Mashabiki wa timu hiyo walijazana kwenye uwanja huo, ambapo walikuwa wakibebwa na kaulimbiu ya 'Kwa Mkapa Hatoki Mtu.'
Ni kweli, Simba imekuwa ikiutumia vema uwanja huo kwenye michezo mbalimbali ya kimataifa, hasa mechi ngumu, lakini imekuwa ikifungwa mara chache.
Kwenye mechi dhidi ya Raja Casablanca ilionekana ni mfupa mgumu kwa Simba, si kwa sababu wachezaji wao hawakucheza vema, lakini kiwango kikubwa kilichoonyeshwa na wageni, kilionyesha utofauti kati ya viwango vya wachezaji wa timu hizo mbili.
Hii ni ishara kuwa ili timu za Tanzania zifanye vema kwenye michuano hiyo ni lazima timu iwe na wachezaji wa viwango vinavyotakiwa. Zinatakiwa zipate wachezaji wenye kusaka matokeo ambao ni hatari na si machachari.
Hapa inaonyesha kuwa gharama zinatakiwa kupata baadhi ya wachezaji wenye viwango vikubwa zaidi ya hao waliokuwapo.
Baada ya mechi hiyo, Simba inakamata nafasi ya mwisho kwenye msimamo Kundi C ambalo lina timu hizo, pamoja na Horoya AC ya Guinea na Vipers ya Uganda.
Wakati Raja Casablanca ikiwa na pointi sita, Horoya ina nne, Vipers baada ya suluhu nyumbani ina pointi moja, huku wawakilishi wa hao wa Tanzania wakiwa hawana pointi yoyote.
Kwa jinsi nilivyoiona Raja Casablanca, kama ikiamua, inaweza kushinda mechi zote sita za kundi hilo, yaani kuzifunga timu zote tatu nyumbani na ugenini. Ni timu iliyo kwenye kundi ambalo lina timu ambazo hazipo kwenye viwango vyake.
Kwa maana hiyo basi kwenye kundi hili wala haina shaka kuwa 'Waarabu' hao wameshaichukua nafasi ya kwanza na sasa timu tatu za Simba, Horoya na Vipers ndiyo wanaisaka nafasi moja iliyobaki.
Wala siidai Simba kwa lolote lile kwa kupoteza mechi dhidi ya Raja Casablanca juzi, lakini nawalaumu kwa kushindwa kushinda au kupata sare nchini Guinea ilipocheza dhidi ya Horoya kwa sababu mechi ile ilikuwa mikononi mwao.
Nadhani sasa itajifunza kitu kimoja kuwa isitegemee sana kushinda nyumbani, kama kuna uwezekano wa kupata pointi tatu ugenini zoa tu.
Wakati wengi wakiikatia tamaa Simba, binafsi naona bado timu hiyo ina nafasi na kutinga hatua ya robo fainali kama inazichanga karata zake vizuri kwenye mechi tatu mfululizo itakazokwenda kucheza.
Februari 25 itakwenda nchini Uganda kucheza dhidi ya Vipers na Machi 7, itacheza tena dhidi ya timu hiyo hiyo Uwanja wa Benjamin Mkapa, kabla ya kukutana na Horoya Machi 17 hapa hapa nchini.
Hizi ndizo mechi za Simba kucheza karata yake vizuri kwani timu inazocheza nazo ziko chini ya uwezo wao kama viongozi watafanya maandalizi mazuri na wachezaji wakacheza kwa kujituma na kuusaka ushindi kwa udi na uvumba.
Waitoe kabisa mechi ya mwisho dhidi ya Raja Casablanca nchini Morocco, ambayo sidhani kama Simba inaweza kwenda kupata hata pointi moja, ingawa kwenye soka lolote linaweza kutokea.
Simba inatakiwa kupata pointi sita dhidi ya Vipers ambapo hilo kwao linawezekana, halafu pia ina uwezo wa kupata ushindi dhidi ya Horoya na kukusanya pointi tisa.
Hapo mpinzani wake mkubwa atakuwa Horoya, ambayo sidhani kama inaweza kwenda kushinda Morocco, hivyo itabaki na pointi nne. Itarudiana tena na Raja Casablanca ambapo kwa asilimia kubwa mgeni anaweza kushinda au sare, hivyo kuwa na pointi tano.
Horoya ina uwezo wa kuifunga Vipers nchini Guinea, hivyo inaweza kufikisha pointi nane. Ikifungwa dhidi ya Simba, inamaliza ikiwa na pointi hizo na Simba itakuwa na tisa. Hayo ni mahesabu ya vidole ambayo yanaweza kuifanya Simba kutinga robo fainali na kwa viwango vya timu husika, matokeo niliyoyataja inawezekana kabisa.
Kikubwa ni Simba kujifunga kibwebwe kwa mechi tatu zilizobaki. Kufungwa au sare yoyote ni dhahiri kuwa itakuwa haina chake msimu huu kwenye michuano hiyo ambayo mara kwa mara imekuwa ikifika robo fainali.