Hadi sasa, kazi inakwenda vizuri kwa maana ya kupata taarifa za mara kwa mara kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ambazo zinaonyesha kazi inakwendaje na hadi sasa kaya ngapi zimefikiwa na makarani na idadi ya watu waliohesabiwa.
Aidha, Kamisaa wa Sensa, Spika mstaafu Anne Makinda, ameonekana maeneo mbalimbali nchini akihamasisha wananchi na kutoa ufafanuzi wa mambo kadha wa kadha ambayo ni muhimu kukamilisha kazi hiyo.
Kasoro zilizojitokeza ni baadhi ya makarani kutolipwa stahiki zao na wengine kupunjwa hali iliyoleta hofu. Hata hivyo, mara kadhaa viongozi akiwamo Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Alibina Chuwa, walifafanua kuwa fedha zilipelekwa kwenye halmashauri ambako ndiko walipaswa kuwalipa makarani hao kwa wakati.
Kadiri siku zinavyokwenda, malalamiko yanazidi kujitokeza na huku wengine wakisotea fedha zao kwenye ofisi za kata au vituo maalum. Jambo hili halistahili kwa kuwa linaathiri kazi kwa ujumla wake.
Pia baadhi ya wananchi wamekataa kuhesabiwa kwa sababu mbalimbali ambazo zikifuatiliwa kwa kina ni kwamba hawajaelimishwa vya kutosha kujua kinachofanywa na serikali na kwa kiasi gani kina umuhimu kwao. Lakini wengine ni kwa sababu wana malalamiko ya muda mrefu ambayo hayajatatuliwa.
Wilayani Babati kwa mfano, kuna mwenyekiti wa kitongoji amekataa kuhesabiwa yeye na wananchi wake hadi mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu utatuliwe. Hatua hiyo ilisababisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Makongoro Nyerere, kwenda kuzungumza nao ndipo wakakubali kuhesabiwa.
Mkoani Njombe pia kuna mwananchi amegoma kuhesabiwa hadi Mkuu wa Mkoa, Anthony Mtaka, alipokwenda kuzungumnza naye akabadili uamuzi na kukubali kuhesabiwa. Hawa ni wachache walioandikwa na vyombo vya habari lakini kuna ambao wanawakataliwa makarani hadi wanalazimika kuondoka baada ya nguvu ya ushawishi kushindwa.
Hii inaonyesha bado kuna tatizo la uelewa kwa wananchi wengi na kazi kubwa ilipaswa kufanywa na wajumbe wa nyumba kumi na wenyeviti wa vitongoji na serikali za mitaa.
Naamini kama kungefanyika vikao kwenye vitongoji na mitaa kwa kushusha elimu ngazi hiyo, kwa kuwa na uwajibikaji mzuri kungesaidia sana wananchi kuelewa kinachozungumzwa na kama kuna matatizo yakafika kwenye mamlaka za juu mapema kabla ya siku husika.
Hii inaacha fundisho kwamba kunapokuwa na kampeni ya kitaifa mbinu za kutoa elimu ziwe kwa muundo tofauti tofauti, inaweza kuonekana ni wachache sana waliogomea zoezi hilo lakini kimsingi inaweka dosari.
Lililotia dosari kubwa ni makarani kutolipwa fedha zao au wengine kulipwa pungufu, yaani wamefyekwa fedha zao na watu ambao wameamua kufanya hivyo. Pia wako waliokwenda kufanya kazi kwa shingo upande kwa sababu kuna watu wamekula fedha zao. Jambo hilo si sawa kwa kuwa ni hujuma kwa kazi ya kitaifa, hivyo ni muhimu mamlaka zikafanya uchunguzi wa kina wa madai ya makarani ili kuchukua hatua.
Sensa inafanyika kila baada ya miaka 10 na inatumia fedha za Watanzania ambazo ni lazima kuwe na thamani ya fedha kwa kuwa kuliko kupoteza fedha hivyo zingeelekezwa kutatua changamoto zao za huduma muhimu za kijamii kama afya, elimu na maji.
Baadhi walisema hawaoni umuhimu wa kushiriki sensa kwa sababu wanaona hali zao za maisha hazibadiliki na wanaona fedha zinatumiwa ndivyo sivyo na baadhi ya viongozi wa serikali.
Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inaonyesha kila mwaka fedha zilivyotafunwa kwenye idara na ofisi mbalimbali za umma na wananchi wanaposikia hali zao zinazidi kuwa duni, wanaona hakuna umuhimu wa jambo fulani linapofanyika.
Hivyo ni lazima kuwe na uwajibikaji pande zote, wananchi wanapowajibika kufanyakazi na kulipa kodi, basi waliopewa dhamana nao watimize wajibu wao kwa kusimamia fedha ya umma ili ilete matokeo chanya kwa maisha ya wananchi.
Ni muhimu kuhakikisha kazi hazitolewi kwa kujuana kwamba unamjua nani au unajuana na nani au wewe ni mtoto wa nani ndio upate kazi husika, hilo likifanikiwa kutakuwa na uchaguzi wa watu wenye ujuzi sahihi kwenye majukumu yao.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







