Mbali na nyumba za wanasoka hao, pia msanii mahiri wa vichekesho, Bambo naye ni miongoni mastaa ambao nyumba zao zinapaswa kubomolewa kwa kujenga maeneo hatarishi.
Wachezaji ambao nyumba zao zimewekwa X ni pamoja na Dua Said, Sanifu Lazaro, Peter Manyika, Shaban Ramadhan na Mtwa Kiwhelo.
Akizungumza kwa uchungu na NIPASHE jana, Dua -- mchezaji wa zamani Simba, alisema Serikali haijawatendea kubomoa nyumba zao kwa vile wamekuwa eneo hilo kwa zaidi ya miaka 23 sasa.
"Haki hakuna hapa," alisema Dua. "Niko hapa kwa zaidi ya miaka 23 na kwa kipindi chote nimekuwa nikilipa kodi ya majengo kwa mujibu wa sheria. Sasa leo iweje tubomoe kwa madai ya kujenga eneo hatarishi?," alihoji mshambuliaji huyo wa zamani Taifa Stars.
Alisema eneo analoishi pia ni makazi ya wanasoka wenzake, Manyika, Ramadhan na Kiwhelo.
"Niko na wenzangu, hatuamini kinachotokea mbele yetu, nyumba tulizojenga na kuishi kwa miaka mingi tunatakiwa kubomoa," alisema Dua wakati akizungumza kwa simu na Nipashe.
Alisema madai kwamba nyumba hizo zinapaswa kubomolewa kutokana na kujengwa sehemu hatarishi, hayana ukweli.
"Kuna watu (wawekezaji) walikuja miaka kama miwili iliyopita wakitaka tuwauzie eneo hili tunaloishi, lakini wakazi wa hapa waligoma kutokana na pesa ndogo," aliongeza.
"Wawekezaji hao wametuzunguka baada ya kugoma kuwauzia na kwenda Serikalini na leo tunaambiwa tuhame."
Kwa upande ake, Dickson Makwaya, maarufu kama 'Bambo' anayeishi Kigogo Darajani, alisema nyumba yake ilipigwa X juzi na kutakiwa kubomoa kabla ya mamlaka husika hajafanya ubomoaji.
Akizungumza na Nipashe jana, Bambo alisema alijibana kwa miaka mingi kujenga nyumba hiyo eneo la Kigogo Sambusa, lakini anasikitika kwani ndani ya dakika tano itakuwa imeshuka chini yote.
"Nina watoto wananitegemea, napaswa kuwalipia ada na mambo mengine mengi, sasa leo nitawapeleka wapi baada ya nyumba yangu kubomolewa?" alihoji Bambo.
"Hapa napozungumza na wewe ndiyo nafanya kazi ya kuhamisha vitu vyangu," alisema Bambo wakati akizungumza kwa simu na Nipashe.
Katika hatua nyingine, Klabu ya Yanga imesema inastahili kulipwa gharama za kubomolewa ukuta wake kama ilivyoagizwa na mamlaka husika.
Klabu hiyo ya Mtaa wa Jangwani ilipewa hadi jana iwe imebomoa ukata wake wa Uwanja wa Kaunda, kinyume chake nguvu itatumika kutekeleza agizo hilo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Yanga Jonas Tiboroha alisema hawapingi agizo hilo na hawana wasiwasi kwani wana hati ya umiliki waliyoipata tangu mwaka 1973.
"Tumepeleka maombi yetu kwa wataalamu wa kutathmini wa majengo ili kujua tunastahili kulipwa kiasi gani kwa kubomoa ukuta wetu. Tuko hapa kihalali, hivyo tunastahili kulipwa," alisema
Aprili 5, mwaka 2011, aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka alisema maeneo yote yanayopitiwa na Bonde la Msimbazi kuanzia Daraja la Salender, Muhimbili, Jangwani hadi Vingunguti hayapaswi kujengwa mradi wowote, huku akiwataka watu wote waliokuwa wamejenga katika maeneo hayo kuondoka.









