Mara nyingi kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa wakulima wakiwatuhumu wafugaji kwa kuingiza mifugo kwenye mashamba yao hali ambayo hupelekea kuzuka kwa mtafaruku mkubwa dhidi yao.
Inaporejewa, matukio ya kikatili miezi mitatu iliyopita huko Mkoani Pwani Wilaya ya Kibaha kulitokea tukio la kijana aliye shambuliwa hadi kuvunjwa mkono na wafugaji wa jamii ya kisukuma wakati alipokuwa akijaribu kuwazuia wasiingize mifugo kwenye shamba lake.
Hata hivyo, polisi mkoani humo ilichukua hatua ya kudhibiti ikiwa ni pamoja na kuwahamisha wafugaji waliokuwa karibu na mashamba ya wakulima.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo kupitia sakata hilo, akaagiza mtuhumiwa aliyetenda kosa hilo akamatwe na afikishwe kituo cha polisi kwa ajili ya hatua za kisheria.
"Kwenye kupambana na hali hiyo, tulishafika mpaka sehemu yenye migogoro, tukaamuru wafugaji waondoke eneo lile kwa sababu licha ya mifugo kuharibu mazao ya wakulima lakini bado ilikuwa inachangia kuharibu miundombinu na vyanzo vya maji" alisema.
Licha ya kuwapo kwa malalamiko hayo, bado kumeendelea kuripotiwa kwa matukio ya kinyama wanayofanyiana makundi hayo, hapo ndipo dhana ya kuwekeza nguvu kwenye utatuzi wa madhila hayo inapohitajika.
Mnamo Februari 2 mwaka huu, gazeti hili liliripoti wafugaji walivyouwa maofisa misitu kwa kutumia panga na shoka, kwenye msitu wa hifadhi ya kijiji cha Chakulu na Ilunde wilayani Uvinza, mkoani Kigoma.
Ni kitendo kilicholaaniwa vikali na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kupitia Mkurugenzi wake Ana Henga, akiitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhakikisha waliohusika na kutenda kosa hilo wanachukuliwa hatua za kisheria.
Ni hali inayotishia amani kutokana na muendelezo wa matukio hayo, ambayo wafugaji wamekuwa wakiyafanya pale wanapohitaji sehemu za malisho kinguvu, ipo haja ya mamlaka husika kukaa chini na kutafakari kwa kina lini migogoro kati ya wafugaji na wakulima itafikia ukomo.
Kama imefikia hatua hadi askari anauliwa vipi kwa raia wa kawaida? Ni dhahiri kuna kitu hakipo sawa kati ya wafugaji na wakulima, jambo linalohitaji utatuzi wa kina.
Undani wa hilo kama Nipashe ilivyothubutu kudodosa, unaonyesha kuna wakati wafugaji wanakuwa wakorofi kwa wakulima, lakini wakati mwingine wakulima wanakuwa wakorofi kwa wafugaji. Hiyo mara huishia na sintofahamu kati ya sehemu ya malisho na kilimo.
Mkulima mwingine wa mahindi kijijini Msagali, katika wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma, akasema mara nyingi hulazimika kulala shambani kulinda mifugo kama Ng’ombe na Mbuzi, isiingie shambani kula mazao.
"Ninalala shambani kwa sababu, nisipofanya hivyo wafugaji wanaweza kuingiza mifugo yao, nikakosa chochote kama ilivyokuwa mwaka jana.
"Mwaka jana niliikuta mifugo imetawala shamba langu ikabidi niwatafute wahusika lakini nilipowapata walikuwa wabishi kulipa mpaka kesi ilipofika mahakamani" Kibago anasimulia kilichomsibu.
Pia, mkulima wa mkoani Iringa, wilaya ya Kilolo, katika kata ya Nyanzwa, naye ana kilio sawa na mtangulizi wake, akiiomba serikali kuangalia namna ya kumaliza migogoro ya kila siku kati ya wafugaji na wakulima.
"Watu wanapigana, wanapeana ulemavu wa kudumu, wengine wanakufa kisa migogoro ya wafugaji na wakulima, hili si jambo la kufumbiwa macho, watu wanapoteza maisha" analalamika.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








