Wanahitaji kuchunguzwa  akili kwa kuzika aliyehai

30Aug 2022
Halfani Chusi
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wanahitaji kuchunguzwa  akili kwa kuzika aliyehai

HILI halivumiliki. Ndivyo unavyoweza kusema, ukirejea tukio la wananchi wanaojidai wana hasira kali pamoja na baadhi ya wanafamilia huko mkoani Ruvuma kumwadhibu hukumu ya kifo Mzee John Komba (78), kwa kumzika akiwa hai, kwa madai ya kuhusishwa na mauaji ya mwanawe Severine Komba (34).

Uhalifu huo ulitokea katika Kijiji cha Mahanje wilayani Madaba, jambo lililosababisha wazee wengine mkoani humo kuishi kwa wasiwasi na mashaka makubwa ya kuuliwa , kama vile si watu wanaostahili kuwapo dunia.

Huu naweza kusema ni zaidi ya unyama, kukatisha uhai wa mtu kwa kusingizia mambo ambayo hayana uhakika, lakini hata kama ni ukweli sheria haimruhusu mtu yeyote kuzikwa au kuzika mwenzake akiwa hai. Wala kuhukumu kuwa ni muuaji bila kufikishwa mahakamani.

Ni siku kadhaa zimepita tangu mzee Komba afariki dunia kwa kukuzikwa hai akisababishiwa kifo na watu wanaoamini ushirikina na ambao huenda hawana imani za dini zinazokataza kuua na tena kumtendea ubaya binadamu mwenzao.

Kupitia tukio hilo Baraza la Wazee la Taifa (BWZT), pamoja na mtandao wa mashirika yanayotetea haki za wazee nchini kama  HelpAge International Tanzania, wamejitosa kukemea unyama huo.

Mwenyekiti wa Baraza, Lameck Sendo, anasema tukio hilo ni mwendelezo wa matukio ya kinyama wanayofanyiwa wazee kutokanana na imani potofu ya dhana za kishirikina.

“Tumepokea kwa masikitiko tukio la mauaji ya Mzee John Komba, aliyeuliwa kwa kuzikwa akiwa hai katika Kijiji cha Mahanje, kitendo hicho inasemekana kimefanywa na baadhi ya wananchi na wanafamilia yake, wakati wakiwa kwenye mazishi ya mtoto wake Severine Komba, wakimtuhumu mzee huyo kuwa alihusika katika mauaji ya mwanaye. Hili limeshangaza na kusikitisha.”

Anasema, mkasa huo unawakumbusha tukio jingine kama hilo lililotokea mkoani Singida, katika Kijiji cha Kisharita wilayani Iramba, ambako wazee watatu wanawake waliuawa siku moja kwa kutuhumiwa  kwa uchawi, mambo ambayo hayawezi kuthibitika.

Kitendo alichofanyiwa John Komba, ni kuvunja sheria za nchi,  katiba pamoja na kwenda kinyume na imani za dini kwa hiyo ifike mahali watu watambue kuwa uzee ni hatua katika ukuaji ambayo ni muhimu, hata watoto, vijana na yeyote ataifikia hivyo wawaheshimu hao waliozeeka.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu haikijanyamaza, ni jambo lisilovumilika, Mkurugenzi Mtendaji Anna Henga,anaeleza kuwa kitendo hicho hakikubaliki katika jamii na kuitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya wa waliohusika kutoa hukumu ya kifo kwa mzee huyo, ambaye hana hatia.

Ni ombi la kila mmoja serikali ichukue hatua kali ambazo zitakuwa funzo kwa watu wengine ambao wanajihusiha na unyama huo, hii ni ajabu watu kumzika mtu akiwa hai, si jambo zuri mwenye jukumu la kukatisha uhai wa mtu ni aliyemuumba siyo wanakijiji au familia.

Sisi tunaomba serikali ifanye hima kukomesha tabia hiyo maana sasa inaota mizizi mtu akizeeka  kidogo utasikia mchawi uzee upo hata ukiwa kijana ukifanikiwa kukaa kwa muda mrefu lazima utazeeka tena watu wanaomba kuishi na kuufikia uzee mwema, hivyo jambo hilo halikubaliki.

Jamii inapaswa kukumbuka kuwa wazee hawa ndiyo waliowalea wakiwa wadogo mpaka wamefikia umri wa kutambua baya na zuri sasa kama wanania mbaya si wangekatisha uhai wao tangu wakiwa wadogo kwa sababu kwa kipindi hicho ingekuwa raisi zaidi.

Jeshi la Polisi mkoani humo kwa kushirikiana na uongozi wa  Wilaya ya Songea akiwamo Mkuu wa Wilaya na kamati yake ya ulinzi na usalama, wanastahili pongezi kwa hatua za haraka walizozichukua ikiwamo kuwabaini na kuwakamata washtukiwa wa tukio hilo.

Ushauri wangu kwa wananchi ni vyema linapotokea tatizo kama hilo kutoa taarifa kwa polisi ili mtuhumiwa akamatwe na kuhojiwa itasaidia kubaini ukweli ulipo kuliko kujichukulia sheria mkononi kwa sababu unaweza kumuua mtu asiye na hatia kama ilivyokuwa kwa Mzee John Komba.