiongoza JKT Ruvu iliyofungwa 5-1 dhidi ya Mgambo JKT wikiendi iliyopita, wakati Mayanja atakuwa kwenye mchezo wa pili tangu arithi mikoba ya Muingereza, Dylan Kerr, Simba. Mayanja aliiongoza vyema Simba katika mchezo uliopita kwa kuifunga Mtibwa bao 1-0. Hata hivyo, huenda Simba ikamkosa straika, Ibrahim Ajib aliyeumia Jumamosi dhidi ya Mtibwa.
Mayanja amesema, “Leo nina kibarua cha pili dhidi ya Kagera, naamini nitafanya vizuri kwakuwa nimekuwa nikikitengeneza kikosi changu kwa kuwajengea wachezaji wangu stamina na uwezo wa kupambana kwa dakika 90. Naamini tutaibuka na ushindi mkubwa."
Naye kocha Kibadeni alisema, “Tunahitaji pointi tatu, haitakuwa kazi rahisi lakini tumeshajiandaa na Simba na naamini tutaweza kuishinda."

Mechi nyingine leo
Mechi nyingine za Ligi Kuu kesho ni kati ya Ndanda na Mbeya City Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Prisons dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Stand United na Toto Africans Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Mechi za Kesho
Mechi nyingine za Ligi Kuu zitakazopigwa kesho mbali na ule wa Yanga ni kati ya Mwadui na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga na African Sports wataikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kocha wa Yanga,
inatarajiwa kuendelea leo na kesho, huku mvutano mkubwa zaidi ukiwa kwenye mechi za miamba watatu wanaofukuzana kileleni; Azam, Simba na Yanga.