Simba yarudia makosa ya 2015

06Jan 2016
Nipashe
Simba yarudia makosa ya 2015

Mashabiki wa Simba wamesikitishwa na sare ya 2-2 ambayo timu yao iliipata dhidi ya Jamhuri FC ya Pemba kwenye Uwanja wa Amaan juzi usiku? Wakumbuke timu yao ilianza kwa kipigo dhidi ya Mtibwa Sugar mwaka jana, lakini ikatwaa ubingwa!

Kikosi cha simba

Ikiwa Kundi C pamoja na timu za Mtibwa, JKU na Mafunzo, Simba iliianza michuano ya Kombe la Mapinduzi 2015 kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya mabingwa wa 1999 na 2000 wa Tanzania Bara, Mtibwa Sugar, lakini ikabadili upepo kwenye michezo iliyofuata ikiwamo kuitungua Mtibwa kwa matuta 4-3 siku ya fainali.

Juzi Muingereza Dylan Kerr alianza na kikosi cha wachezaji ambao hawakupata nafasi ya kucheza dakika zote 90 katika mechi zote 13 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu, na kujikuta akikumbana na upinzani mkali kutoka kwa Jamhuri FC.

Matokeo ya sare ya 2-2 yameiweka Simba katika nafasi ngumu ya kutinga kwenye hatua inayofuata ya Nusu-Fainali ya michuano hiyo kutokanana na URA kuanza na ushindi wa 3-1 dhidi ya JKU ya Zanzibar juzi. Kikosi cha kitalazimika kusaka ushindi dhidi ya timu hiyo ya Ligi Kuu ya Uganda ili kuweka hai matumaini ya kutetea ubingwa.

Kiungo Mzanzibar, Awadh Juma Issa alitupia goli moja kila kipindi huku Mwalim Khalfan Mohammed na Ammy Khamis Baghaseka wakiifungia Jamhuri katika dakika za 16 na 53.

Awadh alianza kuwafurahisha Simba katika dakika ya 12, akiwatoka mabeki wa Jamhuri na kuachia shuti la mguu wa kulia nje ya boksi baada ya kupewa pasi na Mussa Hassan 'Mgosi' aliyekuwa katatikati ya Uwanja wa Amaan kabla ya kiungo huyo kurejea tena nyavuni akiitendea haki krosi kali ya mtokea benchini Emery Nimubona dakika ya dakika 14 kabla ya kipenga cha mwisho cha refa Rashid Farahan.