Baada ya kuchambua na kutafakari leo sitaki longolongo wala mizungusho bali kusema kwa kinywa kipana tena kwa herufi kubwa kuwa kaya yetu inahitaji katiba mpya ili kufanya mambo kisasa na si kizamani kama ilivyo na ilivyozoeleka.
Hebu msomaji tuseme pamoja kwa herufi kubwa “TUNATAKA KATIBA MPYA ILI TUFANYE MAMBO MAPYA”
Naona yule anagwaya akidhani yatanikuta yanayowakuta akina Tunduni . Ogopa Mungu si wengine. Wanaweza kufunga mwili wako lakini si mdomo wako wala mawazo yako. Kwani kaya hii ni yao au mama zao? Hebu tusema pamoja “tunataka katiba mpya sasa vinginevyo hapakaliki hapa.”
Kuna maswali ya kujiuliza. Je ilikuwaje mwana wa mfalme akanyang’anywa tonge mdomoni wakati alikuwa na kila zana za kuchakachua? Si baada ya kustukia mchezo wa uchakachuaji, mpinzani wake Jadwong Madwong ambaye by extension ni rafiki yangu na dingi, akaenda kwa Pilato.
Kwa vile katiba ya kule inaruhusu kila mlevi kwenda kwa Pilato anapohisi hajatendewa haki si Pilato akampa alichotaka kwa kumpiga chini mwana wa mfalme. Just imagine. Unadhani ingekuwa Bongolalaland na katiba yetu viraka jamaa Ufreedom angetoboa kama wasemavyo huko? Wala.
Kwa vile nimependa chesi hii, nawaalika walevi wote wapenda demokrasia bila ghasia na maendeleo vya kweli waje tupange namna ya kuwabana wanene wetu warejeshe k atiba yetu mpya ya jaji Jose Waryuba iliyouawa mafisadi I wa kisiasa.
Au vipi walevi? Semeni kwa pamoja ‘Tumechoka na longolongo, ubabaishaji na mauaji ya katiba mpya ya kaya.” Sema tena “Tunataka katiba mpya na si uongo mpya.”
Ninapoandika hapa, dingi atakuwa akitabasamu kwa swahiba yake kupata fursa nyingine ya kujaribu urahisi huku ndugu yangu Eddie aliyeshabikia upande wa pili akiugulia kwa machungu ya hukumu hii takatifu.
Tukirejea umuhimu na majaliwa ya katiba mpya, lazima niseme bila kumung’unya kuwa huwezi kuendeleza kaya bila kuwa na haki na uhuru kwa wanakaya kama ilivyo sasa. Hivyo basi, wote wanoota ndoto za nchana kuwa kaya inaweza kuendelea kwa maigizo wanapoteza muda.
Maana, Katiba mpya ndiyo muarobaini wa ufisadi, uvivu na ubabaishaji ambavyo dingi amejaribu kutumbua akaishia kuchoka kabla hata hajamaliza ngwe moja.
Hata hivyo, amejitahidi, hakuna jambo la maana angewatendea walevi kama kufufua nchakato wa katiba mpya ili itumike kuleta usawa, haki na uwajibikaji kayani kama ilivyotokea kwa majirani zetu wa the country of man eat man hivi karibuni.
Huwezi kuendeleza kaya wakati kuna matabaka ya walevi ambao wapo wasioguswa na wanaotolewa kafara kwa sababu wanaeleza mawazo yao ambayo ni haki yao kikatiba. Huwezi kuendeleza kaya kwa katiba viraka na makengeza kiutendaji ambapo baadhi ya wahalifu wanakingiwa kifua kutokana na ukaribu wao kwa wakubwa au ukubwa wa vyeo walivyoshika au kushikwa na maswahiba au waramba viatu wao kama ilivyo.
Leo sichongi sana. Nakwenda kujiandaa kulianzisha la kudai upya katiba mpya. Kusema ukweli natamani David Maraga , Jaji Mkuu wa Kenya, angekuwa Bongo lau tumpe ofa na kumpongeza. Kwa wale wanaoatamia katiba yetu mpya wakae wakijua kuwa wanakalia kaa la moto. Kumbe naota! Hata hivyo, tuseme "tunataka katiba mpya."










