Huku akiwa na pointi tatu baada ya kushinda 3-0 katika mechi ya kwanza dhidi ya Mafunzo FC juzi, kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, aliiambia Nipashe visiwani hapa jana asubuhi kuwa anatarajiwa kupata upinzani mkali kutoka kwa kikosi cha Muingereza Stewart Hall ambacho kiliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar juzi.
"Itakuwa mechi ngumu, tuko kwenye kundi gumu pia, hilo liko wazi. Timu yangu itaendelea kupambana kwa sababu haikuja Zanzibar kufanya utalii, tumekuja kusaka ushindi katika kila mchezo. Ninategemea (Thabani) Kamusoko atakuwa bora zaidi kesho (leo)," alisema Pluijm.
"Timu inaonyesha ubora wake kulingana na mpinzani unayecheza naye, tutakuwa tofauti kesho (leo) ili kusaka ushindi," aliongeza kocha huyo.
Kwa upande Hall, alisema atashusha kikosi kamili leo dhidi ya Yanga kwa sababu anafahamu ubora wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
"Sitachezesha timu iliyocheza jana (jana), nitashusha kikosi kamili, Yanga ni timu ngumu, nitaanza na kikosi imara kwa ajili ya kusaka ushindi na heshima, hata wao wanalijua hilo," alisema.
Yanga iliyotwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2007, inaongoza Kundi B ikifuatwa na Azam FC na Mtibwa Sugar kila mmoja akiwa na pointi moja huku Mafunzo fc inayonolewa na Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Hemed Morocco, ikishika mkia wa kundi hilo.
Mechi ya Yanga dhidi ya Azam itatanguliwa na mechi ya Mafunzo dhidi ya Mtibwa Sugar itakayoanzasaa 10:15 jioni.










