Mwaka huu kauli mbiu inakumbusha ushirikiano na wanaume na wavulana kubadilisha mifumo ya kijamii na jinsia ili kutokomeza ukeketaji.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) zaidi ya wanawake na wasichana milioni 200 wamefanyiwa ukeketaji jambo ambalo halikubaliki kwa kuwa ni kinyume na haki za binadamu.
Ingawa kumefanyika juhudi kubwa kupunguza ukatili huo, bado inakadiriwa wasichana na wanawake 3,000,000 wako katika hatari ya kukeketwa kila mwaka na Tanzania imo kwenye hatari.
Kwa mujibu wa utafiti wa Kidemografia na Afya Tanzania wa mwaka 2015/16 Manyara ndio mkoa unaoongoza kwa ukeketaji nchini kwa asilimia 58 ikifuatiwa na Arusha yenye asilimia 47 na Mara 41.
Aidha, utafiti huo pia unaonyesha kuwa mwanamke mmoja kati ya 10 nchini amekeketwa ukiongezeka kulingana na umri. Asilimia 19 ya wanawake wenye umri wa miaka kati ya 45 hadi 49 walikuwa wamekeketwa ukilinganisha na asilimia 5 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 19.
Utafiti huo unadhihirisha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kutokomeza vitendo hivyo ikiwamo kuwekeza zaidi kwenye elimu kwa kuwa unaonyesha wanawake wenye elimu ya sekondari wana uelewa mkubwa zaidi kuhusu athari za ukatili kwa asilimia 97 ukilinganisha na wanawake ambao hawakufikia ngazi ya elimu ya sekondari kwa asilimia 71.
Kwa mantiki hiyo kuna haja ya serikali pamoja na wadau wa haki za wanawake na binadamu kwa ujumla kuangalia ni wapi wamekosea katika suala zima la kutoa elimu kwa jamii kwa kuwa linaonekana bado halijazaa matunda.
Katika maadhimisho ya siku hiyo WHO inatoa rai kwa wadau wanaohusika katika kukomesha ukeketaji kusherehekea mafanikio, kutetea kuachana na mila na desturi hiyo na kuongeza uelewa.
Kuna haja ya kutoa elimu kwenye jamii zinazoshamiri vitendo hivyo, ili wazitambue mila na desturi mbaya zinazochangia kuwapo kwa vitendo hivyo kwa kuwa ukeketaji kwa baadhi ya makabila ni sehemu ya utamaduni hivyo si rahisi kuumaliza bila jamii yenyewe kwa hiyari yao kuamua kuachana nao.
Lakini kuwaelimisha wale ambao wamepitia kadhia hiyo ili wawe mstari wa mbele kukemea kwa kuelezea madhara wanayoyapata baada ya kufanyiwa ukatili huo kwa kuwa ripoti inaonyesha asilimia 86 ya wanawake waliokeketwa hawakubaliani na kitendo hicho na wanatamani kisiwepo kabisa.
Kuna haja ya kuongeza nguvu katika kuwasaka na kuwaelimisha mangariba ambao kuwapo kwao kunashawishi kuendelea kushamiri kwa vitendo hivyo, wapewe elimu pamoja na kuwawezesha kiuchumi ili waachane na vitendo hivyo.
Vilevile kuna haja ya serikali kuyaunga mkono mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi kubwa ya kukemea vitendo ili kuwaongezea nguvu ya kupambana kwa kuwa peke yao hawawezi, watu hawa wanafika maeneo ambayo wakati mwingine serikali haiwezi kufika.
Pia kuwapo na sheria kali inayojitegemea inayokemea vitendo vya ukeketaji ili kuongeza uzito katika suala hilo kwa kuwa inaonekana kuwa sheria zilizopo misumeno yake sio mikali sana ndio maana vitendo vinaendelea kufanyika licha ya maonyo ya serikali.
Moja ya madhara wanayopata wanawake waliokeketwa ni vifo vinavyotokana na kutokwa na damu muda mrefu, maambukizi, maumivu ya muda mrefu, huzuni na utasa.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








