UKISIKIA PAAAH NI OKWI SIMBA

18Sep 2017
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
UKISIKIA PAAAH NI OKWI SIMBA
  • ***Omog afunguka kifo cha Mwadui Uhuru

UKISIKIA PAAAH! Basi tambua ni kishindo cha mshambuliaji wa Simba, Mganda Emmanuel Okwi, kushusha kipigo kwa timu penzani Ligi Kuu Tanzania Bara!

Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya jana straika huyo kurejesha furaha ya ushindi Msimbazi wakati wakiibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mwadui FC.

Simba ilikosa huduma ya Okwi katika mechi ya mzunguko wa pili dhidi ya Azam FC kufuatia kuchelewa kujiunga na wenzake katika maandalizi ya mchezo huo akitokea kwenye majukumu ya timu yake ya Taifa, hivyo kujikuta ikilazimisha sare tasa katika Uwanja wa Chamanzi jijini Dar es Salaam.

Lakini kurejea kwa Okwi jana katika mechi hiyo ya Ligi Kuu raundi ya tatu dhidi ya Mwadui FC, kumerejesha kasi ya Simba iliyoanza nayo ligi kwa kuichapa Ruvu Shooting mabao 7-0.

Baada ya Okwi katika mechi hiyo ya ufunguzi kutupia mabao manne, jana aliendelea kujiimarisha kileleni mwa orodha ya wafungaji bora Ligi Kuu msimu wa 2017/18 baada ya kutupia mabao mawili katika ushindi wa 3-0 walioupata dhidi ya Mwadui FC huku John Bocco 'Adebayor' naye akifungua rasmi akaunti yake ya mabao Ligi Kuu msimu huu baada ya kutupia moja.
Mabao hayo mawili yamemfanya Okwi kufikisha mabao sita katika michezo miwili aliyocheza.

Okwi alifunga bao la kwanza kwa Simba katika dakika ya saba ya mchezo kwa shuti lililombabatiza beki wa Mwadui na kutinga wavuni.

Simba iliendelea kulisakama lango la wapinzania wao, lakini mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika matokeo yalisoma 1-0.
Kipindi cha pili Simba waliendelea kulisakama lango la Mwadui na dakika 68, Okwi aliwainua tena mashabiki kwa kufunga bao la pili.

Pamoja na Mwadui kuonekana kujikakamua kuwabana Simba, Bocco aliipatia Simba bao la tatu dakika ya 73 hilo likiwa lake la kwanza tangu kuanza ligi.

Kocha wa Simba, Joseph Omog, akizungumza baada ya mchezo huo alisema wachezaji wake, walifuata maelelezo yake na kufanikiwa kupata ushindi.

"Nashukuru kwa ushindi, wachezaji, wangu walipambana na walifuata maelekezo, tunaenda kujipanga kwa mchezo ujao," alisema Omog.

Baada ya mchezo wa jana, Simba itasafiri Alhamisi kwenda Kanda ya Ziwa kucheza michezo miwili Shinyanga na Bukoba.
Matokeo ya jana yameifanya Simba kufikisha pointi saba na mabao 10 huku ikiwa haijaruhusu nyavu zake kuchanwa.