Msimu uliopita na mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kulikuwa na malalamiko mengi kuhusu waamuzi kutokana na maamuzi yao ambayo yalionekana kuwa ya utata na ya kujirudia rudia, ambayo yalikuwa yakivikwa nguo ya 'makosa ya kibinadamu.'
Kilichoonekana ni kama waamuzi walikuwa wakishindana kufanya makosa. Huyu akikosea leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, mwingine atakosea kesho kwenye Uwanja wa CCM Kirumba. Kesho kutwa yupo mwingine atakosea Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Lindi. Ilikuwa ni kama utamaduni, huku mashabiki, wapenzi, wadau wakiwamo waandishi wa habari na wachambuzi wakipiga kelele.
Kwa mara ya kwanza nilimsikia Hamdoun akikiri kuwapo tatizo na hata alipokuwa akiongea, alionyeshwa kukerwa na hilo.
Muda si mrefu yeye na kamati yake walianza kuchukua hatua kwa kuanza kuwafungia baadhi ya waamuzi wakiwamo wale maarufu kuchezesha Ligi Kuu na mechi kubwa, wakiwa pia na beji za Fifa.
Hamdoun alisema kabisa kuwa makosa yalikuwa mengi kiasi kwamba inafikirisha kama kweli ni ya kibinadamu, kwani wamekuwa na mafunzo ya mara kwa mara, lakini wanapokwenda kuchezesha wanarudia makosa yale yale.
Kwenye mechi za mwishoni mwa mzunguko wa kwanza na wa pili wameonekana waamuzi wengi wapya vijana, wakiwa na baadhi ya wakiwamo wa zamani wachache ambao hawakuwa na majina makubwa.
Cha kushangaza ni kwamba waamuzi hawa wameonekana kuchezesha mechi mbalimbali za Ligi Kuu kwa ubora wa hali ya juu kiasi kwamba, kwa siku za karibuni hatusikii makocha, wapenzi na mashabiki wakiwalalamika.
Timu zinacheza mmoja anafungwa, wachezaji, makocha na viongozi wanakubali kuwa walizidiwa. Husikii kuwa ni mbeleko, au makosa ya waamuzi. Kwenye mitandao ya kijamii hakuna zile video fupi za makosa ya waamuzi kama ilivyokuwa zamani na hata wachambuzi sasa kwenye vipindi wanachambua mpira na wachezaji, badala ya kipindi kizima kuongelea madudu ya waamuzi.
Hamdoun mwenyewe akikaririwa hivi karibuni akisema hayo ni mapinduzi makubwa na wataendelea kulisimamia hilo.
Alisema hayo yametokana na utayari wao na kuona soka la Tanzania linasonga mbele na wamekuwa wakipokea na kuyafanyi kazi maoni ya wadau wa soka, wakiwamo waandishi wa habari na wachambuzi.
Kiongozi huyo kama akiendelea kukaa hapo kwa muda mrefu na yeye mwenyewe akaendelea na dhamira hii, soka letu linaweza kupanda tena juu, baada ya kuwa wa tano, msimu ujao na mingine Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS), linaweza kuipandisha Ligi Kuu ya Tanzania kutoka hapo ilipo na kwenda juu zaidi.
Hiki ndicho kilikuwa kilio kikubwa cha wapenzi wa soka, kwani walitaka maamuzi ya haki. Na kweli sasa yanaonekana kiasi kwamba kwa sasa kumekuwa na utani kuwa makosa ya kibinadamu yamehama kwa waamuzi na kutua kwa wachezaji.
Wana maana kuwa wachezaji wengi kwa sasa wamekuwa wakifanya makosa mengi yanayosababisha timu zao kufungwa. Makosa hayo ni kama yale ambayo waamuzi wengi waliofungiwa walikuwa wakiyafanya na baadhi ya timu hasa zile kubwa kunufaika.
Kwa wachezaji haina tatizo kwa sababu ni wao wenyewe, anafanya kosa timu yake inafungwa, baada ya hapo yeye atajuana na kocha wake. Na wakati mwingine ni lazima kosa lifanyike ili bao lipatikane.
Kilichokuwa kinawasikitisha wengi ni waliokuwa wanatakiwa kutoa maamuzi ya haki kuwa na makosa mengi ambayo yanafikirisha.
Unajiuliza hawa na sasa ambao wengi hawana hata uzoefu, ni kitu gani walichozidi kiasi cha kuchezesha vizuri?
Hata hivyo, natoa angalizo kwa Hamdoun na kamati yake kuendelea kuwakumbusha na kuwafuatilia kwa sababu waamuzi hawa pia nao ni binadamu, wanaweza baadaye wakajisahau na kuanza kufanya mambo yale yale. Lakini kwa hili Kamati ya Waamuzi wanastahili pongezi.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








