Hata hivyo, muda wa mkataba uliongezwa hadi kufikia Aprili 2022, ili ujenzi uwe umekamilika, lakini hadi kufika Januari mwaka huu, mkandarasi bado alikuwa anaendelea na ujenzi.
Nadhani, tunaendelea kuchelewa. Ukamilishaji wa mradi huo unaweza kuchangia kukwamisha shughuli za kiuchumi za Musoma Vijijini, zikiwamo biashara zao maarufu samaki, madini na mazao ya biashara.
Kama kipande cha kilomita tano kimejengwa kwa miaka hiyo yote na bado hakijakamilika. Najiuliza je, hizo kilomita 92 zitachukua miaka mingapi kukamilika?
Ni vyema sasa, ujenzi huo ukafuatiliwa ili kujua tatizo liko wapi. Pamoja na kwamba, kilomita tano ni ndogo, lakini zinasaidia kupunguza kero ya barabarani, hasa wakati wa mvua ikiwawezesha wananchi kusafirisha mazao yao kirahisi.
Kuchelewa kukamilishwa kipande hicho kilomita chache, kunaashiria rehani ya hizo kilomita nyingine 87 zilizobaki kwenye mradi, pale ujenzi awamu ya pili utakapoanza.
Niseme, kiuchumi eneo hilo linapaswa kutazamwa kwa jicho la ziada, kuhakikisha barabara inajengwa yote kwa kiwango cha lami, tena kwa wakati, ili wananchi wanufaike ipasavyo.
Mnamo Machi Mosi mwaka jana, Wajumbe wa Bodi ya Barabara Mkoa waliutembelea mradi huo, mkuu wa kampuni inayojenga barabara, akajitetea kwa ufafanuzi mradi huo unatekelezwa kwa kasi.
Akawaambia wajumbe hao kuwa, ili kuhakikisha mradi unakamilika, yapo mambo kadhaa yaliyofanywa na kampuni yake, ikiwamo kufunga mtambo wa kusaga kokoto wenye uwezo wa kusaga tani 200 kwa saa.
Pia, akataja mambo mengi waliyokuwa wameyafanya kuwa ni ujenzi wa tuta lenye ujazo wa mita za ujazo 430,000, kusambaza tabaka la kwanza kisha la pili ili baadaye kuwekwa lami na kuahidi kazi ingekamilika ndani ya siku 60 zilizobakia.
Pia, akataja sababu zinazoufanya mradi kutekelezwa kwa kasi ndogo, ni kutopatikana fedha, mkataba wa kazi, huku akifafanua kuwa utekelezaji wa mradi ni wa kuridhisha kulingana na hali halisi, ingawa hakutoa ufafanuzi zaidi.
Maelezo hayo yalimfanya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara wakati huo, Ally Hapi, kumuagiza mkandarasi huyo kumaliza mradi kwa wakati, akikumbusha asimame kwenye takwa la mkataba wake.
Pamoja na kutumia miaka hiyo yote bila kukamilika, kuna malalamiko kutoka kwetu wakazi wa vijiji jirani kama vya Kusenyi na Suguti.
Binafsi nahisi dalili za ufanisi kwenye mradi huo wa barabara ya lami kusuasua njia panda, nikilalamikia uende kwa ufansi wa kimkataba, kwa wakati na hata ubora. Ni ushauri, wenye mamlaka kutafutia majibu sahihi.
Sisi wakazi tunaamini hilo la kutokamilika barabara, haliishii tu katika kutukwamisha kihuduma, bali inagusa maisha yetu kwa undani na ndiyo maana tunaona haja kwa wataalam wa mradi huo kuwajibika zaidi na uongozi wao hata mradi uwe na tija, pia manufaa kwetu sote na ndiyo inavyojengwa.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







